KAMA zali vile. Simba imefanikiwa kutwaa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi baada ya kuifunga Mtibwa Sugar kwa penalti 4-3. Dakika 90 za mchezo huo zilimalizika suluhu.
Wakati mashindano hayo yalipoanza hakuna aliyeipa
Simba nafasi ya kutwaa taji hilo. Kikosi cha Simba kilionekana kuwa
hovyo. Soka lake halikuwa na mvuto na hata morali ya timu ilikuwa chini.
Hali hiyo ilisababishwa pia na kupoteza mchezo wao wa kwanza dhidi ya
Mtibwa ilipofungwa bao 1-0.
Siku zimeenda kasi na mambo yakaonekana kubadilika
ghalfa. Yanga na Azam zilizokuwa zinapewa nafasi kubwa ya kutwaa taji
hilo ziliondoshwa katika hatua ya robo fainali. Waliokuwa mabingwa
watetezi KCCA ya Uganda nayo iliondolewa katika hatua hiyo. Mwanaspoti
inakuletea baadhi ya mambo yaliyojionyesha kwenye michuano hiyo na
taswira yake kwenye mechi za Ligi Kuu Bara zinazoendelea.
Kopunovic aliisoma Simba mapema
Kocha wa Simba, Goran Kopunovic, aliipokea timu
hiyo baada ya kupoteza mchezo wake wa kwanza wa mashindano hayo ambao
aliutazama akiwa jukwaani, Simba ilipofungwa bao 1-0 na Mtibwa.
Baada ya kugundua mapungufu kadhaa kwenye mechi
hiyo, kocha huyo alituliza akili na kuwapanga wachezaji wake kwa ajili
ya mapambano. Kazi kubwa aliyoifanya ni kuhakikisha Simba inakuwa na
pumzi ya kucheza kwa dakika zote 90 jambo lililonekana kuisaidia timu.
Kopunovic pia alionekana kuwaamini wachezaji wote wa timu hiyo jambo
lililonekana kuisaidia pia. Alifanikiwa pia kupandisha morali ya timu
iliyokuwa chini na kuwapa wachezaji wake matumaini ya kupata ushindi.
Simba haikudharau timu
Simba iliingia kwenye mashindano hayo ikiwa na
hali ya hofu. Iliamini kuwa ikiteleza kidogo itakuwa vibonde wa
mashindano hayo. Kiwango kikubwa kilichoonyeshwa na Yanga kwenye mechi
za awali kilionekana kuinyong’onyeza zaidi Simba. Hali hii iliwafanya
wachezaji wa timu hiyo kucheza kwa kujiamini na kujituma zaidi.
Hawakutaka kudharau mechi na waliuchukulia kila mchezo kama fainali.
Beki ya timu hiyo chini ya nahodha, Hassan Isihaka, ilionekana kucheza
kwa umakini mkubwa. Hali hii iliisaidia Simba kujituma hadi dakika ya
mwisho na kupata matokeo.
Mexime ana kazi kwenye ushambuliaji
Mtibwa Sugar ilifanikiwa kucheza fainali yake ya
tatu ya Kombe la Mapinduzi juzi Jumanne baada ya kuwahi kucheza fainali
hizo mwaka 2008 na 2010. Kikosi cha Mtibwa kwenye mashindano hayo
kilionekana kuimarika na kucheza kwa ushirikiano mkubwa.
Mbali ya timu, uwezo wa washambuliaji wa Mtibwa ni
wa juu. Tazama majina kama Ame Ally, Mussa Mgosi, Ally Shomary, Vicent
Barnabas na Mzamiru Yassin. Ni washambuliaji wenye uwezo wa juu. Kila
mmoja anaweza kumiliki mpira, kupiga chenga na hata kufunga.
Kwa bahati mbaya Mgosi na Shomary pekee ndio
waliofunga bao moja moja kwenye mashindano hayo, wengine hawakufunga.
Mbali na hilo Mtibwa imecheza mechi sita za mashindano hayo na kufunga
mabao matatu pekee.
Hapa kuna shida. Yawezekana viungo wa Mtibwa wanashindwa
kuwachezesha vizuri mastraika hawa na kuhakikisha wanapachika mabao
mengi zaidi. Yawezekana pia mastraika hawa wanakosa umakini kidogo
katika umaliziaji wao. Maxime anatakiwa kulifanyia kazi hili.
