Rais
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF, Jamal Malinzi ametuma
salamu za pongezi kwa Mwenyekiti wa klabu ya Young Africans, Yusuf Manji
kufuatia timu yake kutwaa Ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom msimu wa
2014/2015.
Katika
salamu zake za pongezi, Malinzi amesema kutwaa Ubingwa wa VPL ni jambo
muhimu na sasa wanapaswa kuanza maaandalizi kwa ajili ya michuano ya
kimataifa barani Afrika mwakani.
Klabu
ya Young Africans imetwaa Ubingwa wa Ligi Kuu nchini kwa mara ya 25
(ishirini na tano) jana, baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi
ya timu ya Polisi Morogoro katika uwanja wa Taifa huku ikiwa na michezo
miwili mikononi kabla ya ligi kumalizika.
Waziri
wa Habari, Vijana Utamuduni na Michezo, Dr. Fennela Mkangara
anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika sherehe za kukabidhi Kombe la
Ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Mei 6, 2015 katika mchezo kati ya Azam FC
dhidi ya Young Africans.
VILABU VPL VYAPIGWA FAINI, WAAMUZI WAFUNGIWA
Pia
Ruvu Shooting imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa kutoingia
vyumbani wakati wa mapumziko kwenye mechi hiyo. Adhabu hiyo imetolewa
kwa kuzingatia Kanuni ya 14(13) ya Ligi Kuu.
Stand
United imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) baada ya washabiki
wake kuwatupia chupa za maji wachezaji wa akiba wa timu ya Polisi
Morogoro katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 42(1) ya Ligi Kuu.
Naye
Meneja wa Polisi Morogoro, Manfred Luambano alitolewa kwenye benchi la
Polisi Morogoro kwa kosa la kutoa lugha za kashfa kwa mwamuzi msaidizi
namba moja Martin Mwalyanje. Suala lake linapelekwa kwenye Kamati ya
Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa ajili ya
hatua za kinidhamu.
Kipa
wa Ndanda SC, Wilbert Mweta amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya
sh. 500,000 (laki tano) kwa kumkanyanga na kutaka kumpiga mwamuzi Eric
Onoka kwenye mechi namba 155 dhidi ya Polisi Morogoro iliyochezwa Uwanja
wa Jamhuri mjini Morogoro. Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni
ya 37(5) ya Ligi Kuu. Kabla ya kufanya kitendo hicho alikuwa ameonyeshwa
kadi nyekundu.
Meneja
wa Kagera Sugar, Mohamed Hussein anapelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu ya
TFF kwa kutoa lugha ya matusi kwa waamuzi na kutaka kumpiga mwamuzi
msaidizi namba 2, Said Mnonga kwenye mechi namba 158 dhidi ya Azam FC
iliyochezwa Uwanja wa Azam Compex jijini Dar es Salaam.
Naye
Kipa Andrew Ntala wa Kagera Sugar amefungiwa mechi tatu na kupigwa
faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa kuingia kwenye vyumba vya waamuzi
na kuwatolea lugha ya matusi mazito ya nguoni baada ya mechi hiyo.
Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 37(5)(c) ya Ligi Kuu.
Mwamuzi
wa mechi kati ya Azam FC na Kagera Sugar, Stephen Makuka na mwamuzi
msaidizi namba mbili Said Mnonga wameondolewa kwenye orodha za waamuzi
wa Ligi Kuu na kufungiwa miezi 12 kwa kushindwa kumudu mchezo kwa
uzembe. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 38(1) ya Ligi
Kuu.
Pia
Kamishna wa mechi hiyo Bevin Kapufi amefungiwa mwaka mmoja kwa kutoa
taarifa isiyo sahihi. Adhabu hiyo imetolewa kwa uzingativu wa Kanuni ya
39(1) ya Ligi Kuu. Naye Kamishna wa mechi namba 159 kati ya Mbeya City
na Simba, Joseph Mapunda amepewa onyo kutokana na ripoti yake kuwa na
upungufu.
Simba
imepigwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) kwa kuzingatia Kanuni ya
14(9) ya Ligi Kuu kwa kutoingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo
(changing room) katika mechi namba 159 dhidi ya Mbeya City iliyochezwa
Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya. Pia Simba imepigwa faini ya sh. 500,000
(laki tano) kwa kutoingia vyumbani wakati wa mapumziko kwenye mechi
hiyo. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(13) ya Ligi Kuu.
Mgambo
Shooting imepigwa faini ya sh. 100,000 (laki moja) kwa kuchelewa kufika
kwenye kikao cha kitaalamu cha maandalizi ya mechi (technical meeting)
dhidi ya Ruvu Shooting. Mechi hiyo namba 161 ilichezwa Uwanja wa
Mabatini mkoani Pwani, na adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya
14(2)(a) ya Ligi Kuu.
LIGI YA MABINGWA WA MIKOA SASA MEI 9
Michuano
ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) sasa itaanza Jumamosi Mei 9, 2015
badala ya Jumamosi Mei 2, 2015 kama ilivyokua imetangazwa awali.
Uamuzi
huo umefanyika ili kutoa fursa kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) kukamilisha maandalizi ya mwisho ikiwemo ukaguzi wa
viwanja ambavyo vitatumika katika RCL na masuala mengine ya kumsingi.
Tunaomba
radhi kwa usumbufu ambao utakuwa umejitokeza kutokana na taarifa hii ya
kusogeza mbele kuanza kwa ligi, lakni pia kuzitakia kila la kheri timu
zinazoshiriki katika maandalizi yao.
Ratiba ya mashindano itatolewa/kutumwa leo kama ilivyopangwa awali.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)