Simba waligoma kuingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo walipocheza na Mbeya City jumamosi iliyopita uwanja wa Sokoine
Na Shaffih Dauda
MTANDAO huu kwa muda mrefu sasa
umekuwa ukifanya tafiti na kufuatilia mwenendo wa klabu ya Simba katika
mechi za ligi kuu soka Tanzania bara msimu huu.
Mwishoni mwa juma lililopita,
Simba ilifungwa magoli 2-0 na Mbeya City fc katika uwanja wa Sokoine,
Mbeya na kuifanya klabu hiyo kongwe nchini kuendelea kukaa nafasi ya
tatu kwa pointi 35 walizokusanya baada ya kushuka dimbani mara 22.
Machi 18 mwaka huu walifungwa
magoli 2-0 na Mgambo JKT katika uwanja wa CCM
Mkwakwani Tanga, lakini
wakashinda 2-1 ugenini dhidi ya Kagera Sugar uwanja wa CCM Kambarage,
Shinyanga na ilikuwa aprili 6 mwaka huu (jumatatu ya pasaka).
Katika mechi hizo tatu, mtandao huu ulikuwa unachunguza mwenendo wa Simba na namna wanavyoiandaa timu kwa ajili ya mechi.
Katika mechi ya Tanga
waliyochapwa na Mgambo, timu iligoma kuingia kwenye vyumba vya
kubadilishia nguo, wachezaji wakakaguliwa ndani ya basi nje ya geti
karibu na vyumba vya kubadilishia nguo.
Simba walifanya hivyo wakihofia
kurogwa na wenyeji wao, lakini mwisho wa siku wakafa mbili bila na
walipoenda Shinyanga kucheza na Kagera walifanya hivyo hivyo, walikataa
kuingia vyumbani na kukubali kutozwa faini na TFF.
Simba waliendeleza tabia yao ya
kutoingia vyumbani kwa madai ya kuogopa kurogwa huku wakisingizia vyumba
ni vibovu. Inawezekana kweli ni vibovu, lakini dhahiri walikuwa na
mawazo mengine kichwani mwao kwani viongozi walionekana kuwapangia
wachezaji maeneo ya kupita wakati wanaingia uwanjani.
Baada ya safari ndefu ya
uchunguzi, hatimaye jibu limepatikana kule Mbeya ambako Simba amekufa
tena mbele ya Wagonga nyundo wa Mbeya, Mbeya City fc.
Tulipiga kambi jijini Mbeya na
kugundua kuwa Simba wameharibikiwa kwasababu wanawatumia Waganga wa
kienyeji kwa muda mwingi wakiamini watawasaidia kupata matokeo ndani ya
uwanja.
Dunia ya leo klabu kongwe ya
Simba, mfano wa kuigwa inaendekeza imani za kishirikina kwa kiwango cha
juu namna hii, inasikitisha sana.
Chakusikitisha zaidi ni kwamba,
tunaamini viongozi waliopo madarakani ni vijana wa kidijitali yaani wa
kisasa au kileo. Imefika wakati tunaamini wazee kama vile Hassan Dalali
na wengineo hizi si zama zao, lakini hayo ni maneno tu, inawezekana wale
wazee wakawa na mafanikio makubwa kuliko vijana ambao tunaamini
wanaweza kuiendesha timu kileo au kisasa, vijana ambao ukiwaangalia ni
watanashati, lakini matendo wanayoifanyia klabu ni mabaya mno.
Kwa aina ya viongozi wa sasa wa
Simba, ni jambo la aibu kutumia muda mwingi kuwekeza katika uchawi ,
kutumia waganga au ndumba wakiamini watasaidia kupata matokeo kuliko
kujikita katika maandalizi ya kitaalamu na kiuweledi.
Simba wamefungwa na Mbeya City
kwasababu hawakutoa nafasi ya kiuweledi katika maandalizi yao,
waliwekeza nguvu kwa mambo ya nje ya uwanja wakiamini yatawasaidia
kupata matokeo.
Utaratibu ulivyo, unapoenda
uwanja wa ugenini, siku moja kabla ya mechi, timu inatakiwa kufanya
mazoezi kwenye uwanja ambao watachezea mchezo, kwahiyo Simba walitakiwa
kwenda kufanya mazoezi Sokoine siku ya ijumaa, lakini kutokana na
kuamini mambo ya kishirikina hawakwenda kufanya mazoezi siku hiyo,
matokeo yake ilibidi wafanye mazoezi kwenye bustani (Garden) ya Hoteli
waliyofikia, wanafanyia mazoezi ‘Garden’ eti kwa sababu wanaogopa
kurogwa na Mbeya City.
Hii ilikuwa kinyume, mwalimu na
benchi la ufundi walitaka timu ikafanye mazoezi uwanjani, lakini baadhi
ya viongozi walioandama na timu waliona timu ikienda kufanya mazoezi
Sokoine wataenda kupoteza mchezo wa jumamosi.
Mwisho wa siku wakafanya mazoezi uani, wakafanya mazoezi ‘Garden’, na wakawa ‘wamefeli’ rasmi.
Ikaja siku ya mechi, badala ya
kupita kwenye mlango wa kawaida wakapitia mlango wa nyuma, wachezaji
wakashuka na kuingilia mlango wa nyuma, wakashindwa kuingia kwenye
vyumba vya kubadilishia nguo, wakakaa pembeni kwenye kona kulia kwa
jukwaa kuu la Sokoine, sehemu ambayo maaskari Polisi wanapenda kuweka
magari yao.
Baadaye kidogo wakaenda karibu na
sehemu ya vyumba vya kubadilishia nguo na kukaa nje upande wa kulia
kwenye chumba chao , lakini wachezaji wakaamuriwa waondoke tena.
