Baraka Mbolembole
“Labda niseme mimi nina bahati na Simba sababu kila mechi niliyochezesha kati yao na Yanga walipata ushindi. Sijawahi kuipendelea Simba na hata ukichunguza mechi zao nilizowahi kucheza nilitoa kadi nyekundu kwa wachezaji wao lakini bado wakashinda mechi (2005, fainali ya Tusker na 2007, ligi kuu ndogo)”
Aliwahi kuniambia mwamuzi niliyepata kumuhusudu sana nchini, Othman Kazi siku ya kwanza nilipoonana nae mwaka 2011.
Kazi ni mwamuzi ambaye wakati nakua nilipendezwa sana na uchezeshaji wake. Alikuwa ‘mstaarabu’ kwa wachezaji na aliweza kutoa nafasi kwa mchezaji aliyefanya makosa kujitetea, lakini daima alikuwa ‘mtu imara’ ambaye si tu aliweza kutafsiri vizuri sheria 17 za kandanda, bali namna alivyokuwa anasimamia maamuzi yake ni jambo ‘lisilo mfano.’
Kashfa ya upangaji matokeo ambayo ilimkuta wakati fulani haikunifanya nipoteze imani yangu kwake, naendelea kumchukulia mwamuzi bora zaidi Tanzania niliyepata kumshuhudia.
Siku ambayo alinipigia simu na kujitambulisha kwangu niliona ni ‘kati ya siku za bahati’ katika maisha yangu.
‘ARSENAL; MELI INAYOZAMISHWA NA ARSENE WENGER’ ilikuwa ni makala niyoandika Jumatano moja ya miezi ya mwishoni mwa mwaka 2011 katika gazeti la Dimba. Kazi alivutika sana na makala yale, hakusita kunipa pongezi. Basi kwa mara ya kwanza nikapata kuongea na ‘shujaa wangu huyu kiuchezeshaji Tanzania.’
Tulizungumza mengi, kisha akaniambia anahitaji kukutana na mimi ili tuzungumze masuala ya mpira wa miguu, nilifarijika sana kwa kweli. Ikafika siku akanikaribisha katika moja ya mikutano ya chama cha soka Kinondoni ( KIFA) na vilabu vyake.
Baada ya kumalizika kwa mkutano ule, nikiwa na rafiki yangu pamoja na Kazi, huku tukitembea, nikajikuta nikimuuliza ni kwanini harejei kuchezesha mechi za ligi kuu wakati tayari ilithibitika na vyombo vyenye mamlaka kwamba, hakuchukua rushwa na kwa maana hiyo hakuwa na hatia.
Alinitazama, Kazi ni mtu makini sana, akaniambia tutazungumza kuhusu hilo wakati mwingine. Alichokuwa ameniitia pale ni jambo lingine kabisa, aliniambia amevutiwa na vitu vingi katika uandishi wangu wa makala na alihitaji nimuandikie makala kuhusu historia ya mpira wa miguu Tanzania. Kwa namna ya masimulizi ya watu na ufahamu wangu mwenyewe.
Akaniambia madhumuni makubwa ya makala yale. Kiukweli, Kazi ni mtu mwenye mapenzi ya dhati na soka. Niliona jitihada zake kwa dhati, tulipata kwenda huku na huko kwa baadhi ya watu na kuelezea mpango uliokuwapo.
Yo te hayo ni kumbukumbu tu, lakini siku moja nikiwa nafanya kazi ya kuandika makala tuliyokusudia, tukiwa sebuleni kwake akanisimulia kila kitu kuhusu tukio lile la Bukoba, Kagera. Aliniambia kwa masharti ya kwamba ile isiwe habari bali ni mazungumzo tu kati yetu.
Nilichokuja kuelewa baada ya kupata mazungumzo yake ni kwamba, Kazi si ‘muathirika wa kwanza’ na kampeni ya ‘mabepari wa kandanda la Tanzania,’ ambao ama kwa kushirikiana na viongozi wa Chama cha Waamuzi Tanzania (FRAT,) pamoja na ushirikiano mwingine kutoka Shirikisho la soka nchini ( TFF ) ‘kuwakata’ waamuzi wenye sifa na viwango/uwezo wa kuchezesha kwa haki na kuwapa nafasi wale wasio na uwezo kwa kutokana na maslai ya watu.
Mwamuzi makini kama Kazi si rahisi kupewa nafasi kubwa na ‘mabepari’ ambao kwao ni kikwazo cha kutimiza malengo yao. Waamuzi dhaifu wamekosa ubora, na pengine matukio yao ya ‘kuvurunda’ katika uchezeshaji wao ni matokeo ya matakwa ya ‘mabwana zao’ ambao huwapa nafasi ya kuchezesha VPL, FDL hata michezo ya mashindano mengine kwa kigezo cha kufanya maamuzi yale watakayopewa na wale waliowapa nafasi.
Nilimsikia kocha wa Kagera Sugar, Adolf Richard akizungumzia tukio la kupigwa jiwe kwa mwamuzi wa game ya nusu fainali ya kombe la FA kati ya Coastal Union ya Tanga na Yanga SC. Mechi ambayo ilivunjika.
Mwalimu, Adolf alisema kwamba, miaka ya nyuma makocha walikuwa wakiwalamikia wachezaji wao na kukubali matokeo ya kupoteza mchezo wakati wa mahojiano na vyombo vya habari, lakini miaka ya karibuni kila kocha ambaye timu yake hupoteza game huelekeza lawama zake kwa waamuzi kama sababu ya kupoteza mechi.
