STORI: DUSTAN SHEKIDELE, WIKIENDA
MOROGORO: Mzozo mkali umeibuka kati ya baba aliyejulikana kwa jina la Shukuru Muhome na mama wa mtoto wake, Amilieth Temo ambao wanadaiwa kugombea maiti ya mtoto wao, David (8) kwa sababu ya utofauti wa dini.
Tukio hilo lilitokea wiki iliyopita mjini hapa ambapo kabla ya kukutwa na umauti, David alikuwa akisoma darasa la pili katika Shule ya Msingi Msingisi iliyopo wilayani Gairo mkoani hapa. Kufuatia mzozo huo, mwili wa David ulikaa mochwari kwa zaidi ya siku sita kwenye Hospitali ya Mkoa wa Morogoro baada ya mama wa mtoto huyo kwenda Mahakama ya Wilaya ya Morogoro kupinga mwanaye kuzikwa kwa dini ya baba yake ya Kikristo akitaka azikwe kwa dini yake ya Kiislamu.

Shukuru Muhome na Amilieth Temo pamoja na mtoto wao marehemu David.
Kesi hiyo namba 11/2016 ilirindima kwenye mahakama hiyo kwa siku tatu ambapo Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Alisile Mwankesela alisikiliza madai ya pande zote kisha kutoa hukumu ya kesi hiyo ambapo baba wa mtoto huyo alikabidhiwa mwili wa mwanaye huyo akazike. Hakimu huyo alisema kuwa mahakama iliridhika na utetezi wa wakili wa mlalamikiwa (baba) ambaye alipangua hoja zote za mlalamikaji.
Ilielezwa mahakamani hapo kuwa, mlalamikaji alidai kuwa, kiimani kama wazazi hawajafunga ndoa, mtoto ni mali ya mama.
Ilielezwa mahakamani hapo kuwa, mlalamikaji alidai kuwa, kiimani kama wazazi hawajafunga ndoa, mtoto ni mali ya mama.

Wanafamilia wakijadiliana jambo.
Katika hoja ya pili, mlalamikaji alidai baada ya kutengana na mzazi mwenzake huyo na yeye kubadili dini na kuolewa na mwanaume mwingine, baba wa mtoto huyo hajawahi kupeleka matunzo kwa mtoto na kwamba mtoto huyo alikuwa akilelewa na babu yake. Hakimu huyo alisema kuwa mahakama ilikubaliana na hoja ya wakili wa mlalamikiwa kuwa mtoto huyo alikuwa bado mdogo.
Shukuru Muhome.
Pia hakimu huyo aliongeza kuwa kwa mila za Kabila la Kikaguru ambalo ni kabila la wazazi wote wa marehemu zinasema mtoto ni mali ya baba huku akiweka wazi kuwa kama kuna upande haujaridhika basi unaruhusiwa kukata rufaa ndani ya siku 30.
Akizungumza na Wikienda baada ya hukumu hiyo, baba wa marehemu, Shukuru alisema anaishukuru mahakama kwa kutenda haki.
Alisema: “Mimi na Amilieth tulikuwa wachumba na kubahatika kupata mtoto mmoja (David), nikiwa kwenye harakati za kutaka kufunga naye ndoa aliniacha na kubadili dini kutoka Ukristo na kuwa Muislamu kisha akaolewa na mwanaume wa dini hiyo.
“Kwa kuwa mtoto alikuwa mdogo, mama yake alimchukua na kumpeleka kwa baba yake (babu mzaa mama wa David).
“Wiki mbili zilizopita, mwanangu aliugua sana, nikaenda kumchukua na kumpeleka hospitalini lakini kwa bahati mbaya Mei 6, mwaka huu akafariki dunia.”
Ijumaa iliyopita, mwili wa David ulisafirishwa kwenda kijijini Msingisi, Gairo kwa mazishi.



0 comments:
Post a Comment