Na George Mganga
Kwanza na awali ya yote napenda
kutoa shukrani na pongezi kwa wale wote mmekuwa karibu na mimi kusoma
hizi makala ambazo nimekuwa nikiziandaa kwa hizi siku za karibuni.
Natoa pole na pongezi pia kwa
Shirikisho na mpira wa miguu hapa nchini TFF kwa majukumu mazito na
changamoto mbalimbali ambazo wanakutana nazo katika kuhakikisha soka
letu linasimama.
Tunajua TFF ndiyo kiongozi mkuu wa mpira hapa nchini na bila wao soka letu lisingekuwa hapa lilipo hivyo ni sawa kuwapongeza.
Ni mechi kadhaa sasa zimesalia kwa kila timu kumaliza idadi stahiki katika ligi kuu ya hapa Tanzania.
Na hapa tutajua ni timu zipi
zitashuka daraja na zipi zitakuwepo katika michuano ya kimataifa na
halikadhalika zitakazoshuka daraja.
Mengi zaidi tumeyashuhudia katika
msimu huu ambayo yameshusha hata hadhi ya ligi yetu na yamekuwa
yakirudisha zaidi maendeleo nyuma ya soka letu badala ya kwenda au
kuendelea mbele zaidi.
Moja kati ya mambo ambayo
hayaleti ubora na umakini wa ligi hii ni baadhi tu ya waamuzi ambao
wamekuwa wakipigiwa kelele kila kukicha kwa tuhuma za maamuzi mabovu.
Waamuzi wengi tulionao hapa kwetu
huwa hawawezi kabisa kuumudu mchezo kwa kwenda tofauti kabisa na
maamuzi ya uwanjani ambayo huzingatia uwepo wa sheria 17 za soka.
Udhaifu huwa unakuja pale mwamuzi
anapotoa kadi ovyo ovyo tu bila kuzingatia taaluma yake inapaswa afanye
maamuzi gani pindi tukio la kimchezo linapotokea uwanjani.
Nadhani rushwa pia imekuwa ni
sababu tosha inayosababisha haya yote kutokea kwani baadhi yao wamekuwa
wakihongwa pesa ilimradi tu timu fulani iondoke na matokeo mabovu ili
mwamuzi naye apate pesa yake.
Hili sio jambo dogo hata kidogo na inabidi TFF ichukue hatua pindi inapobainika mwamuzi kafanya jambo kama hili.
Kingine ni mvurugano wa ratiba na
kupelekea mechi kubadilishwa tarehe mara kwa mara na naweza kusema
tangu nianze kufuarilia soka la hapa kwetu sijawahi kuona ratiba
ikibadilika mara kwa mara kiasi hiki.
Asili na asilimia kubwa ya timu
zetu zimekuwa zikitegemea mapato ya viingilio vya milangoni na pesa
inayopatikana ndiyo imekuwa ikiendesha timu hizo katika shughuli zote.
Fikiria timu kama Ndanda au Stand
united imekuja hapa Dar es salaam kuweka kambi ya siku 4 na leo hii
unawapa taarifa tena kwa kuwashtukiza tu kuwa mechi itachezwa siku 3
zijazo.
Moja kwa moja utakuwa umeshazitia
hasara timu kama hizo ambazo hazijaimarika vizuri kiuchumi na badala
yake utakuwa unazitia hasara tu.
Bodi ya ligi inajukumu la kujipanga tokea mwanzo pindi inapoandaa ratiba ya ligi kuu.
Inabidi tufikie wakati sasa wa
kujaribu kuiga hata ligi za wenzetu sasa ili tuweze kuondoka katika
hatua hizi tulizopo hivi sasa nantufike mbele zaidi katika soka letu.
Jambo lingine ni kuhusiana na
maandalizi ya viwanja kuwa duni, ni malalamiko mengi sana yamekuwa
yakitolewa na wachezaji pamoja na vilabu kuwa viwanja havina ubora.
Mfano mzuri ni kile kiwanja cha
Mkwakwani Tanga kimekuwa kibovu sana siku zote na malalamiko yapo lukuki
lakini hakuna hata urejesho wa kauli yoyote tokea TFF na wapo wanaona.
Timu mwenyeji siku zote hawezi
kusema uwanja wake ni mbovu sababu ya uzoefu alivyozoea kuchezea hapo na
hata mazoezi huwa anafanya lakini kwa timu ngeni huwa ni tatizo zaidi.
Timu mbili zenye jina kubwa hapa
nchini zilishawahi kuulalamikia uwanja wa Mkwakwani kuwa haufai hata
kuwa na hadhi ya kuuchezea sababu una kama mabonde kwenye pitch.
Naomba haya TFF iyaangalie kwa
macho mawili makini zaidi ikiwepo na kufungia au kuzuia hivi viwanja
vibovu au kupiga hata faini kwa vilabu husika hadi ukarabati
utakapofanyika.
Gumzo kubwa ambalo lilitokea hapa
katikati ya msimu wa ligi kubadilika kwa sheria ya mchezaji pindi
anapopata kadi 3 za njano awe na fursa sasa ya kuchagua mechi ipi
acheze.
Kwangu mimi naona ni maamuzi
ambayo hayakuwa sawa kabisa kutokana na uamuzi wenyewe kuhusisha timu
moja tu na vingine vikiwa havina taarifa sijajua hatima yake ilifikiaje
baada ya uamuzi huo.
Ingekuwa vizuri zaidi kama chombo
cha ligi kingekuwa kinandaa taarifa hizi mapema kufikisha katika timu
zenyewe ili kuepusha malumbano ya kila siku.
TFF inapaswa kukaa na kujenga
misingi mzuri katika kuendesha soka letu na kuwa na wajibu wakati wa
kuandaa ratiba kila kitu kikishakamilika kusiwe na uhitaji wa mabadiliko
mengine hapo baadae.
Hatuhitaji kuona ligi yetu
inaenda kienyeji bali ni wakati sasa wa kuhakikisha tunaenda na wakati
zaidi na sio tunarudi huko tulipotokea.
Ni halali yako kucomment chochote juu ya hiki nilichokiandaa hapa au kama una wazo lolote kwa kunipata na hii namba
0688665508
Ahsanteni na majukumu mema
Credit shaifi duada