MAMLAKA
ya Mapato Tanzania (TRA) imesema kupungua kwa mizigo bandarini
kumeathiri si Tanzania pekee bali dunia nzima na kwamba kubanwa kwa
mianya ya wizi kumesababisha kuongezeka kwa mapato kutoka Sh bil 458
Aprili mwaka huu kufikia Sh bil 517.
Aidha,
TRA imesema itaanza uhakiki wa namba za utambulisho wa mlipakodi (TIN)
kutokana na kuwepo watu wenye namba mbili na wasiohakiki watalazimika
kudaiwa kodi na TRA.
Akizungumza
katika mkutano na wanahabari jana, Kamishna wa TRA, Alphayo Kidata
alisema upungufu huo wa mizigo bandarini umezikumba pia bandari za
Beira, Msumbiji, Mombasa, Kenya na kwingineko na kusababisha mapato
kupungua.
“Lakini
sisi pamoja na upungufu wa mizigo bandarini makusanyo yanazidi
kuongezeka kutokana na kuzibwa mianya ya kukwepa kodi, hivyo napenda
kuwapongeza wafanyakazi wote wa mamlaka na kusema kwa sasa hakuna mtu
anayeweza kukwepa kodi na wale waliozoea wakae katika njia kuu,” alisema
Kidata.
Kidata
alisema wananchi wanatakiwa kuwaunga mkono kwani sasa kodi inaonekana
katika kufanya shughuli za serikali kama kuboresha miundombinu pamoja na
kutoa elimu bure.
Alisema
TRA imefikia na kuvuka lengo la makusanyo ya kodi kwa mwaka wa fedha
2015/16 kwa kukusanya Sh trilioni 13.8 sawa na asilimia 100.04 ya lengo
la kukusanya Sh trilioni 13.4 iliyokuwa imepangwa na serikali.
Kidata
alisema katika kipindi cha Juni mwaka huu, TRA imekusanya Sh trilioni
1.4 sawa na asilimia 107.83 ya lengo la kukuzanya Sh trilioni 1.3 ambapo
makusanyo ya mwaka wa fedha 2015/16 ni sawa na ongezeko la asilimia
23.70 la makusanyo ya mwaka 2014/15.
Akizungumzia
mashine za kielektroniki za EFDs, Kidata alisema walipoanza utoaji
mashine hizo zilikuwa 5,703 na mpaka sasa mashine 1,700 zimegawiwa kwa
watumiaji na wataanza kupita duka hadi duka kuhakiki matumizi ya mashine
hizo.
Kamishna
wa mapato ya ndani, Elijah Mwandumbya, alisema mwaka huu wa fedha
wamejipanga kuhakikisha wanaondoa changamoto kwa mtu mmoja kuwa na TIN
zaidi ya moja hivyo watafanya uhakiki.
0 comments:
Post a Comment