Yanga iwe makini kwenye hesabu
Katika timu zilizoonekana kukosa hesabu kwenye
mashindano ya Kombe la Mapinduzi basi ni Yanga. Mabingwa hawa wa
kihistoria wa Bara walionekana kuwa tishio. Katika mechi mbili tu za
mwanzo walionekana kuwa tishio, walifunga mabao manane baada ya
kuzifunga Taifa Jang’ombe na Polisi Zanzibar mabao 4-0 kila mmoja. Yanga
ilifanikiwa pia kushinda mchezo wa mwisho na kujikita kileleni mwa
kundi lao. Katika hali ya kushangaza Yanga ilijikuta ikikosea hesabu.
Ilishindwa kucheza kwa kasi na umakini katika mechi yao ya robo fainali
tofauti na ilivyofanya kwenye mechi za awali. Hali hii ilisababisha timu
hiyo kufungwa bao 1-0 na JKU na kuondoshwa kwenye mashindano hayo.
Yanga inatakiwa kujipanga katika hesabu zake kama inataka mataji.
Ligi ya Zanzibar iko chini, vipaji kibao
Hii ni sawa na hadithi ya masikini mwenye ng’ombe
100. Ligi ya Zanzibar inaonekana kuwa chini. Timu zake zinaonekana
kucheza soka la kisasa lakini uwezo wao wa kupambana uwanjani upo chini.
Hili lilithibitika tu mara baada ya mechi za hatua ya makundi
kumalizika. Hakuna timu ya Zanzibar iliyofanikiwa kuongoza kundi hata
moja licha ya uwepo wa timu nyingi kutoka visiwani humo. Timu nyingi za
Zanzibar zilionekana kujikongoja kwenye mashindano hayo. Hata Polisi na
JKU zilizotinga nusu fainali zilionekana kutembelea nyota tu. JKU
ilifunga bao moja kwenye mechi ya Yanga ikiwa ndiyo shuti lake la kwanza
na la mwisho kulenga lango kwenye mechi hiyo. Mbali na viwango hivyo
duni vya timu za Zanzibar, vijapi kem kem vimeonekana visiwani humo.
Wachezaji wengi wa Zanzibar wanaonekana kuufahamu vizuri mpira, wamekosa
tu ile hali ya kupambana.
Azam duuh!
Chukua dakika chache kutafakari viwango vya
wachezaji wa Azam. Timu hiyo ina makipa wawili wa Taifa Stars, Mwadini
Ally na Aishi Manula. Ina mabeki wenye uwezo wa juu kama Muivory Coast
Paschal Wawa, Aggrey Morris na Shomary Kapombe. Timu hiyo ina
washambuliaji wa uwezo wa kimataifa kama Kipre Tchetche, Didier
Kavumbagu, John Bocco na Brian Mwajega. Hata hivyo licha ya viwango vya
wachezaji hao, Azam bado inaonekana kuwa na tatizo. Ilishinda mechi
mbili pekee za michuano hiyo, tena kwa ushindi mwembamba wa bao 1-0
dhidi ya Mtende Rangers na ule wa mabao 2-1 dhidi ya KMKM. Hali hii
inazua hofu juu ya uwezo wa kocha Joseph Omog katika kuwaunganisha
mastaa wa timu hiyo na kuifanya iwe hatari zaidi nchini.
Usajili wa dirisha dogo ni matata
Usajili uliofanywa na timu za Ligi Kuu Baara
wakati wa dirisha dogo unaonekana kuwa wa maana. Kombe la Mapinduzi
limethibitisha hilo baada ya wachezaji hao kuonyesha viwango vya juu.
Straika wa Yanga, Kpah Sherman, beki wa Simba Juuko Murshid na kiungo
Simon Sserunkuma wanaonekana kuwa makini katika kazi zao.
Viwango walivyoonyesha kwenye mashindano hayo
vimeanza kuthibitisha thamani zao uwanjani. Sherman kafunga mabao mawili
wakati Sserunkuma alikuwa nguzo muhimu kwenye mechi za robo fainali na
nusu fainali za Simba. Kiungo mshambuliaji wa Azam, Brian Majwega naye
amethibitisha thamani yake pale Azam baada ya kupika mabao manne kwenye
mashindano hayo. Straika wa Simba Dan Sserunkuma pekee ndiye
aliyeshindwa kutamba kwenye mashindano hayo kwani alilazimika kusubiri
hadi mechi ya fainali kufunga bao, tena kwenye mikwaju ya penalti.

