Na Baraka Mbolembole, Dar es Salaam,
Itakuwa ‘ bonge ya gemu’ jioni
hii katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kati ya mabingwa watetezi wa
ligi kuu Tanzania Bara, Vodacom Premier league, Azam FC dhidi ya
mabingwa mara 19 wa zamani ambao wanasotea nafasi mbili za juu kwa msimu
wa tatu sasa, Simba SC. Azam FC inaongoza ligi kabla ya michezo ya
Jumapili hii wakiwa na pointi 20 itaingia uwanjani ikiwa imetoka
kushinda michezo miwili mfululizo ugenini dhidi ya Stand United 0-1 Azam
FC, Kagera Sugar 1-3 Azam FC.
Simba chini ya Goran Kopunovic
imeshuka dimba mara moja na kupata ushindi wa pili msimu huu kufuatia
ushindi wa Ndanda FC 0-2 Simba SC katika uwanja wa Nang’wanda wiki
iliyopita. Simba wananing’inia katikati ya msimamo wakiwa na pointi 12
wanahitaji ushindi ili kupunguza gepu la pointi na viongozi hao.Kitendo
cha kupoteza mchezo huo itakuwa ni sawa na kujiondoa katika mbio za
ubingwa, kwani licha ya kuwa nyuma kwa mchezo mmoja, kitendo cha
kuwaruhusu Azam kushinda itawafanya Simba kuwa nyuma ya pointi 11 dhidi
ya mabingwa hao watetezi.
SI MECHI YA KIPIMO CHA UBINGWA, LAKINI……
Mabadiliko yote ya uchezaji
katika kikosi cha Simba yametajwa kuletwa na kocha, Goran ambaye tangu
alipoanza kazi klabuni hapo mwezi uliopita, ameisaidia Simba kushinda
michezo yote saba ya kimashindano ikiwemo kushinda ubingwa wa Mapindu
Cup huko Visiwani Zanzibar. Goran ameiongoza Simba dhidi ya timu za Bara
katika michezo miwili. Mchezo wa kwanza ulikuwa ni ule dhidi ya Mtibwa
Sugar 0-0 Simba SC katika fainali ya michuano hiyo ya Mapinduzi. Simba
ilishinda kwa changamoto ya mikwaju ya penalti.
Mchezo wa pili wa Goran dhidi ya
timu za Bara ni ule wa ligi kuu waliopata ushindi ugenini dhidi ya
Ndanda FC wiki iliyopita. Kiuchezaji Simba imeonekana kuimarika kiasi
cha kufufua matumaini ya mashabiki wake kuwa huenda wakarudi katika
nafasi mbili za juu ambazo hutoa wawakilishi wa nchi kaika michuano ya
Afrika upande wa vilabu. Msimu uliopita Simba ilipoteza michezo yote
dhidi ya Azam FC na pointi hizo sita ziliwasaidia Azam kufikia ndoto na
kutwaa ubingwa wa kwanza wa ligi kuu Bara. Je, Simba imeimarika kweli?
Azam ilianza msimu kwa spidi ya
chini ikiwemo kupoteza michezo miwili mfululizo dhidi ya JKT Ruvu 1-0
Azam FC, Ndanda FC 1-0 Azam FC vipigo ambavyo viliambatana na sare dhidi
ya Mbeya City na Tanzania Prisons. Simba pia walianza kwa mwendo wa
kusuasua, sare sita mfululizo, kabla ya ushindi wa kwanza katika raundi
ya saba, Simba SC 1-0 Ruvu Shooting, kisha kichapo Simba SC 0-1 Kagera
Sugar katika raundi ya nane, imezinduka dhidi ya Ndanda FC huku vijana
wa Goran wakicheza michezo saba pasipo kuruhusu goli langoni mwao.
