Dar/Dodoma. Bunge la 10 likielekea ukingoni baada ya kupitisha Bajeti ya Serikali leo, mambo matatu mazito yametajwa kama ‘madudu’ yaliyoleta mtikisiko na kuonekana kama ishara ya kuisimamia Serikali na kusababisha baadhi ya mawaziri kupoteza nafasi zao.
Mambo hayo ni matokeo ya ripoti za Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG), Operesheni Tokomeza na ufisadi katika akaunti ya Tegeta Escrow.
Hata hivyo, pamoja na kutaja kashfa hizo, baadhi ya wabunge waliozungumza na Mwananchi wamelichambua Bunge hilo kwa mitazamo tofauti baadhi wakimsifia Spika Anne Makinda kuwa alisimamia kanuni na wengine wakimkosoa kwa kuilinda Serikali.
Bunge hilo lililozinduliwa Novemba 18, 2010 kwa Rais Jakaya Kikwete kulihutubia, anatarajia kulihutubia tena kwa hotuba ya mwisho, kati ya Julai 9 na 10, mwaka huu na kulivunja kwa kwa mujibu wa sheria kupitia Tangazo la Serikali (GN).
Ripoti ya CAG
Mwaka 2012, Bunge hilo likiwa na miaka miwili tu, CAG alitoa ripoti iliyoonyesha ufisadi mkubwa Serikalini na mawaziri kushindwa kuwajibika kisiasa kusimamia mali za umma.
Ripoti hiyo ilizua mjadala mzito bungeni na wabunge wakashinikiza baadhi ya mawaziri wajiuzulu kutokana na kushindwa kuwajibika.
Baada ya mvutano mkali Rais Kikwete alifanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri baada ya kuwatema mawaziri sita na naibu mawaziri wawili.
Operesheni Tokomeza
Sakata jingine lililoteka Bunge hilo ni ripoti ya Operesheni Tokomeza Ujangili iliyoanzishwa na serikali kwa lengo la kukomesha ujangili nchini.
Operesheni hiyo ililalamikiwa na wabunge kuwa utekelezaji wake ulivunja sheria, kanuni na taratibu.
Bunge kupitia kamati ndogo iliyotokana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira ilichunguza operesheni hiyo na kubaini uvunjifu mkubwa wa sheria.
Katika sakata hilo mawaziri wanne walitimuliwa na Januari 19, 2014 Rais Kikwete akateua wawili wapya na naibu mawaziri wanane, huku akiwapandisha vyeo manaibu mawaziri wanne kuwa mawaziri kamili.
2. Akaunti ya Escrow
Sakata la uchotwaji wa fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow liliibuliwa na Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR- Mageuzi), David Kafulila baada ya kufichua ufisadi uliohusisha uchotwaji wa Sh306 bilioni kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Katika sakata hilo, mawaziri wawili walipoteza nyadhifa zao pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali baada ya Ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuwahusisha na sakata hilo.
Maofisa wengine kadhaa wa Serikali walisimamishwa au kufunguliwa mashtaka kutokana na kuhusika kwao kwenye ufisadi huo.
Kauli za wabunge
Mbali na matukio hayo, baadhi ya wabunge wamesema katika Bunge hilo walijitahidi kuwa wamoja katika masuala yanayoligusa Taifa, ingawa wakati mwingine walitofautiana kwa sababu kadhaa zikiwamo za kiitikadi.
Moja ya mambo waliyoainisha kama kasoro za Bunge hilo ni usimamiaji usioridhisha wa Serikali katika utekelezaji wa bajeti unaosababisha fedha zinazotengwa kutofika kwa wakati, kutofika kabisa au kufika pungufu katika maeneo zilikopangwa.
Mbunge wa Gando, Khalifa Suleiman Khalifa (CUF), alisema pamoja na kumpongeza Spika Anne Makinda kwa kutekeleza mambo mengi yaliyopendekezwa, kuna baadhi ya mambo ambayo yameachwa bila ya kujua iwapo ni kwa makusudi au kwa bahati mbaya.
Alipoulizwa ni mambo gani alisema baadhi ya maazimio ya Bunge kuhusu sakata la Escrow hayajafika mwisho.
