“Nahitaji majimbo yote ya Kigoma kuchukuliwa na
ACT bila kukosa hata moja na hili hata Serukamba (Mbunge wa Kigoma
Mjini-CCM) analijua. Mwanasiasa anayetaka kuwa mbunge Kigoma lazima aje
ACT,” alisema Zitto ambaye pia alirejea kauli yake kuwa atagombea ubunge
katika jimbo jingine lakini siyo Kigoma Kaskazini.
Kauli hiyo ya Zitto inawagusa wabunge wa sasa wa
majimbo ya Kigoma ambao ni; Felix Mkosamali (Muhambwe), Moses Machali
(Kasulu Mjini), Agripina Buyogela (Kasulu Vijijini) na David Kafulila
(Kigoma Kusini), wote wa NCCR-Mageuzi na Peter Serukamba (Kigoma Mjini,
Christopher Chiza (Buyungu) na Albert Obama (Manyovu) wa CCM.
Alipoulizwa iwapo wabunge hao wa majimbo ya mkoa
huo ni miongoni mwa watu watakaohamia chama hicho alisema, “Sasa huo ni
mtizamo wenu. Ukiwa mwanasiasa lazima uwe na msingi, nataka msingi uwe
Kigoma.
Tutakutana tena kwenye chumba hiki (cha mikutano)
baadaye mwezi Novemba ili mnisute kwa kauli yangu na hapo itakuwa baada
ya matokeo kutoka. Nahitaji kushinda kila kitu.
Pia, amewatangazia vita wabunge wa majimbo manane
ya Mkoa wa Kigoma, akijigamba kuwa ili waweze kuibuka na ushindi katika
uchaguzi huo ni lazima wakubali kujiunga na ACT kwa kuwa chama hicho
kimejipanga kuyabeba majimbo yote.
“Tuna wagombea ubunge wengi wakiwamo wabunge wa
sasa ambao katika Uchaguzi Mkuu Oktoba hawatagombea kupitia vyama vyao
vya sasa. Wapo ambao hawatakwenda hata katika kura za maoni za vyama
vyao na wameshafanya uamuzi,” alisema.
Huku akizungumza kwa kujiamini, Zitto alisema
wabunge hao ndiyo sababu ya chama hicho kuwa na uwezo wa kujiendesha na
kufafanua kuwa ACT kinawakaribisha wabunge na makada wote kutoka vyama
vya Chadema na CCM.