Kipimo zaidi cha malengo yao
mapya ni mchezo wa leo, kama ushirikiano wa Kipre Tchetche, Didier
Kavumbagu na Brian Majwega hautazalisha goli lolote kwa kuthibitiwa na
safu ‘ kabambe’ ya ulinzi chini ya nahodha mpya wa timu kijana Hassan
Isihaka, 20, Murisheed Juuko, Hassan Kessy na Mohamed Hussein bila shaka
Goran anaweza kuwa sababu kubwa ya mafanikio. Lakini bado kuna safari
ndefu ambayo Goran na vijana wake wanayo kwanza ni kuwazima mabingwa
watetezi waliorudi katika ‘ mwendo wa ushindi’.
Frank Domayo atacheza mchezo
wake wa kwanza mkubwa baada ya miezi takribani saba, lakini ni mchezaji
kijana mwenye uzoefu mkubwa, mara nyingi ameshiriki kiuhakika katika
mipambano ya Simba na Yanga SC. Kiungo huyo maarufu kwa jina la ‘
chumvi’ alifunga bao pekee katika ushindi dhidi ya Stand United na
akashiriki katika upishi wa moja ya mabao matatu ya Azam katika ushindi
dhidi ya Kagera Sugar. Sasa ndiye kiungo-namba-8 wa Azam atakutana na ‘
mtu mbishi’, nahodha msaidizi Jonas Mkude.
Sehemu hii ya kaikai ya uwanja
itakuwa na ushindani mkubwa, baada ya kutokea benchi na kutengeneza moja
ya mabao mawili ya timu yake dhidi ya Ndanda FC, Mganda, Simon
Sserunkuma anatazamiwa kuanza sambamba na Mkude na Said Ndemla katika
eneo la kiungo upande wa Simba. Kipre Bolou ambaye urejeo wake katika
mchezo dhidi ya Kagera siku ya Jumanne kumeifanya safu ya kiungo ya Azam
kuwa na nguvu. Himid Mao anaweza kuanza mahala kwa Mudathir Yahya.
Salum Abubakary Hajaonekana katika michezo kadhaa sasa ni kiungo ambaye
huwasumbua sana Simba. Kila timu itakuwa na nafasi ya kutawala mchezo,
timu itakayokuwa na mbinu bora inaweza kushinda.
Kocha wa Azam FC, Joseph Omog
anahaha kuziba ‘ nyufa’ katika ngome. Shomari Kapombe atakuwa akicheza
kwa mara ya kwanza dhidi ya timu yake ya zamani atakutana na Danny
Sserunkuma ambaye licha ya kucheza katika eneo la ushambuliaji
hupendelea kucheza pembeni upande wa kushoto, huko hutulia na mpira na
kushambulia kwa kasi. Danny atahitaji spidi
Mchezo huu ni kipimo kwa safu ya
ulinzi ya wawakilishi hao wa Tanzania katika klabu bingwa Afrika, kwani
wanakutana na safu ya mashambulizi yenye kasi na uwezo wa kumiki mpira.
Licha ya uwepo wa Danny, Emmanuel Okwi anataraji pia kuanza sambamba na
Ramadhani Singano katika wingi ya kulia. Omog anaweza kuwatumia Kapombe
upande wa kulia, Erasto Nyoni katika beki-3, Paschal Wawa na kaimu
nahodha Aggrey Morris.
Azam wamekuwa na tatizo katika
ngome, mipira ya krosi, kona na faulo imekuwa ikiwagharimu sana kama
wataziba nyufa za kupitishwa mipira kutokea pembeni mwa uwanja wanaweza
kufanikiwa kushinda, lakini bahati mbaya Simba hutumia krosi za chini
ambazo ni hatari kwa walinzi wasio na utulivu. Nani msindi? Timu
itakayokuwa na mbinu bora inaweza kushinda mchezo huu. Azam wanauwezo wa
kufunga mabao mawili, Simba wataweza?. Danny tayari amefunga bao katika
mchezo wake wa pili wa ligi kuu, anaweza kufunga tena leo.
Credit Shafiidauda