MKURUGENZI
wa Kampuni ya Msama Promotions ambayo ndio inaandaa matamasha ya Pasaka
na Krismasi, Alex Msama amekemea waimbaji wa muziki wa Injili Tanzania
kufanya kazi ya Mungu na kuachana na siasa ambazo zinawaondoa kwenye
uinjilishaji.
Msama
ameyasema hayo wakati tukielekea kwenye uchaguzi Mkuu wa Madiwani,
Wabunge na urais unaotarajia kufanyika Oktoba 25 mwaka huu.
Msama
anasema karipio hilo linawahusu pia viongozi wa dini wakiwamo
Wachungaji na Maaskofu ambao wanaonesha nia ya kutaka kuwania uongozi
wa kisiasa katika nafasi hizo tatu.Sababu
za Msama kukemea waimbaji wa Injili kujihusisha na Wanasiasa wakiwemo
wagombea urais, kuna baadhi ya waimbaji wametunga nyimbo za ‘kuwatukuza’
wagombea urais wakati wao wanatakiwa muda wote kumtukuza Mungu na si
binaadam wenzao.
“Waimbaji
tunatoka katika mstari, kwani Mungu anawategemea kufikisha ujembe wake
kwa lengo la kuachana na machukizo ambazo yanapoteza mwelekeo wa jamii
mbalimbali ambazo zinahitaji maono ya Wainjilisti,” alisema Msama na
kuongeza. “Waimbaji
ambao ninashirikiana nao katika kufikisha huduma ya neno la Mungu,
nashangaa wanatoka katika mstari nawaomba wamrudie Mungu kwani wanapotea
wakiwatumikia mabwana wengine.” Alisema.
Anasema
kitendo wanachokifanya waimbaji na wachungaji ni kinyume na huduma
ndani ya mioyo yao kwa sababu wanachokifanya si sahihi. Anafafanua
kwamba kazi ya muziki wa injili ni kuhubirisha, waimbaji ni Wainjlisti
wanawatoa waovu kwa shetani na kuwapeleka kwa Mungu ambaye ndiye
tegemezi kwa binadamu wote.
“Ni
jambo la kusikitisha sana, wanamhuzunisha bwana Yesu, alipoondoka
kwenda mbinguni aliwaambia wafuasi wake, nendeni ulimwenguni kote
mkaihubiri injili yangu, mwenye kuamini ataokoka na asiyeamini
ameangamia,” alieleza Msama.
Anasema
kwa kufanya hivyo waimbaji hao ndio wanahubiri uovu kwa kuwapamba
wachafu na kuwafananisha na Yuda Eskariot aliyemsaliti bwana Yesu kwa
ajili ya pesa na kuwataka waliofanya hivyo waache mara moja.
Msama
anaendelea kueleza na kufafanua kupitia maandiko matakatifu kwamba ya
Kaisari wamuamuachie Kaisari, mwenye kupewa sifa na wao ni Mungu peke
yake, mwanadam hawezi kupewa sifa na kuinuliwa kwa sifa.
Pia
anawakemea wagombea urais waache kuwatumia waimbaji wa Injili na
kujificha kwenye Kanisa kwamba ndio sehemu ya kuombea kura na kugawa
pesa Makanisani, Mungu hahongwi na waache pia kumchokoza Mungu kwani
akichukia zaidi mwisho wake ni mbaya.
Anasema
siasa na dini ni vitu viwili tofauti kwani kwenye siasa uongo ni mwingi
ambao katika uinjilishaji hautakiwi kwa sababu unakwenda tofauti na
maandiko matakatifu ya Mungu. “Nahuzunishwa
na wanaotumia mfumo huo kwa sababu siasa inayohubiriwa ni ya kumjenga
mgombea urais na kumpamba, wakati katika maandiko matakatifu hakuna
mambo ya kupambana kama inavyofanyika sasa,” alisema.
Anaeleza kwamba Wachungaji wanasahau kazi zao ambazo ni kuwachunga kondoo wa Mungu na kuhubiri Injili na si lingine lolote. “Nia
zao wakazitangaze huko na wakiendelea nitawaweka hadharani kwani
nitawaumbua kwa kuwaeleza kwamba hawafai kuwa Marais kwa mtindo
wanaoutumia,” alisema. Msama
ndiye ‘anayedili’ na waimbaji wa muziki wa injili waache na watubu
sambamba na kukiri makosa yao kwa Mungu na waachane na dhambi ambayo ni
kero kwa Mungu.
Wachungaji
wanaojielekeza kwenye siasa waache mpangilio huo kwa sababu haiwezekani
kuwatumikia mabwana wawili na kazi yao kwa Mungu ni Injili pekee. “Ukijikita
huko utakuwa huna muda wa kumtumikia Mungu, siasa inasababisha kusema
uongo wakati uchungaji una heshima kubwa,” alisema Msama.

