UMOJA wa Katiba ya Wananchi (UKAWA),
umesema kuwa, ajenda yao kubwa sasa ni kuwahamasisha wananchi
kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapigakura na si vinginevyo. Anaandika Pendo Omary … (endelea).
Kwa mujibu wa Ukawa inayovishirikisha
vyama vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD, hawana mpango wa kushiriki
kura ya maoni ya katiba inayopendekezwa licha ya tarehe ya awali
iliyotangazwa na Rais Jakaya Kiwete kufutwa.
Jaji Damian Lubuva – Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), jana alifuta 30 Aprili mwaka huu kutumika kama “siku ya kupiga kura ya maoni kuhusu Katiba inayopendekezwa”.
Awali tarehe hiyo ilitangzawa na Rais
Kiwete kinyume cha Sheria ya Kura ya Maoni ya mwaka 2011, iliyofanyiwa
marekebisho mwaka 2013.
Kwa mujibu wa sheria hiyo, Rais amepewa
mamlaka ya kutangaza muda (kipindi). NEC imepewa mamlaka ya kutangaza
muda na siku ya upigaji kura.
Wakizungumza na MwanaHALISIOnline leo, baadhi viongozi Ukawa, wamesema “msimamo wao wa kususia kura ya maoni upo palepale.”
Dk. Willibrod Slaa – Katibu Mkuu wa Chama
Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) amesema “sisi nguvu yetu
haijapungua. Iko palepale. Tangu mwanzo tulikuwa tukihamasisha watu
kujiandikisha”.
“Chadema ndio chama kikuu pekee kilichopo
Njombe katika kuhakikisha watu wanajiandikisha. Pia tumeweka mawakala
katika uangalizi wa zoezi zima. Tunafanya haya kwa ajili uchaguzi mkuu
na sio kura ya maoni,” amesema.
Aidha, Dk.Slaa ameongeza kuwa, NEC
inapaswa kutoa ratiba mapema ili kuwapa furasa ya kujipanga mapema
tofauti na awali ambapo walipoteza fedha nyingi kutokana na ratiba za
uongo.
Magdalena Sakaya – Naibu Katibu Mku
(Bara) wa Chama cha Wananchi (CUF) amesema, “Tuna mambo makubwa mawili.
Kwanza kuhamasisha wananchi kujiandikisha katika daftari la kupiga kura.
Pili kuwekeza nguvu zetu katika suala la uchaguzi mkuu ambapo
tunahamasisha watu kujitokeza kupiga kura wakati ukifika”
“Msimamo wetu tangu mwanzo ni kutoshiriki
katika mchakato huu. Dunia nzima inajua huu mchakato ni wa CCM. Hauna
baraka za viongozi wa dini. Umegawa watanzania na kuhatarisha amani ya
nchi,”amesema Sakaya.
Ameongeza kuwa CUF na Ukawa kwa ujumla
watashiriki kura ya maoni endapo Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba
iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba itarejeshwa na maoni
yaliyopendekezwa na wananchi yatajadiliwa.
Pia Mesena Nyambabe – Katibu Mkuu wa NCCR
– Mageuzi, amesema “Tumempongeza Jaji Lubuva kutekeleza jukumu lake
kuhusu kutangaza nani anapaswa kutangaza tarehe ya kura ya maoni.”
“Lakini kusema kura ya maoni itafanyika
baada ya Julai ni kudanganya na kujichanganya. Baada ya Julai tunaelekea
kwenye uchaguzi mkuu. Kiuhalisia kura ya maoni haitakuwepo. Ikiwepo
hatutashiriki. Kwa sasa tunajiandaa na uchaguzi mkuu,”amesema Nyambabe.
Credit: http://mwanahalisionline.com
Credit: http://mwanahalisionline.com