WAANDISHI WA HABARI WATAKIWA KUEPUKA LUGHA ZA CHUKI
Meza kuu. (Picha zote na Geofrey Adroph wa Pamoja blog).
Mshehereshaji
wa Semina Bi. Rose Mwalongo akiwakaribisha washiriki wote waliofika
kwenye semina ya siku mbili iliyoandaliwa na shirika lisilo la
kiserikali nchini la International Association of women in radio and
television (AWRTT) kwa kushirikiana na Ethical Journalism Network ambapo
wamewakutanisha wanahabari mbalimbali kutoka nchini Tanzania pamoja na
nchi za Afrika.
Bi.
Rose Haji Mwalimu kutoka IAWRT Tanzania akifungua semina kwa kwa
washiriki ambao walikuwa ni wanahabari (hawapo pichani) mbalimbali
kutoka nchini Tanzania pamoja na nchi za Afrika wa pili kutoka kushoto
ni Rais wa IAWRT Bi. Rachael Nakitare, wa pili kutoka kulia ni Bi.
Elisabeth Scwabe-Hansen pamoja na Mkurugenzi wa Ethical Journalism
Network (EJN).
Rais
wa IAWRT Bi. Rachael Nakitare akitoa semina kwa wanahabari namna ya
kusimama katika ukweli na uwazi na pia kuepuka lugha ambazo zinaweza
kuleta chuki kwa jamii, na baadae kusababisha machafuko kwenye Uchaguzi
mkuu wa 2015.
Bi.
Elisabeth Scwabe-Hansen kutoka ubalozi wa Norway akiwasisitiza
washiriki wa semina hiyo kuwa makini kipindi chote wanapochukua au
kutafuta taarifa ili kuondoa vurugu kwa nchi hasa Tanzania inayotegemea
kufanya uchaguzi mwaka huu.
Mkurugenzi
wa Ethical Journalism Network (EJN), Aidan White akitoa semina kwa
wanahabari pamoja na wadau wa habari (hawapo pichani) kuhusu matumizi
mazuri ya uandishi hasa kwenye hiki kipindi cha Uchaguzi.
Baadhi ya washiriki wa semina.
Rais wa Shirikisho la waandishi wa Habari Afrika (FAJ), Mohamed Garba.
Mkurugenzi
wa Uwezeshashi na Uwajibikaji wa LHRC, Bi. Imelda Lulu Urio akielezea
kuhusu vyombo vya habari vya Tanzania vilivyoanza kuonekana kama kuna
aina ya lugha ambazo hazikuwepo hapo awali ambapo amesema kuwa ni wakati
sasa wa kuanza kuzuia maana zinaleta chuki kwa taifa hasa suala la
udini ambalo limeonekana kushika kasi hapa chini Tanzania.
Bi. Irene Burungi Mugisha kutoka IAWRT nchini Uganda akizungumza jambo.
Wadau wakifuatilia mada kwa umakini.
Mhariri
mkuu wa gazeti la The New Times la nchini Rwanda, Bw. Kennedy Ndahiro
akitoa mada kwa wanahabari pamoja na wadau wa habari waliohudhuria
kwenye semina ya matumizi mazuri ya vyombo vya habari kuelekea uchaguzi
mkuu unaotegemea kufanyika mwaka huu.
Rais
wa Umoja wa waandishi nchini Uganda, Bi. Lucy Ekadu akiwaasa waandishi
wa habari kuwa makini katika utoaji wa habari katika kipindi hiki cha
uchaguzi mkuu unaotegemea kufanyika mwaka huu na pia kutoa elimu ya
msingi kwa wanahabari ili kutochochea vurugu.
Mhadhiri
kutoka chuo kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Ayoub Rioba akitoa semina kwa
washiriki (hawapo pichani) akiwasilisha mada yake kwenye semina
iliyofanyika kwenye hoteli ya Peacock jijini Dar.
Mshiriki Borry Mbaraka akiuliza swali kwa watoa mada.
Rais wa IAWRT, Bi. Rachael Nakitare (wa tatu kutoka kushoto) akiuliza swali kwa mtoa mada (hayupo pichani).
Mtafiti wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Patience Mlowe akiwasilisha mada yake kwa wanahabari(hawapo pichani).
Mhariri
Mtendaji wa Gazeti la Tanzania Daima, Neville Meena akiuliza swali kwa
mmoja wa watoa mada wakati wa semina iliyofanyika jana katika hoteli ya
Peacock jijini Dar.
Mweka hazina kutoka IAWRT Tanzania, Razia Mwawanga akikazia jambo kwenye semina ya wanahabari.
