Shirika
la Ugavi na Usambazaji wa Umeme nchini (TANESCO), limekiri kuwepo na
matatizo ya mfumo wa kununua Lipa Umeme Kadiri Utumiavyo (LUKU),
ulioanza Ijumaa jioni wiki iliyopita hadi jana na kuwa matatizo hayo
yanatokana na mfumo wa kuuza umeme wa LUKU.
Akizungumza
na mwandishi jijini Dar es Salaam jana, Meneja Mawasiliano wa TANESCO,
Adrian Shogholo alisema ni kweli kuwa tatizo hilo lipo na limetokana na
mfumo wa manunuzi wa umeme wa LUKU.
“Ni kweli
tunaomba radhi wateja wetu kwamba kuanzia Ijumaa jioni kulianza tatizo
la kununua umeme wa luku, kwa wateja wetu, ila tumegundua tatizo na
mafundi wetu kwa kushirikiana wa mafundi kutoka Afrika Kusini, ambao
walitengeneza mfumo huo, wanalishughulikia tatizo hilo”,
alisema Shogholo.
Aidha
aliahidi kwamba muda wowote kuanzia leo, huduma zitaanza kupatikana na
kwamba wakati tatizo hilo likiendelea kushughulikiwa, wateja wa Luku
wanaweza kununua umeme kupitia benki ya CRDB, NMB na Max Malipo.
“Kuna
wateja wanaotumia simu kununua umeme, wapo waliotuma fedha na
hawajarudishiwa majibu ya umeme, na wengine wamepata umeme ila
wakiingiza kwenye LUKU hauingii, wasihofu fedha zao ziko salama na
watapata umeme, tutawatumia namba nyingine ambazo wakiingiza
zitakubali”,
alisema Shogholo.