NI KUFUATIA OMBI LA KAIMU RC WA DAR ES SALAAM ALLY HAPI
NI ZILE ZILIZO NJE YA UTARATIBU WA KISHERIA
Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa amefuta posho
zote ambazo hazipo kwa mujibu wa sheria, kwa watumishi na madiwani wa
halmashauri zote nchini.
Miongoni
mwa Posho zilizofutwa kuanzia mwezi huu, ni pamoja na posho ya
vitafunwa, posho ya mazingira magumu ya kazi kwa wakuu wa idara, posho
za kuchochea maendeleo na kujengewa uwezo zinazolipwa binafsi kwa
madiwani na aina nyinginezo zote ambazo kisheria hazipaswi kuwepo na
kuwataka wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha fedha hizo zinapelekwa
kwenye miradi ya maendeleo.Maamuzi hayo yametolewa leo jijini Dar es
salaam wakati Waziri Mkuu alipokutana na watumishi wa manispaa ya
Kigamboni, wakati alipofanya ziara ya siku moja kutembelea wilaya hiyo
mpya mkoani humo.
Mh.
Waziri Mkuu amefikia maamuzi hayo baada ya kuombwa na Kaimu Mkuu wa Mkoa
wa Dar es salaam ALLY HAPI kuangalia uwezekano wa kuzifuta posho ambazo
hazipo kwenye utaratibu wa kisheria, na kuelezea kuwa halmashauri za
mkoa wa Dar es salaam zilikuwa zinatenga na kulipa zaidi ya shilingi
bilion 4.5 kwa mwaka kwa ajili ya posho za vitafunwa, mazingira magumu
ya kazi, kujengewa uwezo n.k. fedha ambazo amependekeza zinaweza
kusaidia kujenga madarasa zaidi ya 250 ya sekondari kwa mwaka mmoja ili
kuziba upungufu wa vyumba vya madarasa na kuwapa nafasi wanafunzi
waliofaulu na kukosa nafasi kupata elimu.
"Amesema
hapa Kaimu Mkuu wa Mkoa Hapi, kuwa kuna utaratibu wa kulipana posho
zilizo nje ya utaratibu wa kisheria kwenye manispaa...Naagiza kuanzia
Januari hii posho hizo zisilipwe na nimezifuta rasmi. Mkurugenzi yeyote
atakayelipa atakua amejiandalia mazingira ya kupoteza nafasi yake..."
Amesema Waziri Mkuu.
Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania KASSIM MAJALIWA pia amewataka
watumishi wa umma nchini, kuwajibika kwa mujibu wa majukumu ya kazi zao
na kuachana na utamaduni wa njoo kesho.
Kuhusiana
na watumishi kumi waliohamishiwa kwenye halmashauri ya manispaa ya
Kigamboni na kushindwa kuripoti, waziri mkuu ametoa siku tatu kwa
watumishi hao kufika vituo vyao vya kazi.
Mkuu wa
Wilaya ya Kigamboni, Hashim Mgandilwa amemuomba waziri mkuu
kushughulikia changamoto ya kimamlaka inayoikabili wilaya hiyo, kutokana
na kuwepo Mamlaka ya Uendelezaji Mji wa Kigamboni KDA inayomiliki
asilimia 12 ya ardhi, na Manispaa inayomiliki asilimia 88 ya ardhi yote.
Naye
Mbunge wa Kigambon Dk Faustine Ndungulile, amemuomba waziri Mkuu
kushughulikia changamoto zinazowakabili wakazi wa Kigamboni wanaotumia
daraja la Nyerere, ambazo miongoni mwake ni foleni za magari na gharama
kubwa ya tozo kwa mabasi ya abiria yanayotumia daraja hilo .
0 comments:
Post a Comment