kamanda wa polisi mkoa wa Arusha
Hali
ya Sintofahamu imeukumba mji wa Tengeru leo Asubuhi baada ya wanafunzi
wa chuo cha ualimu Patandi Kufunga barabara kwa muda wa masaa mawili na
kuacha shughuli za maendeleo kusimama kwa muda huku magari ya abiria
yanayokwenda katika mikoa ya Kilimanjaro,Tanga na Dar es salaam na mji
mdogo wa usa river na maeneo mengine kupata adha hiyo.
Wanafunzi hao walizuia bara bara hiyo wakishinikiza madai yao kusikiliza kwani wameshatoa malalamiko yao kwa uongozi wa chuo hicho bila ya kushughulikiwa kwa muda sasa wakiainisha kuwa wamekuwa wakipatiwa adhabu zisizo stahiki ikiwemo kurushwa kichura kuchapwa makofi huku kanuni za utumishi zikivunjwa na uongozi wa chuo hicho cha ualimu Patandi kilichopo wilayani Meru..
Wakizungumza kwa nyakati Tofauti na libeneke la kaskazini blog Mmoja wa wanafunzi Jenny Mlay alisema kuwa leo Asubuhi mkuu wa chuo alimkuta mwanafunzi mwenzao amelala bwenini akiumwa na kuacha taa ikiwa inawaka na ndipo alimpiga makofi na wao kwa umoja wao wakaamua kuingia barabarani ilikufikisha kilio chao cha muda mrefu.
Alisema kuwa kumekuwepo na unyanyasaji wa wanafunzi kwa kupewa adhabu zisizoendana na maadili ya vyuo ikiwemo kupiga magoti,kuruka kichura, na nyingine kama hizo ambazo ni kinyume na haki za binadamu na kanuni za chuo.
“Utakuta mtu anarukishwa kichura tena muajiriwa ambaye amekuja kuongeza daraja hapa chuoni huyu sio mwanafunzi wa darasa la kwanza hivyo tumefikisha ujumbe wetu mara nyingi kwa uongozi lakini hatupatiwi majibu ndio tukaamua kufunga barabara ilikufikisha ujumbe wetu kuwafikia walengwa”alisema Mlay
Mlay alisema kuwa kufuatia malalamiko yao kupuuzwa na tukio la Asubuhi la kupigwa kwa mwenzao wao wanautaka uongozi akiwemo mkuu wa chuo hicho kuachia ngazi kwani amekuwa ndio tatizo la migogoro hapo chuoni.
Nae Mkuu wa chuo hicho cha ualimu patandi Zaina Kabelwa akijibu hoja zilizotolewa na wanafunzi hao alisema kuwa ualimu wao unaishia Geti la chuo na wakishaingia chuoni hapo wanakuwa kama wanafunzi wengine wa vyuo na wanatakiwa kufuata kanuni na sheria za chuo.
Kabelwa alisema kuwa matumizi ya vifaa vya chuo yakiwemo majengo na usafi wa mazingira ni kwa kila mwanafunzi bila ya kujali huyu ni mwajiriwa au la wote wananafasi sawa kwa mujibu wa kanuni za chuo hicho
Kwa
upande wake kamanda wa jeshi la polisi mkoani hapa Liberatus Sabas
alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwataka wale wote wenye kuvunja
sheria kufuata mikondo ya sheria ikiwemo kufuata mamlaka husika ili
malalamiko yao yaeweze kupatiwa ufumbuzi na sio kuchukuwa sheria
mkononi.
Kamanda
Sabas alisema kuwa wanafunzi hao walisimamisha msafara wa magari kwa
saa mbili hadi walipotawanya na askari wake wa kituo cha usa river baada
ya kukaidi amri ya mkuu wa chuo hicho aliewataka warudi chuoni hapo
iliwaweze kukaa na kujadili mamalamiko yao.
"Nawasihi
wote wanajichukulia sheria mikononi kufuata sheria bila shuruti kwani
jeshi hilo lipo macho kwa wote wanaovunja sheria kwani sheria itachukuwa
mkondo wake bila ya kumuonea mtu"alisisitiza Sabas