………………………………………………………………………………………………………
Na. Aron Msigwa- DODOMA.
Serikali imesema kuwa itaendelea
kuboresha maslahi ya askari wa Jeshi la Polisi na kuwajengea nyumba za
kisasa za kuishi ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri
Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Luhaga Mpina wakati
akijibu maswali ya wabunge kuhusu mkakati wa Serikali wa kuboresha
maslahi ya Askari wa Jeshi hilo kwa niaba ya Naibu Waziri wa Mambo ya
Ndani ya Nchi Bungeni mjini Dodoma leo
Amesema kuwa Serikali katika
mwaka wa fedha 2016/2017 itatekeleza Mpango kabambe wa ujenzi wa nyumba
za Polisi 4136 ambao utakwenda sambamba na ujenzi wa vituo vya Polisi.
Amesema Serikali imechukua hatua
za haraka kulishughulikia suala la ukosefu wa nyumba za askari hao
katika maeneo mbalimbali nchini ili kuimarisha ulinzi na usalama katika
maeneo yenye ukosefu wa nyumba hizo.
Amelieleza Bunge kuwa Serikali
imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha kuwa maslahi ya
Askari Polisi yanaimarishwa ikiwemo malipo ya Posho ya pango kwa askari
wasio na nyumba ambayo ni asilimia 15 ya mishahara yao ili waweze
kulipia gharama hizo.
Ameongeza kuwa askari wenye
utalaam maalum wakiwemo madereva na madaktari wamekuwa wakilipwa posho
ya asilimia 15 ya mishahara yao na kuongeza kuwa askari wanaoajiriwa
katika ajira mpya kama madaktari wamekuwa wakilipwa mishahara sawa na
madaktari wengine bila kujali vyeo vyao.
“Serikali tumefanya jitihada
kubwa sana kuboresha maslahi ya askari wetu, kama Serikali tumetoa posho
za nyumba, posho za utalaam maalum kwa askari wote ambayo ni asilimia
15 ya mshahara wa kila Polisi hii yote ni kuwafanya askari wetu waweze
kumudu gharama za maisha” Amesisitiza Mhe. Mpina.
Ameeleza kuwa kwa askari
wanaofanya kazi katika mazingira magumu wakiwemo wa Kikosi cha Kutuliza
Ghasia (FFU) wamekuwa wakipewa posho ya kufanya kazi katika mazingira
magumu (Hardship allowance) kiasi cha shilingi laki moja (100,000) kila
mwezi.
Mhe. Mpina amebainisha kuwa
askari wote wanaohitimu mafunzo yao wamekuwa wakikatiwa Bima ya Afya kwa
asilimia 100 na Serikali pamoja na udhamini wa mikopo mbalimbali katika
taasisi za kifedha ili waweze kupewa mikopo na taasisi hizo.
Aidha, amesisitiza kuwa serikali
imewapandishia kiwango cha Posho ya katikati ya mwezi (Ration Allowance)
kutoka shilingi 180,000 za awali hadi 300,000 ambazo wanalipwa kwa sasa
nchi nzima.
Katika hatua nyingine Wizara ya
Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imetoa ufafanuzi kuhusu vijana wa
kidato cha nne kutochukuliwa kujiunga na Mafunzo ya Jeshi la Kujenga
Taifa (JKT).
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la
Kujenga Taifa Dkt. Hussein Mwinyi amesema kuwa hatua ya kuwachukua
vijana wote wanaomaliza kidato cha nne kwa sasa haiwezekani kutokana na
uwezo mdogo wa kifedha wa Serikali.
Amesema kuwa uwezo wa JKT
kuchukua vijana wa kujitolea kwa sasa ni 5000 hadi 7000 kwa mwaka
kulingana na bajeti inayotolewa na kuongeza kuwa mpango wa Serikali ni
kuendelea kutenga fedha na kujenga kambi zaidi za mafunzo ili
kuwawezesha vijana wengi kujiunga na mafunzo hayo kulingana na
upatikanaji wa fedha.
Kwa upande wa wahitimu wa kidato
cha sita wanaotakiwa kujiunga na JKT kwa mujibu wa Sheria Mhe. Mwinyi
amesema Serikali imewachukua vijana 14,000 na inaendelea kujenga uwezo
wa ndani wa kuchukua vijana wengi zaidi.
Amesema Serikali inakusudia
kujenga majengo ndani ya makambi ili kuwezesha vijana wote wanaohitimu
kidato cha sita kupitia JKT kabla ya kujiunga na vyuo mbalimbali hapa
nchini.
Aidha, Amefafanua kuwa kwa wale
wanaojiunga na JKT kwa kujitolea ambao idadi yao inafikia 5000 sio wote
wanaopata nafasi ya kuajiriwa katika vyombo vya Ulinzi na Usalama na
kuongeza kuwa ni asilimia 71 ndio hupata ajira kwenye vyombo hivyo huku
waliobaki wakilazimika kurudi nyumbani.
Amebainisha kuwa Serikali kupitia
Ofisi ya Waziri Mkuu inaangalia utaratibu wa kuwawezesha vijana hao ili
wanaporudi uraiani waweze kupatiwa mitaji ya kuwawezesha kujiajiri
wenyewe.


0 comments:
Post a Comment