Mahakama
Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imemtaka Gavana wa Benki Kuu (BoT) Benno
Ndulu, na Mwendeshaji wa benki ya FBME, Lawrence Mafuru, wafike
mahakamani kujieleza jinsi watakavyotekeleza amri iliyoitaka BoT kulipa
Sh bilioni 92.
Maofisa
hao wanatakiwa kuieleza mahakama watakavyoilipa kampuni ya Coast
Textiles Ltd fedha hizo na kama watashindwa kufanya hivyo, watafungwa
jela kama wafungwa wa kesi ya madai.
Utekelezaji
wa amri hiyo unatokana na uamuzi wa shauri namba 129 la mwaka 2009,
ulioiamuru benki ya FBME kuilipa kampuni ya Coast Textiles Ltd fedha
hizo baada ya kukamata kiwanda chake na kukiuza kwa kampuni ya Five Star
Investment ltd.
Uuzwaji wa kiwanda hicho ulitokana na mgogoro wa ulipaji mkopo ambao kampuni ya Coast iliuchukua katika benki hiyo.
BoT
inahusishwa kwenye shauri hilo kutokana na kuchukua uendeshaji wa benki
ya FBME baada ya benki hiyo kuhusishwa na utakatishaji fedha nchini
Cyprus.
Maofisa
hao walitakiwa kufika mahakamani hapo Septemba 16 mwaka huu kwa ajili
ya kueleza jinsi watakavyotekeleza amri hiyo, lakini hawakufika kwa kuwa
wamewasilisha maombi ya kusimamisha shauri hilo ambayo yamepangwa
kusikilizwa leo mbele ya Jaji Ama Munisi.
Katika
kesi ya msingi iliyofunguliwa na kampuni ya Coast, mahakama iliamuru
FBME iilipe kampuni hiyo Sh bilioni 21.2 na riba ya asilimia 21 kwa
mwaka tangu Juni 28, 2001 hadi hukumu ilipotolewa, Julai 27, 2015.
Baada
ya uamuzi huo, walalamikaji walipeleka maombi ya utekelezwaji wa hukumu
hiyo, ambayo ukijumlisha na riba ni sawa na Sh bilioni 92.2.
Kutokana
na maombi hayo, mahakama ilimuelekeza Gavana wa BoT kukamata akaunti
mbili zinazomilikiwa na benki ya FBME, hata hivyo BoT iliwasilisha
maombi ya kuchunguzwa kwa umiliki halali wa akaunti zinazoshikiliwa na
kuiomba mahakama isitishe amri hiyo kwa kuwa BoT siyo miongoni mwa
walalamikiwa kwenye shauri la msingi.
BoT
iliingilia kati suala hilo, kwa kuwa kwa sasa ndiyo inayosimamia
uendeshwaji wa benki ya FBME kwa ajili ya kulinda amana za wateja baada
ya benki hiyo kuhusishwa na utakatishaji fedha.
Baada
ya kusikiliza maombi hayo, mahakama iliondoa amri hiyo na kuamuru benki
hiyo ilipe fedha, hata hivyo walalamikaji waliwasilisha maombi mengine
ya kukazia hukumu katika Mahakama Kuu.
Katika
maombi hayo Msajili wa Mahakama Kuu, Projest Kahyoza alitoa siku saba
kwa maofisa hao kufika mahakamani kujieleza jinsi watakavyolipa fedha
hizo na wakishindwa watafungwa jela kama wafungwa wa madai.
0 comments:
Post a Comment