………………………………………………………………………………………………………………….
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt John Pombe Magufuli
amewataka wakandarasi nchini kujiepusha na vitendo vya rushwa ili
kulisaidia Taifa kupiga hatua ya kimaendeleo.
Mhe.
Rais Magufuli ameyasema hayo leo wakati akifungua Mkutano wa
Mashauriano wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi nchini (CRB) uliofanyika
jijini Dar es Salaam.
“Mnaweka
viwango vikubwa vya fedha kwenye miradi ili muweze kupata fedha ya
kutoa rushwa, kwa nini mnafanya hivyo?”amewauliza Mhe. Rais Magufuli na
kuwambia kuwa kama wapo watumishi wa serikali wanaowaomba rushwa ili
wapate kazi waitaarifu Takukuru mara moja ili wachukuliwe hatua.
Mhe.
Rais amewataka wakandarasi wazawa wajipange kufanya kazi na kuwaonya
wasiwe wanaweka viwango vikubwa ambavyo vinachangia kuwakosesha zabuni.
Akitoa
mfano, Mhe. Magufuli alisema katika ujenzi wa mahakama za mwanzo hapa
nchini, jengo moja lilikadiriwa kukamilika kwa milioni 200 lakini
wakandarasi wa Tanzania walioomba zabuni hiyo walitoa kiwango cha kati
ya shilimgi milioni 670 na bilioni 1.4. Amesema kwa jinsi hii hata mtu
awe na huruma ya namna gani hawezi kuwapa kazi.
Amesema
serikali yake itawajali kwanza wakandarasi wa hapa nchini lakini
akawataka wajipange na pengine waungane ili kufanya kazi kwa pamoja.
Aidha,
Mhe. Rais amesema ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima, Uganda hadi
Tanzania unakaribia kuanza lakini akauliza wakandarasi wa hapa nchini
wamejipangaje katika kushiriki ujenzi huo.
Kuhusu
ulipaji wa madeni ya wakandarasi, Mhe Rais amesema, serikali yake
imekuwa ikilipa madeni hayo na itaendelea kufanya hivyo hadi deni
litakapoisha. Amesema kwa kuanza serikali imelipa bilioni 650 na baadaye
ikatumia bilioni 462 kutoka Mfuko wa Barabara kuwalipa wakandarasi.
Amesema
wakandarasi ni watu wa muhimu sana katika maendeleo ya Taifa na ni
injini ya maendeleo kwani wako kila sekta ya maendelo. Amesema kwa
mfano wako katika ujenzi wa mioundombinu, kwenye zana za kilimo,kwenye
uvuvi, na pia usafirishaji wakandarasi hawakosekani.


0 comments:
Post a Comment