Hai. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe
amehukumiwa kulipa faini ya Sh1 milioni au kwenda jela mwaka mmoja baada
ya kupatikana na hatia ya kumshambulia mwangalizi wa Uchaguzi Mkuu
mwaka 2010.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi wa
Wilaya ya Hai, Denis Mpelembwa. Mbowe, ambaye ni Mbunge wa Hai alilipa
faini hiyo iliyochangwa chapchap na wabunge saba wa Chadema na wafuasi
wa chama hicho waliokuwa mahakamani hapo.
Wabunge waliochanga fedha hizo ni, Mustafa Akuney
wa Mbulu Lucy Owenya, Grace Kiwelu, Cecilia Pareso, Joyce Mukya, Rose
Kalili na Paulin Gekul wote wa Viti Maalumu.
Utata wa kupoteza sifa ya kugombea
Hukumu hiyo iliibua mjadala mkali kwenye mitandao
ya kijamii juu ya uwezekano wa kumzuia Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa
Upinzani Bungeni kuwania tena ubunge au urais katika Uchaguzi Mkuu wa
Oktoba.
Hata hivyo, Mwanasheria, Alex Mgongolwa akinukuu
Katiba ya Tanzania Ibara ya 67 (1)(c); 67(2) (c na d) alisema hukumu
hiyo haiwezi kumzuia kugombea ubunge kwa sababu hakwenda jela na kosa
lake halihusu kukosa utovu wa uaminifu, kukwepa kodi wala kuvunja Sheria
ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Suala hilo linafanana na lililotokea katika
mchakato wa uteuzi wa wagombea urais mwaka 2005 wakati aliyekuwa mgombea
urais wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila na mgombea mwenza wake,
Saidi Soud Said walipowekewa pingamizi kutokana na kutumikia kifungo
jela, Mtikila akitumikia mwaka mmoja kwa kosa la uchochezi, Said
akitumikia chuo cha mafunzo kwa kosa la biashara ya vitambaa. Hata
hivyo, pingamizi hilo lilitupwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa
ya Uchaguzi (NEC), Jaji Lewis Makame (marehemu) baada ya kusikiliza
utetezi wa Mtikila na Said, kuwa makosa waliyofungwa kwayo hayakuwa ya
kukwepa kodi, kukosa uaminifu wala kukiuka maadili ya viongozi wa umma.
Mashtaka
Mbowe alikuwa anakabiliwa na mashtaka ya kumfanyia
shambulio la kawaida, mwangalizi wa ndani wa Uchaguzi Mkuu Oktoba 31,
2010, Nassir Yamin katika kituo cha kupigia kura kilichokuwa katika
Zahanati ya Lambo.
Yamin alikuwa ni mwangalizi wa kutoka Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata).
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Mpelembwa ambaye
amehamishiwa Bukoba, alisema kitendo kilichofanywa na Mbowe hakikubaliki
na kinapaswa kukemewa.
“Kitendo alichokifanya mshtakiwa akiwa Mwenyekiti
wa Taifa wa Chadema na Mbunge wa Jimbo la Hai ambaye alipaswa kuwa kioo
cha jamii hakikubaliki na lazima kikemewe,” alisema.
“Kwa hiyo hukumu ya Mahakama ni kwamba atalipa faini ya
Sh1,000,000 au akishindwa kulipa atakwenda magereza kwa mwaka mmoja,”
alisema hakimu huyo.
Ushahidi
Akichambua ushahidi uliomtia Mbowe hatiani, Hakimu
huyo alisema Mahakama imeegemea ushahidi wa shahidi wa kwanza, Yamin na
shahidi wa pili John Mushi aliyekuwa msimamizi wa kituo.
Alisema ushahidi huo ulieleza kuwa siku hiyo Mbowe
aliingia katika Kituo cha Zahanati ya Lambo katika Jimbo la Hai na
kuuliza uhalali wa mlalamikaji kuwapo kituoni hapo.
Mashahidi hao waliiambia Mahakama kuwa walimuona
Mbowe akimkunja na kumtoa nje kwa nguvu mwangalizi huyo wa ndani na
baadaye mbunge huyo kuondoka katika kituo hicho.
Alisema ushahidi wa mashahidi hao uliungwa mkono
na shahidi wa nne wa mashtaka, ambaye ni daktari wa Hospitali ya Wilaya
ya Hai, aliyemtibu mlalamikaji na kujaza fomu PF3.
Alisema ushahidi wa daktari huyo unaonyesha kuwa
mlalamikaji alikuwa na michubuko katika shavu lake moja na shingoni
iliyotokana na kupigwa na kitu butu.
Hata hivyo, aliukataa ushahidi wa shahidi wa saba,
Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Shafii aliyekuwa mpelelezi mkuu kuwa Mbowe
alikiri kufanya kosa hilo alipoandika maelezo ya onyo polisi.
Hakimu Mpelembwa alisema japokuwa upande wa
mashtaka uliwasilisha maelezo hayo kama kielelezo lakini baada ya
kuyapitia, hakuna mahali ambako Mbowe alikiri kufanya kosa hilo.
Utetezi wa Mbowe
Hakimu Mpelembwa alisema wakati akijitetea
mahakamani, Mbowe alikanusha kufanya tukio hilo lakini alikiri kufika
katika kituo hicho na kumtaka mwangalizi huyo kumwonyesha kitambulisho
chake.
