Mkuu wa Jeshi
la Polisi Nchini, IGP Ernest Mangu akitoa hotuba yake katika Mafunzo ya
kuwajengea uwezo viongozi wa dini ya Kiislam katika kuimarisha usalama
nchini yakiwa na kauli mbiu isemayo "Amani na usalama ndio maisha yetu".
Na Frank Geofray- Jeshi la Polisi.
Mkuu wa
Jeshi la Polisi Nchini IGP Ernest Mangu pamoja na viongozi wa dini ya
Kiislamu nchini wameungana kwa pamoja kukemea vitendo vya uhalifu hapa
chini pamoja na kuzitaka familia kutoa malezi bora kwa watoto wao ili
kuondokana na wimbi la watu wanaojiingiza katika vitendo hivyo.
Rai hiyo
ilitolewa leo jijini Dar es salaam na IGP Ernest Mangu pamoja na
Viongozi mbalimbali wa dini ya kiislamu katika muendelezo wa Mafunzo ya
kuwajengea uwezo viongozi wa dini hiyo katika kuimarisha usalama nchini
yakiwa na kauli mbiu isemayo "Amani na usalama ndio maisha yetu".Mafunzo
ambayo yaliratibiwa na Taasisi ya Mwinyi Baraka na kuhudhuriwa na
viongozi mbalimbali wa dini ya kiislamu hapa nchini.
IGP Mangu
alisema Viongozi wa dini wanadhamana kubwa katika kuhakikisha kuwa
vitendo vya uhalifu vinadhibitiwa nchini kwa kuwaelimisha waumini wao na
jamii kwa ujumla juu ya madhara ya uhalifu pamoja na kuwapa mafundisho
yatakayojenga na kuimarisha ulinzi na usalama nchini.