https://play.google.com/store/apps/details?id=com.blog.ya.watanzania


.

.

.
  • Latest News

    .

    Kibano cha wagombea urais CCM hiki hapa


    Dar/Mikoani. Masharti yaliyomo katika fomu za wagombea urais za CCM huenda yakawa mtihani kwa baadhi yao, hasa katika kipengele kinachohoji iwapo mgombea aliwahi kujiunga na chama kingine cha siasa zaidi ya Tanu na Afro Shiraz Party (ASP).
    Wagombea hao jana waliendelea kusaka wadhamini huku Makongoro Nyerere, akieleza kuwa kuna ugonjwa wa kuvunja kanuni na Stephen Wasira akisema hakuna mafisadi ndani ya CCM wakati Dk Gharib Mohamed Bilal na Samuel Sitta wakirejesha fomu.
    Fomu hizo, ambazo wagombea 34 wamezijaza na wanatakiwa kuzipeleka mikoa mbalimbali kutafuta wadhamini, ndizo zitakazotumika kujadili makada hao na kuwachuja hadi kubakia wagombea wasiozidi watano ambao watapelekwa Halmashauri Kuu na baadaye Mkutano Mkuu kwa ajili ya kupigiwa kura kupata mwanachama atakayepeperusha bendera ya CCM.
    Kwa mujibu wa fomu hizo ambazo Mwananchi imepata nakala zake, wagombea hao watatakiwa waeleze iwapo waliwahi kukihama chama hicho kikongwe au ASP, kutaja jina la chama walichojiunga nacho na kueleza walikaa huko kwa muda gani.
    Wagombea watakaotakiwa kutoa maelezo kwenye kipengele hicho ni mwanasiasa mkongwe, Stephen Wasira na mbunge wa Afrika Mashariki, Makongoro Nyerere.
    Makada hao wawili waliihama CCM wakati wa uchaguzi mkuu wa kwanza tangu kurejeshwa kwa siasa za vyama vingi nchini mwaka 1995, na kuhamia NCCR-Mageuzi na wote walishinda ubunge.
    Hata hivyo, ubunge wa Makongoro ulitenguliwa na mahakama wakati Wasira alimaliza kipindi chake cha miaka mitano.
    Hata hivyo, kigezo hicho ni sehemu tu ya maswali yaliyowekwa kwenye fomu hiyo na itategemea jinsi watakavyojieleza kukidhi Kamati Kuu ya CCM ambayo inaundwa na vigogo 34.
    Vilevile fomu hizo zinawataka makada wanaoomba kuteuliwa kuwania nafasi hiyo ya juu nchini, kueleza iwapo waliwahi kuadhibiwa na chama au na jumuiya ya chama kwa kosa lolote.
    Kipengele hiki kinaweza kuwabana wagombea sita waliopewa onyo kali na Kamati Kuu kwa kuanza kampeni mapema na kuhusiana na vitendo vinavyokiuka maadili.
    Wagombea walioadhibiwa kwa kosa hilo ni Wasira na mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye. Wengine ni January Makamba, ambaye ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Taknolojia, William Ngeleja (mbunge wa Sengerema) na Bernard Membe (Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa).
    Pia fomu hizo mbali na kuwataka wagombea kukusanya wadhamini 450 katika mikoa 15, mitatu kati yake ikiwa ya Zanzibar, zinamtaka kila mmoja kueleza iwapo aliwahi kupatikana na hatia mahakamani ya kukwepa kulipa kodi yoyote ya Serikali na kama aliwahi kufanya hivyo, ataje kodi gani na alipewa adhabu gani.
    Wagombea hao pia wanatakiwa kueleza elimu, uzoefu katika uongozi, michango yao katika chama na kueleza iwapo wamewahi kushtakiwa na kuhukumiwa kwa makosa ya jinai, kosa lenyewe na adhabu waliyopewa.
    Makada hao wanatakiwa kukiri kusoma na kuelewa sera za chama hicho, kukiri kuzitekeleza ndani ya vikao na mahali popote.
    Pia wanatakiwa kuapa kwamba hawatazikosoa sera hizo nje ya vikao vya chama na kwamba watashirikiana na mgombea yeyote wa CCM atakayeteuliwa na kwamba watakuwa waaminifu kuhakikisha CCM inashinda.