“Katika utetezi wake, mshtakiwa alikanusha kumpiga
Nasir Yamin wala kumfanyia kitu chochote kibaya, bali alimwamuru atoke
nje kwani hakuwamo kwenye orodha ya waangalizi iliyotolewa na Tume ya
Taifa ya Uchaguzi.”
Hakimu huyo alisema, Mbowe alieleza kuwa hakuwahi kuitwa polisi,
bali alikwenda mwenyewe baada ya kusikia kwenye vyombo vya habari kuwa
amefunguliwa kesi ya aina hiyo.
Sababu za kutiwa hatiani
Hakimu Mpelembwa alifafanua dhana ya kosa la
shambulio kuwa ni kitendo chochote chenye nia ya kudhuru mtu mwingine au
hata kujaribu tu kumdhuru au kumtia hofu.
“Kwa maana nyingine ni kitendo cha kumtia mtu
mwingine hofu na ili kosa hilo litimie ni lazima mshtakiwa awe na nia
isiyo halali kisheria ya kutaka kutenda kosa nililolianisha,” alisema.
Hata hivyo, hakimu huyo alisema shahidi wa kwanza
(Yamin) na wa Pili (msimamizi) waliiambia Mahakama kuwa mshtakiwa
alimkunja na kumvuta nje mlalamikaji atoke nje ya kituo.
“Ushahidi wa Yamin na Mushi ni wa kuona kuwa
mshtakiwa alimkunja na kumtoa nje mlalamikaji. Swali hapa ni je, kumvuta
mtu na kumtoa nje kunapelekea kosa la shambulio?” alihoji.
Hakimu huyo alisema kwa tafsiri ya dhana nzima ya
kosa la shambulio ni dhahiri kitendo alichokifanya mshtakiwa kinaangukia
katika kosa hilo kwa mujibu wa sheria.
“Ushahidi wa shahidi wa kwanza na wa pili wa
upande wa mashtaka unashabihiana na ushahidi wa daktari kwamba kulikuwa
na michubuko. Kwa mantiki hiyo Mahakama inakubali ushahidi huo. Kutokana
na Mahakama kukubali ushahidi wa mashahidi hao watatu, inakutia hatiani
kwa kosa la shambulio kama ulivyoshtakiwa nalo.”
Mwendesha mashtaka, Inspekta Msaidizi wa Polisi,
Feo Simon alisema ingawa hawana kumbukumbu ya makosa ya nyuma ya
mshtakiwa, aliiomba itoe adhabu kali ili iwe fundisho kwake na kwa
jamii.
Wakili wa Mbowe, Issa Rajabu aliyekuwa akisaidiana
na Albert Msando, aliomba Mahakama impe adhabu ndogo mteja wake kwani
hajawahi kutenda kosa lolote la jinai.
Hata hivyo, Hakimu Mpelembwa alisema kwa kutoa
adhabu ya faini ya Sh1 milioni au kifungo cha mwaka mmoja jela
amezingatia ombi la wakili wa Mbowe.
Baada ya hukumu
Hukumu hiyo iliyoanza saa sita mchana hadi saa 7.20 mchana,
wafuasi wa Chadema waliokuwa wamefurika mahakamani hapo walitandika
kanga chini na kuanza kuchangishana faini hiyo kazi ambayo ilisimamiwa
na Kiwelu.
Wakati kazi hiyo ikiendelea, Mbowe aliendelea
kushikiliwa ndani ya chumba cha Mahakama hadi wabunge hao walipokwenda
Benki ya NMB, Tawi la Hai saa 7.40 mchana na kulipa faini hiyo na Mbowe
kuachiwa saa nane mchana.
Mbowe azungumzia hukumu
Akizungumza nje ya chumba cha Mahakama hiyo, Mbowe
aliwatoa hofu wanachama wa Chadema kwamba wasikatishwe tamaa na hukumu
hiyo ambayo alisema alitegemea ingekuwa hivyo.
“Mnanipa pole ya nini? Kuna msiba hapa? Tupeane
hongera. Sikutarajia cha tofauti na hiki kilichofanyika. Hakinivunji
nguvu, bali kinaniimarisha katika mapambano,” alisema.
“Haki katika nchi hii itapiganiwa kwa watu wengine
kuumia na wengine kuokoka. Nimesota mahakamani miaka mitano badala ya
kufanya kazi ya wananchi. Hainivunji moyo,” alisema na kuongeza:
“Hainivunji moyo katika azma yangu ya kuikomboa
nchi hii na ukombozi uko jirani. Mahakama ya nchi hii vimekuwa ni vyombo
vya kutoa dhuluma kwa wananchi japo siyo mahakimu wote. Lakini iko siku
Mahakama zitakuwa ni sehemu ya kutolea haki, kutenda haki na haki
ionekane imetendeka. Mapambano yanaendelea na nawaomba msiwe wanyonge,”
alisisitiza.
“Sitaki kuizungumzia Mahakama katika hatua ya sasa
lakini ndani ya Mahakama kuna watu wanaotenda haki na ndani ya Mahakama
kuna watu wasiotenda haki,” alisema Mbowe.
Alisema kesi hiyo haikustahili kuiendesha kwa
miaka mitano na kwamba kodi za wananchi zinateketea pamoja na muda,
akisema haiwezekani nchi ikaendeshwa katika utaratibu huo.
“Kama mimi mbunge, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni, mtunga sheria wa nchi hii naweza kusoteshwa mahakamani
miaka mitano, mwananchi wa kawaida atafanywaje?” alihoji Mbowe.