FAINALI za Kombe la Mataifa ya Afrika au Afcon 2015 zinaanza rasmi leo huko Guinea ya Ikweta.
Awali fainali za michuano hii inayoandaliwa na
Shirikisho la Soka Afrika (CAF) zilipangwa kufanyika Morocco lakini
wenyeji hao wakaamua kujitoa na ndipo Guinea ya Ikweta ilipokabidhiwa
jukumu la kuwa mwenyeji.
Kumekuwa na habari kubwa ambayo imetawala katika
fainali za mwaka huu ambazo zitafikia ukomo mapema mwezi ujao kwamba
hazitakuwa na mvuto.
Moja ya sababu inayotajwa kuchangia fainali
kutokuwa na mvuto ni kitendo cha mwenyeji wa awali Morocco kujitoa kwa
madai ya kuhofu maambukizi ya Ugonjwa wa Ebola.
Baada ya Morocco kujitoa ziliibuka dhana kwamba
huenda fainali za mwaka 2015 zisifanyike kutokana na hofu ya maradhi
hayo ambayo tayari yamesababisha vifo vya watu zaidi ya 8,000 wengi wao
wakiwa ni kutoka nchi za Afrika Magharibi.
Hata hivyo, kwa Watanzania hasa waliopewa dhamana
ya soka dhana ya mashindano kukosa mvuto ni dhana ambayo inakosa nguvu
hasa kutokana na ukweli kwamba Tanzania ina zaidi ya miaka zaidi 30
haijashiriki fainali za Afcon.
Mara ya kwanza na ya mwisho Tanzania kushiriki
fainali hizi ilikuwa ni mwaka 1980 nchini Nigeria wakati huo mashindano
haya yakijulikana kama fainali za Mataifa Huru ya Afrika.
Ni wakati ambao Afrika Kusini ilikuwa hairuhusiwi
kushiriki kutokana na sera za ubaguzi wa rangi zilizokuwa zikitumika
nchini humo.
Watanzania walio na mapenzi ya soka ni wazi kwamba
wamekuwa na shauku ya kuona siku moja Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi
shiriki kwenye Afcon.
Juhudi zimekuwa zikifanyika lakini mara zote mambo
yameendelea kuwa magumu hali ambayo imezidi kuifanya Tanzania kuwa ni
timu mshiriki wa kusaka tiketi ambaye ameshindwa kutimiza ndoto ya
kufuzu.
Tunadhani imefika wakati kwa Watanzania hasa
waliopewa dhamana kuja na mikakati ambayo itaifanya Tanzania ifuzu
fainali za Afcon 2017 ambazo awali zilipangwa kufanyika Libya lakini
hali ya kisiasa imesababisha uamuzi huo ufutwe na mwenyeji mwingine
anatarajiwa kutangazwa na CAF.
Tunaamini Tanzania inaweza kufuzu fainali hizo
kama tu kila aliyepewa dhamana atawajibika na kuzitumia fainali za mwaka
huu kuwa sababu ya kuhakikisha Tanzania inakuwa miongoni mwa timu
shiriki.
Ni vizuri kujiuliza ni kwa nini nchi kama Zambia na nyinginezo
ambazo uchumi wao si mkubwa kiasi cha kutisha zinaweza kufuzu na hata
kuchukua kombe wakati kwa Tanzania suala la kufuzu tu limeendelea kuwa
gumu kwa miaka zaidi ya 30.
Ile imani yetu kwamba katika soka la Tanzania
mipango mizuri imekosekana ndiyo jibu sahihi la kwanini Tanzania inahaha
kusaka tiketi ya Afcon kwa miaka zaidi ya 30. Mipango tunayoizungumzia
hapa itakuwa na maana kama viongozi wenye dhamana watajifunza kutoka kwa
nchi ambazo zimewahi kufuzu.
Tunaamini na tutaendelea kuamini kwamba jambo hili
likifanyika Tanzania inaweza kufuzu Afcon na kuondokana na aibu hii ya
miaka zaidi ya 30.
Na hata isipofuzu ushindani wa kusaka tiketi
utaonekana kwani kwa kipindi kirefu Tanzania mbali na kushindwa kufuzu
bado haijaweza kutoa ushindani wa kweli kwa timu inazoshindana nazo
kuwania kufuzu Afcon.

