
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ametoa ufafanuzi kuhusu suala la uandikishaji katika daftari la kudumu la wapigakura na siku maalum ya kupiga kura.
Amebainisha kuwa kutokana na hali ilivyo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC) ndio itakayotoa ratiba kamili kuhusu hatma ya upigaji kura ya
maoni.
Aidha, katika mgogoro na mgomo wa wafanyabiashara unaoendelea, amewataka
wafungue maduka yao kwa kuwa tayari Serikali imeanza kushughulikia na
kuyafanyia kazi malalamiko yao.
Akizungumza bungeni jana wakati wa kuhitimisha shughuli za mkutano wa 19
wa Bunge, alisema Serikali inatambua kuwa muda uliobaki kufikia siku ya
kupiga kura ni mfupi, lakini Tume ndiyo yenye mamlaka kwa sasa ya kutoa
ratiba kamili kuhusu tukio hilo.
“Tunatarajia Tume itatoa taarifa ya Ratiba itakayotumika kutuwezesha
kukamilisha zoezi la uandikishaji pamoja na kutoa taarifa siku za hivi
karibuni kuhusu upigaji wa Kura ya Maoni. Ni dhahiri muda uliobaki
kuanzia sasa ni mfupi lakini Tume ndiyo itakayotujulisha ratiba kamili,” alisisitiza.
Alisema Serikali kwa upande wake, imehakikisha fedha yote kwa ajili ya
ununuzi wa BVR 8,000 zimelipwa kwa NEC na matarajio ni kwamba kazi ya
kuandikisha katika mikoa mingine itaanza na kuendelea kwa kasi.
Pia, alisema wakati tume inajitahidi kufikia malengo hayo, Serikali
inaendelea na mipango ya kuelimisha wananchi kupitia redio,
televisheni, magazeti mbalimbali kuhusu umuhimu wa Katiba
inayopendekezwa ili kila mwananchi aielewe vizuri na kuweza kuipigia
kura kwa matakwa yake mwenyewe bila kurubuniwa muda utakapofika.
Alisema tume hiyo imelenga kuandikisha wapiga kura milioni 21 na
inakadiriwa kutakuwa na vituo 36,164, kila kituo kitaandikisha kwa siku
saba hadi 11 kutokana na idadi ya watu na vituo vitafunguliwa kuanzia
saa mbili hadi saa 12 jioni.
Akizungumzia suala la mgogoro wa wafanyabiashara Pinda, alisema katika
kushughulikia suala hilo, Serikali ilikutana na wafanyabiashara hao na
kukubaliana kuwa kwa sababu Serikali imeonesha nia ya kushughulikia
malalamiko na changamoto zinazowakabili wafanyabiashara nchini ni
vizuri mgomo huo ukasitishwa.
“Serikali inathamini sana mchango wa wafanyabiashara katika kukuza
Uchumi na kuchangia mapato ya Serikali. Napenda kuwahakikishia
wafanyabiashara na wananchi wote kwamba, Serikali ipo tayari kukaa
pamoja na wafanyabiashara kuzungumzia changamoto zinazowakabili na
kuzipatia ufumbuzi wa haraka,” alisisitiza.
Akizungumzia suala la mauaji ya watu wenye ulemavu (albino), alisema
itaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kiuchunguzi na kiupelelezi na
kuwakamata wote wanaohusika na mauaji hayo yaliyojirudia tena nchini na
kuwachukulia hatua za kisheria.
Alisema kwa sasa jumla ya watuhumiwa 181, wakiwemo Wanaume 171 na
Wanawake 10 walikamatwa na kuhojiwa, kati yao watuhumiwa 133
walifikishwa mahakamani na kufunguliwa kesi za mauaji na 46 kwa makosa
ya kujeruhi.
“Chanzo kikubwa cha mauaji hayo ni imani za kishirikina. Aidha,
Matukio 41 kati ya 43 yametokea katika Ukanda wa Ziwa na Magharibi,
kwani hadi sasa yametokea matukio 13 ya Mauaji Mwanza, Kagera matukio
sita (6), Tabora matukio matano (5), Mara matukio manne (4), Geita
matukio manne (4), Kigoma matukio Manne (4) Simiyu matukio matatu (3) na
Shinyanga matukio mawili (2)” alisisitiza.
Kuhusu Mahakama ya Kadhi, alisema katika Mkutano wa 18 wa Bunge Serikali
ilikusudia kuwasilisha bungeni Muswada wa Marekebisho ya Sheria
Mbalimbali na sehemu ya tano ya muswada huo, ilikusudia kurekebisha
Sheria ya Tamko la Sheria za Kiislamu.
Alisema muswada huo ni miongoni mwa Miswada minne ambayo haikupata nafasi ya kujadiliwa na Bunge. “Serikali
itatumia fursa kuendelea kushirikisha wadau mbalimbali kwa lengo la
kupanua uelewa juu ya maudhui na madhumuni ya Muswada huu”.
Pia, Waziri Mkuu alitoa pole kwa ajali zilizotokea na maafa yaliyotokana
na mvua katika mikoa ya Dar es Salaam, Mtwara na Kahama mkoani
Shinyanga.
Spika wa Bunge, Anne Makinda, alilazimika kuvunja kikao cha asubuhi cha
Bunge majira saa nne, baada ya wabunge wa vyama vya siasa vya upinzani
kugoma mijadala mingine isiendelee hadi Waziri Mkuu, Mizengo Pinda,
atakapotoa kauli juu ya mustakabali wa uandikishwaji wapiga kura na
hatima ya kura ya maoni.
