Vyungu vyenye urembo vikionekana kuzana maji eneo la Sayansi Kijitonyama.
HALI tete imeendelea kutanda jijini Dar es Salaam, kufuatia mvua
kubwa inayoendelea kunyesha kwa siku ya tatu sasa na kusababisha
mafuriko hasa katika maeneo ya mabondeni huku familia nyingi zikikosa
makazi baada ya nyumba wanazoishi kujaa maji na vitu vyao, vikiwemo
samani, kusombwa na maji.Maeneo ya Jangwani na Posta yameonekana kuwa miongoni mwa maeneo yaliyoathirika zaidi kwa mvua hizo. Maeneo mengine ni Msasani, Mwananyamala, Masaki na Tegeta, Sayansi, Sinza, Tabata, Tandale na Mbagala.
Taarifa ya jeshi la polisi kupitia vyombo mbalimbali vya habari inasema kuwa watu wapatao wanane wamepoteza maisha na wengine mamia wakikosa makazi kufuatia mfululizo wa mvua hizo zinazoendelea kunyesha mpaka sasa jijini hapa.
Watafiti wa mambo wametaja vitendo vya watu kuziba mitaro ya maji kwa kutupa taka ovyo, kuzibua chemba za maji machafu wakati wa mvua kuwa ni moja ya sababu zilizochangia kufurika maji katika mitaa mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam na kusababisha adha kubwa.
Kwa upande mwingine vijana wamekuwa wakijipatia fedha kwa kuwavusha watu maeneo mbalimbali yaliyojaa maji kwa gharama ya kati ya Sh 500 hadi 2,000.
Kwa upande wake mamlaka ya hali ya hewa nchini imetoa taarifa kwa umma kwamba, mifumo ya hali ya hewa inaonesha kuwa, hali ya mvua inatarajiwa kuendelea kunyesha katika baadhi ya sehemu hadi tarehe Mei 20 mwaka huu.
Tayari serikali kupitia jeshi la polisi imetangaza kuifunga kwa muda barabara ya Morogoro eneo la Jangwani kufuatia eneo hilo kujaa maji kiasi cha kuyafanya magari kushindwa kuingia wala kutoka.
Aidha serikali pia imewataka wananchi jijini kuchukua tahadhari kufuatia mvua hizo kubwa zinazoendelea kunyesha na kuleta maafa.