Serikali imesema ajira za walimu wapya zitaanza rasmi Mei Mosi, mwaka huu huku ikiweka wazi kuwa walimu hao wasitegemee kupangiwa katika maeneo ya majiji, manispaa na miji.
Walimu hao wametakiwa kutotegemea kupangiwa katika maeneo hayo
kutokana na idadi ya walimu waliopo ni kubwa na inakidhi mahitaji, huku
maeneo yaliyopewa kipaumbele ni vijijini na halmashauri ambazo zina
mahitaji na upungufu mkubwa wa walimu.
Idadi ya walimu wapya watakaoanza ajira zao mwezi ujao ni 31,056
ambapo kwa walimu wa ngazi ya Cheti ni 11,795, Stashahada (Diploma)
6,596 na wenye Shahada (Degree) 12,665.
Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa
na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Jumanne Sagini wakati akizungumza na
waandishi wa habari kuhusu ajira mpya za walimu kwa mwaka 2014/2015.
Alisema kwa mwaka huu ajira hizo zimechelewa kutokana na TAMISEMI
pamoja na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kufanya ufuatiliaji wa
kina hadi katika ngazi ya shule ili kubaini kwa uhakika mahitaji halisi
ya walimu kwa kila halmahauri na shule.
“Ufuatiliaji huo umebaini kuwepo kwa halmashauri na shule hasa za
mjini zenye walimu wa ziada na zingine hasa za vijijini zina upungufu
mkubwa wa walimu,” alisema Sagini.
Alisema taarifa hizo zimesaidia kuwapanga walimu wapya kwa usawa ili
kuondoa uwiano usioridhisha kwenye maeneo mengi ya vijijini. Alisema kwa
sasa wanakamilisha taratibu za kupata kibali kwa ajili ya ajira za
walimu na fedha za kuwalipa stahili zao ili waanze ajira zao rasmi mwezi
ujao.
Aidha, alisema orodha ya walimu na vituo watakavyopangiwa vitawekwa
katika tovuti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI ambayo ni
www.pmoralg.com na ya Wizara ya Elimu www.moe. go.tz ifikapo Aprili 24,
mwaka huu.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa TAMISEMI, Zuberi Samataba
alisema, pia ufuatiliaji huo ulikuwa ni kuhakikisha wanakuwa na taarifa
sahihi za walimu wanaoajiri wote ni wapya ambao hawajawahi kuajiriwa ili
kuepuka usumbufu kwa walimu ambao hawatoi taarifa.
Alisema baadhi ya walimu ambao wameshaajiriwa wanapoenda kusoma,
hupangiwa upya vituo na hawatoi taarifa hivyo kuleta usumbufu wa
kuchelewa kutopata mishahara yao.
“Kuna baadhi ya walimu wameshaajiriwa kwa hiyo jina linapoingizwa
katika taratibu za malipo, linagoma kuingia ndipo ukifuatilia unajua
alikuwa ameajiriwa, inabidi umwambie arudi kwa mwajiri wake.
"Kwa hiyo kwa hawa walimu wapya nawashauri waende kuripoti katika
vituo walivyopangiwa na wakubali kufanya kazi katika maeneo hayo, sio
waripoti halafu waondoke,” alisema.
Wakati huohuo, Serikali imewataka Makatibu Tawala wa Mikoa ambayo
shule zake zimefungwa kwa madai ya ukosefu wa chakula, kuwachukulia
hatua wakuu wa shule hizo, kwa kile kilichoelezwa kuwa wamekiuka
utaratibu kutangaza hivyo ilhali serikali ilishatuma fedha kwa ajili ya
chakula cha wanafunzi katika shule mbalimbali nchini.