………………………………………………………………………………………………………..
Na Veronica Kazimoto
26 Mei, 2016.
BENKI
ya Dunia imeahidi kuendelea kuisaidia Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS)
kifedha ili iweze kutekeleza majukumu yake ya utoaji wa Takwimu Rasmi
nchini.
Akizungumza
leo alipotembelea Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Mkurugenzi Mkazi wa Benki
ya Dunia hapa nchini Ms. Bella Bird amesema kutokana na umuhimu wa
takwimu katika kupanga na kupima matokeo ya utekelezaji wa miradi
mbalimbali ya kimaendeleo, Benki ya Dunia itaendelea kuisaidia NBS ili
iendelee kutekeleza majukumu yake ikiwa ni pamoja na kutoa takwimu kwa
wakati.
“Ili
Ofisi ya Taifa ya Takwimu iweze kutoa takwimu kwa wakati, inahitaji
kuwekeza katika matumizi ya technolojia ya kisasa ya ukusanyaji wa
takwimu, hivyo Benki ya Dunia itaendelea kutoa msaada wa kiufundi na
kifedha ili kufikia malengo yaliyoainishwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu
ya utoaji wa takwimu rasmi nchini”, amesema Ms. Bella Bird.
Mkurugenzi
huyo Mkazi amefafanua kuwa Benki ya Dunia inatambua umuhimu wa takwimu
katika maendeleo ya nchi zote duniani ikiwemo Tanzania katika kupanga
sera na kutekeleza miradi mbalimbali ya nchi husika.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina
Chuwa ameishukuru Benki ya Dunia kwa misaada mbalimbali ambayo imekuwa
ikiisaidia Ofisi ya Taifa ya Takwimu ambayo imeongeza tija katika
ukusanyaji na utoaji wa takwimu rasmi nchini.
“Napenda
kuchukua fursa hii kuishukuru Benki ya Dunia kupitia ujio wako
kuitembelea Ofisi ya Taifa ya Takwimu na kujionea shughuli mbalimbali
zinazofanywa na ofisi hii ikiwa ni pamoja na ukusanyaji na utoaji wa
takwimu rasmi hapa nchini,” amesema Dkt. Chuwa.
Dkt.
Chuwa amesema Ofisi ya Taifa ya Takwimu imeendelea kupanua wigo wa
uzalishaji wa takwimu nchini ikilinganishwa na karne zilizopita.
Benki
ya Dunia inaisaidia Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kutoa ushauri wa
kitalaam pamoja na fedha kupitia Mpango Kabambe wa Kitaifa wa Kuboresha
na Kuimarisha Takwimu nchini ambapo awamu ya kwanza itakamilika mwezi
Juni, 2018.


0 comments:
Post a Comment