Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman
Mbowe, amesema hawatamruhusu Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto
Kabwe, kujiunga na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Kauli ya Mbowe imetolewa siku chache baada ya Zitto kutangaza kuwa ACT
ipo tayari kujiunga na Ukawa kama wanavyotaka Watanzania wakiwamo baadhi
ya viongozi wa umoja huo.
Alitoa kauli hiyo jana wilayani Kyerwa alipozungumza na Mwandishi wetu.
Mbowe alisema kuwa hawamwamini tena Zitto kwa madai kuwa akiingia Ukawa
atakuwa akivujisha siri za umoja huo kwenda Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Hatuwezi kumruhusu Zitto na chama chake kiwe miongoni mwa Ukawa.
Tukiruhusu Zitto awepo siri zote zitakuwa zikiwafikia CCM,” alisema
Mbowe.
Aprili 15 mwaka huu, Chama cha Alliance for Change and Transparency
(ACT-Wazalendo), kilitangaza kuwa kipo tayari kushirikiana na vyama
vingine vya siasa kwa lengo la kuleta mapinduzi ya uchumi na kubomoa
mfumo unaowanyonya wananchi.
Zitto alisema hivi sasa taifa limekuwa na shauku ya ACT kushirikiana na
vyama vingine kama njia ya kufanikisha malengo ya kukitoa CCM
madarakani.