Mbunge wa Makunduchi (CCM), Samia Suluhu Hassan alisema Bunge la 10 lilikuwa na changamoto za vijana ambao walikuwa wakiwachemsha, lakini pamoja na yote walishindana ndani ya ukumbi, lakini nje ya bunge wote walikuwa wamoja.
Alisema mafanikio ya Bunge hilo, wabunge watakaokuja katika Bunge la 11 wanatakiwa kuyaendeleza.
Alimsifu Spika Makinda kwa kazi nzuri na kumwelezea kuwa hakuwa akibabaika inapotokea presha za wapinzani hata ilipotokea wanasusia vikao.
Kwa upande wake Mbunge wa Mbozi Magharibi, David Silinde (Chadema) alisema Bunge la 10 linamaliza muda wake likiwa limeweka heshima kubwa kwa Watanzania kwa kushughulikia kashfa kubwa za ufisadi.
Silinde alitolea mfano wa masuala ya Escrow, Operesheni Tokomeza na mengine ambayo yaliibuliwa katika bunge hilo alilosema lilikuwa limesheheni vijana waliokuwa na mchango mkubwa katika kuibua mambo ya msingi.
Hata hivyo, alisema kuwa hawakufikia mwisho kutokana na maazimio mengi ya Bunge kuachwa bila ya kutekelezwa kama ilivyokusudiwa.
Akizungumzia spika ajaye, Silinde alipendekeza awe walau na taaluma ya sheria ili aweze kujua mambo ya kanuni na sheria kwa upana wake.
Mbunge mwingine kijana, Moses Machali (Kasulu- NCCR-Mageuzi) alisema Bunge la 10 halikuwa la msisimko kwa kuwa Spika Makinda alikuwa akiibeba zaidi Serikali na CCM na chombo hicho kushindwa kuibana Serikali pale ilipokosea.
Alisema Spika wa Bunge la Tisa, Samuel Sitta alikuwa akitoa nafasi sawa ukilinganisha na Makinda, hali aliyosema ilisababisha Bunge kuyumba.
Kwa upande wake, Prudencia Kikwembe (Viti Maalumu – CCM) alisema Bunge hilo lilifanya kazi kwa nafasi yake lakini likakabiliwa na changamoto ya ushabiki wa vyama badala ya maslahi ya Taifa.
Mbunge wa Lindi Mjini (CUF), Salum Barwani yeye analia na mfumo wa kikatiba ambao anasema kuwa ulisababisha Bunge kuwa sehemu ya Serikali.
Barwani pia alieleza kuwa hata Spika wa sasa alishindwa kutimiza majukumu yake ipasavyo kutokana na mfumo wa kikatiba uliopo.
Akitoa maoni yake kuhusu Spika ajaye, alisema awe ni kiongozi mwenye busara lakini atambue kuwa chombo hicho ni mhimili unaojitegemea.
Hezekia Chibulunje, (Chilonwa – CCM) alisema Bunge la 10 lilikuwa la ushirikishwaji kwa kuwa uchangiaji ulikuwa mkubwa na Spika alitoa nafasi kwa kila upande bila upendeleo.
Alisema baadhi ya wabunge walikuwa makini kuwasilisha ujumbe kwa kuwa walikuwa wakionekana moja kwa moja kupitia runinga.
Mbunge wa Mji Mkongwe (CUF), Ibrahim Saanya alisema Bunge limefanya kazi yake lakini tatizo linakuja katika utekelezaji wa bajeti.
Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila Kigoma (NCCR-Mageuzi) alisema sehemu kubwa ya Bunge la 10 lilitawaliwa na vijana na wameweza hiyo kazi.
Alisema kuwa uchache wa wapinzani umewafanya wawe wanyonge katika kufikia uamuzi wa jumla.
Murtaza Mangungu (Kilwa Kaskazini, CCM), alisema Bunge hilo lilikuwa la mafanikio kwa kuwa mengi yalitimizwa na kwa kuwa walikuwa wanaonekana kupitia TV, walifanya hadaa ili kuwaaminisha wananchi masuala ambayo baadhi ni ya uongo na hayawezekani.
Imeandikwa na Fidelis Butahe, Ibrahim Bakari na Habel Chidawali
CREDIT MWANANCHI