Wabunge hao, pamoja na kujibiwa na Spika kuwa suala hilo, litatolewa
maamuzi wakati Waziri Mkuu akihitimisha hoja ya kuahirisha Bunge,
waligoma kukaa na wote wakasimama bungeni, na kuanza kuimba wakiwa
wamewasha vipaza sauti huku wakigonga meza wakitaka hoja yao ijibiwe
kwanza.
Chanzo cha vurugu kilianza pale, Mbunge wa Kisarawe Selemani Jafo (CCM),
alipoomba mwongozo wa Spika, akitaka Bunge hilo lisitishe shughuli
zilizopangwa na kujadili suala la kura ya maoni na namna ya kutengeneza
Katiba ya mpito kwa ajili ya uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka
huu.
Katika hoja yake hiyo, Jafo alisema kutokana na hali ilivyo ya
uandikishaji katika daftari la kudumu la wapiga kura, ni wazi kura ya
maoni haiwezi kufanyika Aprili 30, kama ilivypangwa.
Alisema ni wakati sasa Bunge hilo, lianze kujadili vipengele kama vile
mgombea binafsi, kupinga matokeo ya urais mahakamani, kuwepo kwa tume
huru ya uchaguzi na umri wa wabunge na Bunge ili viingizwe na kupitishwa
kwenye kikao cha 20 cha Bunge ili Katiba ya Mpito ipitishwe.
Wakati Jafo akitoa maelezo yake kuhusu mwongozo huo, baadhi ya wabunge
wa upinzani walikuwa wamesha vipaza sauti wakimpinga kwa madai kuwa,
suala analotaka siyo la dharura.
Baada ya maelezo hayo ya Jafo, mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema)
naye aliomba mwongozo kwa kanuni ya 47 (1) inayohusu kusimamisha
shughuli za Bunge zilizopangwa kwa siku hiyo ili jambo la dharura
lijadiliwe.
“Mheshimiwa Spika uandikishaji wapiga kura nchi nzima, haujakamilika
hata katika mkoa wa Njombe, Watanzania wapo katika sintofahamu ni lini
wataandikishwa kwenye daftari la kudumu la wapiga kura,” alisema.
Alisema suala hilo ni la dharura na lilishaombewa miongozo zaidi ya mara
moja bila majibu, hivyo si vyema Bunge hilo likaahirishwa bila kupatiwa
majibu juu ya hatma ya uandikishaji huo wa wapiga kura na kura ya
maoni.
“Tusitishe shughuli zote tuhakikishe tunajali, majibu yapatikane leo
katika mkutano huu wa Bunge, nimeomba miongozo juu ya jambo hili mara
mbili na mara zote Serikali haitoi majibu, sasa hakieleweki hapa hadi
tupatiwe majibu,” alisema Mnyika.
Alisema “Waziri Mkuu yupo hapa anaweza kutoa majibu hapa na tukajadili jambo hili hapa,” alisema Mnyika.
Baada ya Mnyika kumaliza kuomba Mwongozo, Spika Makinda alibainisha kuwa
hoja hiyo ya Mnyika haina tofauti na Jafo, na zote zipatiwa majibu na
Waziri Mkuu wakati akitoa hoja ya kuahirisha Bunge.
Hata hivyo, jibu hilo la Spika halikukubaliwa na wabunge hao wa upinzani
na ndipo mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali, alipowasha kipaza sauti
bila ruhusa ya Spika na kusema “Hoja hii haifanani na hoja ya
kwanza, ile ya kwanza inataka majibu mkutano wa 20 na hoja hii ya pili
inataka majibu mkutano huu.”
Wabunge wote wa upinzani wa vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi na CUF,
walisimama na kuwasha vipaza sauti huku wakiongea kwa nguvu kuwa hoja
hizo hazifanani na ni lazima hoja yao ipatiwe majibu kabla ya shughuli
nyingine za Bunge kuendelea.
Machali alidakia tena na kusema, “Tunataka majibu, tumechoka kuburuzwa.”
Spika Makinda aliwajibu kwa kusema “Anawaburuza nani, nimewaambia
kwamba swali lile litajibiwa leo (jana),au njooni basi nyie muendeshe
hiki kikao, kama hamtaki kukubali majibu yangu tokeni nje.”
Huku wabunge hao wakiwa bado wamesimama na kuimba kuwa wanataka majibu,
Spika alimwita Msemaji Kambi ya Upinzani kwenye Wizara ya Mawasiliano,
Sayansi na Teknolojia, ili asome maoni ya kambi hiyo juu ya Mswada wa
Sheria ya Miamala ya Kielektroniki ya mwaka 2014 na ule wa Makosa ya
Kimtandao wa mwaka 2015, lakini hakutoka.
Aidha Spika aliendelea na kumtaka Katibu ataje shughuli inayofuata,
ambaye aliisoma kwa mara ya kwanza Miswada ya Shera ya Kupata Habari wa
mwaka 2015, wa Sheria Vyombo vya Habari wa mwaka 2015, wa Sheria ya
Marekebisho ya Sheia ya Ushindani wa mwaka 2015 na wa Sheria ya Tume ya
Walimu wa mwaka 2015.
Wakati akisema hivyo, baadhi ya wabunge wa upinzani waliendelea kusema kuwa alichofanya siyo utaratibu.
Baada ya hapo aliwafafanulia wabunge kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 47
kinasema, iwapo Spika ataridhika kwamba jambo hilo ni la dharura na lina
maslahi kwa umma basi ataruhusu hoja litolewe kwa muda dakika tano, na
mjadala wa hoja utawezekana kama Spika ataridhika.
Pamoja na maelezo hayo, vurugu hizo za wabunge ziliendelea hadi alipoamua kuahirisha kikao hicho hadi jioni.

