Waziri
Mkuu aliejiuzulu Edward Lowassa amesafirisha wahariri wakuu wa vyombo
vyote vya habari toka Dar es salaam na kufanya nao mkutano maalum leo
nyumbani kwake mjini Dodoma. Katika mkutano huo kwa ufupi Lowassa
amesema yafuatayo;
1. Amesema Hahusiki lolote na sakata la Richmond na ndio sababu hata
kamati ya Mwakyembe haikuona sababu ya kumhoji. Amesisitiza kuwa cheo
cha uwaziri mkuu ndio ilikuwa lengo la kamati ya mwakyembe na spika wa
bunge kipindi hicho Samwel Sitta. Amesisitiza hicho sio kikwazo kwake
katika kuingia Ikulu kwani sakata la Richmond lilipikwa kumchafua.
Amechukua muda mrefu kuzungumzia hili la Richmond na amesema atalisema
zaidi Arusha wikendi hii.
2. Anaamini kila mtangaza nia ana makundi ya kumuunga mkono. Yeye katika
mkutano huu na wahariri leo ameambatana na Nazir Karamagi, Peter
serukamba, Diana chilolo, Hussein Bashe na wengineo huku wengi wakiwa ni
waliojeruhiwa katika serikali ya awamu ya nne akiwemo Aliekuwa DC
Igunga Elibariki Kingu. Pia aliyekuwa mkurugenzi wa HakiElimu Elizabeti
Misoki ametangazwa rasmi kuwa Mkurugenzi wa mahusiano na mawasiliano
katika timu ya kampeni ya Lowassa. Amehoji kwani akina Karamagi wana
tatizo gani na kwani wao sio binadamu?
3. Lengo kuu atakaloanza nalo ni Elimu na sio Kilimo kwanza cha serikali
ya JK. Amesema serikali ya JK ilikosea kuanza na kilimo na kuweka kando
elimu. Ametangaza kuwa sera yake ni Elimu Kwanza.
4. Kuhusu pesa anasema anapata michango ya rafiki zake na ataendelea
kupokea michango hii wakati wote wa harakati zake na haina madhara
yotote.
5.
Anasema hatahama CCM na asiyemtaka yeye CCM ndie aondoke ndani ya chama
kwani yeye ana uhakika wa kupata nafasi kuwania urais.
6. Amesema hatalipa kisasi kwa lolote lililomtokea katika siasa. Amemwachia Mungu kwani yeye ni mcha Mungu.
7.
Amesema Arusha itawaka moto tarehe 30 mwezi huu na kuwataka watanzania
kutega sikio kwani ataanika kila jambo kuhusu mustakabali wa nchi hii na
mipango yake ya kuiinua nchi kiuchumi katika miaka kumi ijayo.
Hayo ni
kwa ufupi. Wahariri wakuu katika media zote kupitia Jukwaa la Wahariri
walikuwepo, na Absalom Kibanda (New Habari) na Nevil Meena (Free Media)
ndio walikuwa waratibu wakuu wa mkutano huu.