Hatimaye Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza leo imetoa uamuzi wa kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa Ubunge uliompa ushindi Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya (Chadema) dhidi ya Spephen Wassira (CCM).
Kesi hiyo ya kupinga matokeo ya uchaguzi ilifunguliwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, lakini ilikuwa inasikilizwa mjini Musoma, Mkoani Mara.
Mahakama hiyo imeeleza kutoridhishwa na ushahidi wa kupinga matokeo hayo uliowasilishwa na upande wa walalamikaji, hivyo imemthibitisha Bulaya kuwa mbunge halali wa jimbo hilo.
Kesi ya kupinga matokeo hayo ilifunguliwa na wananchi wanne ambao ni wafuasi wa Wassira ambaye alikuwa mbunge wa jimbo hilo kabla ya kuondolewa kupitia uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka jana.
Katika kesi ya msingi, walalamikaji ambao ni wakaazi wa Bunda walidai kuwa uchaguzi haukuwa huru na haki kwakuwa uligubikwa na vitendo vya rushwa, mgombea wanaemuunga mkono kunyimwa fursa ya kuhakiki matokeo pamoja na kuongezeka kwa idadi ya vituo vya kupigia kura visivyo halali.
Katika kesi hiyo, Bulaya alitetewa na mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu.
0 comments:
Post a Comment