Wadau wakifuatilia kwa umakini mada.
Washiriki wa Semina hiyo wakiwa katika picha ya pamoja.
Na Mwandishi wetu
Ikiwa
Tanzania inajiandaa kwa ajili ya zoezi la uchaguzi mkuu wa Rais,
Wabunge na Madiwani, waandishi wa habari nchini wameaswa kujiepusha na
lugha za chuki pamoja na uchochezi kipindi chote cha uchaguzi jambo
ambalo linaweza kusababisha machafuko kama inavyoonekana katika nchi
mbalimbali barani Africa na duniani.
Rai hiyo imetolewa jana
jijini Dar es salaam katika semina ya siku mbili iliyoandaliwa na
shirika lisilo la kiserikali nchini la International Association of
Women in Radio and Television (IAWRT) kwa kushirikiana na Ethical
Journalism Network (EJN) ambapo wamewakutanisha wanahabari mbalimbali
kutoka nchini Tanzania pamoja na nchi za Afrika mashariki kwa lengo la
kujadili masuala yanayohusiana na lugha za chuki kwa vyombo vya habari
vya Afrika pamoja na madhara yake kwa wananchi.
Akifungua warsha
hiyo mgeni rasmi ambaye ni Raisi wa shirikisho la wanahabari Africa
(FAJ) Bw. Mohamed Gabra amesema kuwa moja ya mambo ambayo yamekuwa
yakisababisha machafuko makubwa katika nchi nyingi za Afrika na duniani
kwa ujumla ni lugha zinazotumika na wanahabari wakati wakiripori baadhi
ya habari lugha ambazo amesema kuwa zimekuwa zikileta chuki baina ya
watu na mwisho wake kusababisha madhara makubwa ambayo yangeweza
kuepukika kama hatua zingechukuliwa mapema.
Ametolea mifano kwa
nchi kama Rwanda, Kenya, na nchi nyingine za ulaya ambazo zimewahi
kuingia katika machafuko ya kisiasa katika kipindi cha uchaguzi kutokana
na vyombo vya habari pamoja na wanahabari wenyewe kutumia kalamu zao
kuwajengea chuki wananchi na mwisho kusababisha kuibuka kwa machafuko
makubwa.
Amesema kuwa ili kuhakikisha kuwa Tanzania inafanya
uchaguzi mkuu kwa mafanikio na amani ni lazima wanahabari wahakikishe
kuwa wanasimama kwenye ukweli na kuhakikisha kuwa wanawaambia wananchi
kile ambacho kinatokea na sio kujenga na kutengezeza maneno ambayo
mwisho yatasababisha chuki kwa watanzania.
Awali akizungumza
wakati wa kufungua warsha hiyo Rais wa (IAWRT) Bi. Rachael Nakitare
amesema kuwa ni lazima kipindi hiki cha Tanzania kuelekea uchaguzi mkuu
ni kipindi cha wanahabari kusimama katika ukweli,uwazi na kuepuka lugha
ambazo zinaweza kuleta chuki kwa jamii,na baadae kusababisha machafuko.
Baadhi
ya watu waliotoa mada katika warsha hiyo ni pamoja na wakili na
Mkurugenzi wa uwezeshaji na uwajibikaji kutoka kituo cha sheria na haki
za binadamu LHRC Bi. Imelda Lulu Urio ambapo pamoja na mambo mengine
ameelezea jinsi vyombo vya habari vya Tanzania vimeanza kuonekana kama
kuna aina ya lugha ambazo hazikuwepo hapo awali ambapo amesema kuwa ni
wakati sasa wa kuanza kuzuia mambo hayo ili kuepuka mambo makubwa ambayo
yanaweza kujitokeza hapo baadae.
Wengine waliopata nafasi ya
kuchangia katika warsha hiyo ni mwandishi mkongwe nchini ambaye ni
Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM), Dk. Ayoub Rioba
ambapo amesema kuwa katika chaguzi mbalimbali katika nchi za Afrika kwa
sasa wanasiasa wamekuwa wakiwatumia wanahabari kutaka kujinufaisha wao
kisiasa bila kujali madhara ambayo yanaweze kutokea endapo wanahabari
watakiuka maadili ya taaluma zao.
Baadhi ya wanahabari kutoka
mataifa ya nje ya Tanzania kama Kenya, Uganda,wamesema kuwa hakuna
tofauti kubwa sana kati ya ufanyaji wa kazi za wanahabari zinazofanywa
nchini Tanzania na mataifa yao bali tofauti iliyopo ni sheria
zinazowaongoza wanahari katika mataifa hayo.