Adebayor amekua akizomewa na mashabiki wa Spurs kwa kile kinachodaiwa ameshuka kiwango na hastahili kuwepo klabuni hapo kwa sasa, zaidi ya kutafutiwa mahala pakwenda, ili hali kwa upande wa mashabiki wa Arsenal wanachukula kama msaliti.
Ombi kwa mashabiki wa klabu hizo pinzani jijini London limetoka kwa meneja wa Spurs, Mauricio Pochettino baada ya kuthibitisha huenda akamtumia mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 30 katika mchezo wa kesho ambao utachezwa katika uwanja wa White Hart Lane.
Pochettino, amewataka mashabiki kumstahamilia Adebayor na kumuona sawa kama wachezaji wengine ambao wana haki ya kucheza soka kwa kushangiliwa wakati wote.
Meneja huyo kutoka nchini Argentina, amesisitiza jambo hilo huku akitilia mkazo wa mshikamano kwa wachezaji pamoja na benchi la ufundi ili kutimiza lengo la ushindi ambalo litakua kikwazo kwa mashabiki wa Spurs kumzomea Adebayor wakati wote.
Amesema hiyo ndio njia sahihi ambayo anahisi itakua salama kwa Adebayor hiyo kesho, lakini kama itakwenda tofauti na hapo mambo yatakua magumu zaidi hasa ikizingatiwa mashabiki wa Arsenal wamekua na machungu na mshambuliaji huyo ambaye aliwahama na kujiunga na Man City mwaka 2009.

