Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akizungumza na
wafanyakazi wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), na wadau wa Sekta ya
Mawasiliano (hawapo pichani), wakati uzinduzi wa nembo mpya ya kampuni
hiyo na huduma ya 4G LTE jijini Dar es Salaam.
Mjumbe wa
Bodi ya Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Bi. Edwina Lupembe akifafanua
jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame
Mbarawa, katika hafla ya uzinduzi wa nembo mpya ya kampuni hiyo na
huduma ya 4G LTE
Afisa
Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Dkt. Kamugisha Kazaura
akielezea mafanikio ya TTCL kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (hayupo pichani), katika hafla ya
uzinduzi wa nembo mpya ya kampuni hiyo na huduma ya 4G LTE jijini Dar es
Salaam.
Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akizindua nembo
mpya ya Kampuni ya Simu ya Tanzania (TTCL), jijini Dar es Salam.
Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akijadiliana
jambo na Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Dkt.
Kamugisha Kazaura, wakati wa halfla ya uzinduzi wa nembo mpya ya kampuni
hiyo na huduma ya 4G LTE jijini Dar es Salaam.(P.T)
Baadhi ya
Wafanyakazi wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), wakifatilia sherehe za
uzinduzi wa nembo mpya ya kampuni hiyo na huduma ya 4G LTE jijini Dar es
Salaam.
Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amewataka
wafanyakazi wa Kampuni ya Simu ya (TTCL), kuwa wabunifu ili kuhimili
ushindani wa soko katika sekta ya mawasiliano na hivyo kuiwezesha
kampuni hiyo kupata faida.
Akizungumza
wakati akizindua nembo mpya ya kampuni ya TTCL na huduma ya 4G LTE
inayowezesha huduma ya mawasiliano ya sauti na data kwa haraka Prof.
Mbarawa amesema huu ni wakati wa kubadili mtazamo na kufanya kazi kisasa
ili kuvutia wananchi kutumia huduma za TTCL.
“TTCL
lazima mubadilike ili muweze kuendana na kasi ya mabadiliko ya sayansi
na teknolojia na hivyo kumudu ushindani uliopo sasa katika sekta ya
mawasiliano”, amesema Waziri Prof. Mbarawa.
Amewataka
TTCL kuhakikisha kituo mahiri cha kutunzia taarifa (Data Centre),
kinaanza mapema mwezi Juni ili kuwezesha wadau wengi kunufaika na kituo
hicho.
Prof.
Mbarawa amesema Serikali inaunga mkono TTCL na imetenga masafa ya 800
MHZ ambayo yataiwezesha TTCL kushindana na makampuni mengine ya watoa
huduma ya mawasiliano na kuwaunganisha wateja wengi kutumia huduma za
mawasiliano na data.
“Uzinduzi
wa nembo mpya ya TTCL na huduma ya masafa ya 4G LTE uendane na ubunifu
kwa wafanyakazi ili muwavutie watumiaji wengi wa simu na hivyo kupata
soko kubwa na kuifanya TTCL kuchangia kikamilifu pato la taifa”,
amesisitiza Waziri Mbarawa.
Prof.
Mbarawa amesema mawasiliano ni kiungo muhimu cha kufanikisha ukuaji wa
sekta za kilimo, taasisi za fedha, uwekezaji, ujasiliamali na utendaji
kazi wa Serikali na sekta binafsi hivyo ubunifu katika utendaji
utaiwezesha TTCL mpya kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Katika
hatua nyingine Prof. Mbarawa amewataka wananchi kuzingatia maelekezo
wanayopatiwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kuhusu namna ya
kuzitambua simu na vifaa feki na hatua za kufuata ili ifikapo Juni 16
zoezi la kuzifunga simu feki litakapotekelezwa wasiathirike.
Kwa
upande wake Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL Bi. Edwina Lupembe
amesisitiza kwamba TTCL imejipanga kuboresha huduma za fedha ili
kuwezesha watumiaji wengi wa kampuni hiyo kunufaika na huduma ya kutuma
na kupokea fedha.
“Tumekamilisha
mradi mkubwa wa kusimika mitambo ya GSM, UMTS na LTE ambayo itakuwa na
uwezo wa kutoa huduma ya mawasiliano 2G, 3G na 4G”, amesema Bi. Lupembe
Naye
Afisa Mtendaji Mkuu wa TTCL Dkt. Kamugisha Kazaura amemhakikishia Waziri
Mbarawa kuwa mabadiliko ya muonekano wa TTCL yataendana na mtazamo mpya
wa wafanyakazi wenye lengo la kuiwezesha kampuni hiyo kuwa ya kisasa
hapa nchini.
Amesema
TTCL imejipanga kuboresha simu za mezani, mkononi, na huduma za intaneti
ya haraka ili iweze kupata wateja wengi na hivyo kuongeza mapato yake.
“Teknolojia
ya 2G GSM, 3G UMTS na LTE imeongeza nguvu kwa kampuni yetu kuleta
ushindani katika soko la mawasiliano na zitaendelea kuongeza ufanisi na
ubunifu wa huduma zetu kwa bei nafuu”, amesisitiza Dkt. Kazaura.
Tayari huduma ya 4G LTE inapatikana katika maeneo mengi ya Ilala, Temeke na Kinondoni jijini Dar es Salaam.


0 comments:
Post a Comment