Makundi ya vijana wanaosadikiwa kuwa ni wa jamii ya kimaasai maarufu
kama “Morani” katika eneo la Olasiti Jijini Arusha, wameteketeza kwa
moto mali mbalimbali zikiwemo nyumba pamoja na magari ya wakazi wawili
wa eneo hilo, wanaotuhumiwa kumpiga na kumsababishia kifo kijana mmoja
wa jamii hiyo.
Kijana Melita John anadaiwa kuuawa na Bernard Kavishe mkazi wa
Olasiti akishirikiana na majirani zake wawili akimtuhumu kijana huyo
kuwa ana uhusiano wa kimapenzi na msichana wake wa kazi za ndani ambaye
ni binti wa miaka 17 anayefahamika kwa jina la Monica Emanuel
Taarifa zaidi zinadai kuwa hatua ya morani wa kimaasai kujichukulia
sheria mkononi na kuteketeza nyumba na magari pamoja na mali nyingine za
watuhumiwa hao ni katika kulipiza kisasi kutokana na kifo cha mwenzao
wanayedai hakuwa na hatia.
Inadaiwa mtuhumiwa wa kwanza wa mauaji hayo Benard Kavishe baada ya
kuwasili nyumbani kwake majira ya saa saba mchana na kugonga gate la
nyumbani kwake ilimchukua muda wa dakika kumi msichana wake wa kazi
kufungua ndipo alipoingia ndani na kumkuta kijana Melita akiwa bila nguo
ndipo alipowaita majirani wenzake na kumshambulia kwa kipigo hadi
kumsababishia mauti.
Jeshi la Polisi kupitia wa Kaimu kamanda wa Mkoa wa Arusha Kamishna
Msaidizi Edward Balele akithibitisha tukio hilo amesema baada ya
watuhumiwa wanaosadikiwa kushiriki katika mauaji ya kijana Melita
wanashikiliwa kwa mahojiano zaidi.