    Baada ya kujaza fomu hizo, wagombea hao waliendelea kusaka wadhamini katika maeneo mbalimbali nchini huku wawili kati yao wakiwa wamekamilisha ngwe hiyo na kurejesha fomu zao Makao Makuu ya CCM Dodoma jana.
    Katika kuendelea kusaka wadhamini, jana Makongoro Nyerere jana aliendelea kukosoa viongozi na wanachama wa CCM, akisema wana tatizo la kuvunja kanuni, huku Stephen Wasira akisema hakuna mafisadi ndani ya CCM bali neno hilo hutumika kukashifiana.
    Jana makada wawili wa chama hicho, Gharib Mohamed Bilal, ambaye ni Makamu wa Rais, na Samuel Sitta, ambaye ni Waziri wa Uchukuzi, walirejesha fomu zao baada ya kukamilisha kazi ya kusaka wadhamini kwenye mikoa 12 ya Bara na mitatu ya visiwani, huku wagombea wengine wakiendelea na kazi hiyo kwenye mikoa tofauti.
    Akizungumza mkoani Arusha ambako alienda kutafuta wadhamini jana, Makongoro alisema CCM ina maradhi kwa baadhi ya viongozi na wanachama wake kuvunja kanuni na taratibu kwa makusudi ili kukidhi maslahi yao binafsi.
    “Uchaguzi wa mwaka huu ni fursa ya chama kujisahihisha na kurejea katika misingi yake ya uongozi kuwa dhamana badala ya fursa ya kujinufaisha kiasi cha watu kuwa tayari kutumia fedha na hila kupata nafasi ya kuliongoza Taifa,” alisema mtoto huyo wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
    Alionya kuwa iwapo CCM itashindwa kudhibiti hulka ya kutumia fedha kununua fursa ya uongozi, chama hicho kitapoteza siyo tu haiba machoni mwa umma, bali kitakabiliwa na hatari ya kupotea katika ulingo wa siasa nchini kwa sababu wananchi watakichoka na kukiweka pembeni.
    “Bila kuchukua hatua, kuna muda utafika wana CCM tutaanza kukitafuta chama hiki kila sehemu hadi mifuko mwetu na hatutakipata kwa sababu kitakuwa kimeshaporwa na vibaka,” alionya Makongoro, ambaye hotuba yake ya kutangaza nia ilichambua baadhi ya wagombea na udhaifu wao.
    Alisema ‘vibaka’ hao wako tayari na wamekuwa wakivunja kanuni na taratibu za chama katika kuwania uongozi kwa kununua wajumbe wa vikao vya maamuzi, kujiundia makundi nje ya utaratibu wa chama na kuanza kutoa ahadi badala ya kusubiri ilani ya uchaguzi itakayopitishwa na mkutano mkuu siku moja, kabla ya uteuzi wa mgombea.
    Akitumia kauli mbiu yake ya “turejesheeni chama chetu”, Makongoro alisema CCM hivi sasa kimegeuka chama cha matajiri wachache wenye uwezo wa kutumia fedha zao kuunda makundi aliyosema anayachukia kwa sababu yanakidhoofisha chama hicho tawala.
    Huku akijipigia debe, Makongoro, mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala), alisema ili kiwe salama, CCM inapaswa kuhakikisha inamteua mgombea anayechukia makundi na asiyetumia fedha kujikusanyia kundi la wafuasi, wapambe na wana mtandao, kama yeye.
    Katika hatua nyingine Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Wasira amesema ndani ya CCM hakuna mafisadi bali neno mafisadi ni msamiati unaotumiwa na wapinzani kama njia ya kuwakashifu makada wa chama hicho tawala.
    Wasira alitoa kauli hiyo wakati alipotakiwa na waandishi wa habari kueleza namna atakavyopambana na mafisadi ikiwa atapa fursa ya kuliongoza Taifa.
    Wasira alibainisha kuwa katika mjidala mbalimbali swali la ufisadi halipaswi kulizungumza kwa kuwalenga watu na badala yake linapaswa kujadiliwa kama hoja na kutafutiwa ufumbuzi kama ilivyo suala la umasikini na uwajibikaji.