Muda huo wachezaji wa Mbeya City
walikuwa wanapasha moto misuli ‘Warm-up) na walikuwa wameshafanya kwa
muda mrefu, Simba wao walichelewa hata kupasha moto misuli kutokana na
mambo yao ya kishirikina.
Wakati wanaingia kwenye ‘Warm-up’
badala ya kuingilia kwenye benchi ambalo watakaa upande wa kushoto
kwasababu kulia walikuwa wamekaa Mbeya City kinyume na taratibu
zinazowataka wenyeji kukaa benchi la kushoto na wageni kulia, Simba
wakarudi kwenye kona waliyoingilia mara ya kwanza
Simba walifuata taratibu kwamba
wenyeji wanakaa benchi la kushoto, wageni kulia, lakini kulia ni sehemu
ambayo Mbeya City wanakaa kila siku na Simba walikataa kukaa kushoto
wakiamini pameshapigwa misumari. Walipotaka kukaa kulia Mbeya City
wakagoma na ndipo ikatokea vurumai kati ya watu wa Mbeya City na Simba,
ikabidi Simba wawe wapole na kukubali kukaa kushoto.
Wakati huo wachezaji walikuwa
wamekaa chini nyuma ya lile benchi la ufundi na ilibidi wakafanye
‘warm-up’, kwa itikadi hizo hizo za kishirikiana wakashindwa kuingia
uwanjani kupitia eneo hilo, wakaambiwa watembee na kurudi goli la kusini
wazunguke kwenye kibendera cha kona na waingie uwanjani na mstari ule
wakafanye ‘warm-up’.
Ukiangalia kwa undani, wachezaji
hawataki mambo hayo, wanakasirika, wanaingia uwanjani hawana raha,
lakini kwasababu wamelazimishwa na wapambe wanaojifanya wanajua kila
kitu, timu iingilie wapi, wakanyage wapi na kamwe hawataki kukiuka
maigizo ya waganda wa kienyeji.
Siku ya mechi hakika wachezaji
hawakuwa sawa kisaikolojia, waliingia kupasha misuli na kuanza mechi,
wakati wanacheza Mbeya City waliwazidi Simba, walikuwa wamechangamka,
walionesha kabisa wanahitaji matokeo, lakini Simba walikuwa wanacheza tu
kama vile mtu anayetaka kutekeleza jukumu lake na kuondoka.
Jonas Mkude, Abdi Hassan Banda,
Said Ndemla wakawa wanazunguka tu, wanageuka nyuma na mipira, hawaoneshi
nia ya kwenda mbele, Elius Maguli, Ibrahim Hajibu wakaonekana vimeo
kwasababu walikuwa hawapati huduma kutoka kwa viungo.
Mbeya City walicheza vizuri sana
ukiachana na mambo ya kupiga misumari kwa wale wanaoamini hivyo, lakini
kwasisi ambao hatuamini hivyo, tukiamini kuwa maandalizi ya mechi ni
mazoezi, Mbeya City walicheza zaidi ya Simba, walitengeneza nafasi
nyingi na kilichosababisha Simba washindwe kucheza ni imani za
kishirikina.
Kuna baadhi ya wachezaji ambao
sitaki kuwataja hawafurahishwi na vitendo vya kuendekeza vitendo vya
kishirikina, walienda Tanga kuchuana na Mgambo, kuna mtu mmoja wa kamati
ya utendaji (jina tunalo) anapenda sana mambo ya kishirikina, alienda
na waganga karibia nane (8) Mkwakwani, wakapigwa 2-0 na Mgambo.
Pointi yetu ni kuwakanya Simba na
timu nyingine za ligi kuu kuachana na mambo ya kuamini waganga . Hata
tabia ya Mbeya City kulinda uwanja, kuchimbua uwanja na kufukia vitu ni
ya kishamba, matokeo hayapatikani kwa njia ya Waganda. Mbona kuna
mataifa yanasifika kwa uchawi lakini wanaboronga katika soka?
Hata hapa Tanzania maeneo yanayosifika kwa uchawi mfano Sumbawanga mbona hawana hata timu ya ligi kuu?
Inawezekana waganda wanatumika
kwasababu ya mila na desturi za kizamani, lakini hayatakiwi kufanyika
kwa kasi ya ajabu kama wanavyofanya Simba na timu nyingine.
Kama yanafanyika kwasababu za
kitamaduni basi yafanyike kwa siri pasipokuwahusisha wachezaji,
haiwezekani eti wamekuja waganga usiku Hotelini, wachezaji wanaamushwa
usiku kusikiliza maelekezo ya Waganga.
Unawachosha wachezaji,
hawapumuziki vizuri, matokeo yake wanapoteza malengo, inatakiwa mchezaji
alale mapema, akae kitandani awaze mechi ya kesho, ajiandae na mechi
kisaikolojia, lakini unapomuamsha usiku unamnyima muda wa kupumzika, pia
unamnyima nafasi ya kuuwaza mchezo wa kesho na matokeo yake analala na
msongo wa mawazo na hasira juu kutokana na kusumbuliwa usiku.
Matokeo yake wanaingia kwenye
mechi bila kuwa sawa kisaikolojia na wanafungwa si kwasababu ya kukosa
uwezo bali ni miundombinu ya viongozi kushindwa kuwaandaa wachezaji
kiuweledi.
Waganga hawasaidii katika soka,
maandalizi ya kitaalamu, kiuweledi ndiyo yanatoa nafasi ya kupata
matokeo. Simba na timu nyingine zote badilikeni!
Nawatakiwa jumatatu njema, tukutane tena jumatano ya wiki hii!!