Ni kwanini hali imekuwa hivi? Matatizo mengi ya waamuzi yanatokea katika chama chao ambacho kimekuwa kikiwaondoa wale wenye ubora na msimamo wa kukataa kutumika na kuwapa nafasi ‘watumwa wao.’
Nilishasema hapahapa kwamba, Yanga haibebwi na waamuzi na wataendelea kushinda game zao hata kama itaonekana wanabebwa, nilikuwa na maana zaidi iliyojificha. Kwanza ni kujaribu kukutoa wewe msomaji katika mtazamo wa kuamini hilo kwa maana ya kutafuta chanzo cha kwanini Yanga wanaonekana kubebwa.
Kazi alipigwa vita sana na kushutumiwa kwamba yeye ni mshabiki wa Simba, akatafutiwa sababu za kummaliza na wakafanikiwa, si tu kwamba waliharibu ndoto zake na kumaliza jitihada nyingi alizofanya wakati wa ujana wake kufikia ndoto ya kuwa mwamuzi wa kimataifa.
Kuna wakati walijaribu kumuondoa Martin Saanya eti si mwamuzi bora baada ya kukubali mkwaju wa penalti wa dakika za mwisho katika game ya VPL ( Yanga 1-1 Coastal, Septemba, 2013, uwanja wa Taifa.) Kama si wadau kupiga sana kelele kuhusu adhabu ile ya Saanya bila shaka naye angekuwa katika kapu alimotupwa Kazi.
Ngoja nikupe kisa fulani ambacho labda kinaweza kukufumbua macho. Kwanza kuna upangwaji wa matokeo wa uongozi wa timu moja na nyingine. Pia kuna upangwaji matokeo kati ya mwamuzi na timu husika, pia kuna upangwaji wa matokeo katika vyama vinavyohusika na mchezo husika na waamuzi. Pia kuna upangwaji wa matokeo ambao unaweza kuhusisha mchezaji na timu.
MWAMUZI ANAPIGWA?
Kwa kweli inauma kwa kiasi kikubwa kupoteza mechi kwa sababu tu za waamuzi, ama kwa matakwa yao wenyewe, au matakwa wanayolazimishwa ama kwa kushindwa kutafsiri kwao sheria 17 za soka na kuzisimamia.
Lakini nimejifunza ukubwa wao katika mchezo wa soka na waogope sana waamuzi kuliko mtu mwingine yeyote yule katika mchezo wa kandanda. Mimi napenda kuwaita ‘MABOSI WA DAKIKA 90.’ Ndani ya saa moja na nusu ambayo mwamuzi wa kandanda husimamia mchezo, tambua hakuna aliye juu yake, hata rais wa FIFA.
Akitaka kuharibu mechi ataharibu. Nilisema wiki iliyopita kwamba Yanga SC haibebwi na waamuzi, bali inajibeba yenyewe kwa mbinu zake. Pia nilisema wataendelea kushinda game zao. muhimu hata katika ‘muenekano wa kubebwa’ na waamuzi wanaolazimishwa na baadhi ya watu.
Katika nchi hii ambayo Leonel Messi na Cristiano Ronaldo wanaonekana wachezaji wa kawaida tu, FC Barcelona haitajwi kama timu bora zaidi duniani ya kandanda (tangu kuanza kwa karne ya hii 21) si rahisi shabiki wa kandanda asiye shabikia Yanga kusema, ‘Yanga ni bora zaidi kwa sasa nchini.’
Achana na kikosi chao cha bei mbaya, ubora na uwezo wa mchezaji mmoja mmoja, benchi la ufundi na utulivu klabuni umechagiza matokeo yao mazuri. Kwa miezi 12 sasa ni timu 3 tu zimeweza kuishinda Yanga (Azam FC 2-1 Yanga, Ndanda SC 1-0 Yanga-game za mwisho msimu uliopita katika VPL, Coastal 2-0 Yanga-VPL msimu huu.)
Hiki ni kielelezo tosha kwamba, Yanga wako vizuri ndani ya uwanja. Ukitambua hilo ndio unapaswa utafute sababu za kubebwa kwao. Jamani, Coastal wana ubora gani hasa wa kuitoa Yanga katika michuano kama hii ambayo wanatambua hata ushindi wa penati unawapa nafasi ya kufuzu kwa michuano ya CAF.
Yanga malengo yao ni kushinda VPL na FA, wakati Coastal kupitia kocha wao Ally Jangalu amewahi kusema kuwa ushindi dhidi ya Mtibwa Sugar katika 16 ya FA na ule dhidi ya Simba katika robo fainali ungekuwa na maana kama wangeupata kwenye VPL kwasababu ungewaongezea pointi katika VPL ambako wanaburuza mkia.
TFF inapaswa kuwachukulia hatua wale wote ambao wamechangia kupigwa jiwe kwa mwamuzi wa pembeni katika game kati ya Coastal na Yanga. Hata kama mchezaji atafunga goli la mkono, kama mwamuzi hajaona ni goli tu, hata kama mwamuzi hatapuliza filimbi ya offside katika mazingira yanayoonesha mfungaji yuko offside, mwamuzi akipeta ni goli tu.
Mwamuzi ndiye ‘bosi’ wa mpira wa miguu, jifunzeni kuwaheshimu. Mwamuzi hapigwi katika nyakati hizi, ni makosa makubwa na kama watabainika ni watimu fulani, timu hiyo ipewe adhabu ya kucheza bila mashabiki katika game zake za nyumbani.



0 comments:
Post a Comment