    “Ninavyofahamu mimi ndani ya CCM hakuna mafisadi, lakini kama hoja ufisadi sitaifumbia macho,nitazungumza na kuishugulikia,” alisema Wasira.
    Kukomesha umaskini
    Mkoani Mara, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba amewataka wananchi kumpa nafasi ya kuwa Rais atakomesha umaskaini.
    “Umasikini ni matokeo ya matabaka mawili nchini, tabaka la walio nacho na wasiokuwa nacho, huku tabaka la wasiokuwa nacho likionekana kuwa kubwa sana. Siyo bure kuna tatizo ambalo linahitaji tiba,” alisema Mwigulu.
    Ndengo ampigia debe Lowassa
    Mgombea mwingine wa urais, Boniphace Ndengo jana alifika ofisi za CCM wilayani Butiama na Musoma Mjini na kupata zaidi ya wadhamini 90 kati ya 30 wanaohitajika.
    “Sikutegemea kupata wadhamini wengi kiasi hiki, kati ya wagombea waliofika hapa kutafuta wadhamini kuacha Edward Lowassa, hakuna ambaye amefikia wingi wa wadhamini niliopata mimi,” alisema Ndengo.
    Ndengo alisema kama Kamati Kuu ya CCM inatambua, inatakiwa kukata wagombea wote na kubakiza jina lake na aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowasa ili waingie katika kinyang’anyiro cha urais
    “Naamini mmenielewa nimemaanisha nini... waache majina mawili tu, halafu muone kitakachotokea katika nchi hii hakika nchi itakuwa na neema ya ajabu,” alisema Ndengo.
    Billal, Sitta warejesha fomu
    Dodoma. Makamu wa Rais, Dk Mohamed Billal na Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta jana walikuwa wa kwanza kurudisha fomu ya kuomba kuteuliwa na CCM kugombea urais.
    Dk Bilal, aliyechukua fomu Juni 4 na kurejesha jana saa 7:30 mchana, alisema shughuli ya kutafuta wadhamini ilienda vizuri na wala hakukuwa na kushikana mashati wala kutukanana na mtu.
    “Lilikuwa salama, murua kabisa, hakuna tatizo lolote, hatukutukanana, hatukushikana masharti. Tumelifanya kwa uadilifu mkubwa,” alisema.
    Basi la kukodi
    Sitta, aliyefika katika ofisi za CCM saa 2:00 asubuhi akiongozana na mkewe, alikanusha habari ambazo alisema ameziona kwenye baadhi ya mitandao kuwa amenunua nje ya nchi basi ambalo alitumia kuzunguka mikoani kutafuta wadhamini.
    “Basi hili nilikodisha kutoka Arusha, mtoto wangu Benjamin akachukua vitu vya nyumbani kwangu na kuvifunga humu,” alisema na kuongeza kuwa basi hilo limempunguzia gharama kwa sababu lilitumiwa na timu nzima aliyokuwa nayo.
    Alisema alikwenda kukusanya sahihi za wadhamini katika mikoa 21 badala ya 15.
    Mwanafunzi wa Mzumbe
    Katika hatua nyingine, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Morogoro, Maliki Malupu (33) amechukua fomu ya kuomba kuteuliwana CCM kuwania urais na kusema siku atakayorudisha fomu atatangaza rasimu ya baraza lake la mawaziri.
    Maliki alisema kwa kutangaza baraza mapema kutarejesha uwajibikaji na ushirikishwaji wa wananchi na kupata mapendekezo yatakayowezesha kupata baraza lenye tija.
    “Nitakaporejesha fomu nitatangaza rasimu ya baraza la mawaziri ili kuwapata mawaziri wawajibikaji na kuweka ushirikishwaji,” alisema.
    Habari hii imeandikwa na Geofrey Nyang’oro, Sharon Sauwa, Peter Saramba, Florence Focus, Mwananchi
    https://play.google.com/store/apps/details?id=com.blog.ya.watanzania

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: Kibano cha wagombea urais CCM hiki hapa Rating: 5 Reviewed By: Unknown
    Scroll to Top