Shinyanga. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe amewataka Watanzania kuwa makini katika kuchagua viongozi, badala ya kukurupuka, kwa kuwa baadhi ya waliochukua fomu za kugombea urais wanataka kujaribu tu.
Membe alitoa kauli hiyo jana mkoani Shinyanga alikokwenda kutafuta wadhamini katika nafasi anayoomba ya kugombea urais.
Alisema makada hao wanajua kwamba hawana sifa, lakini wanachukua fomu kwa ajili ya kujipima.
“Lazima uwe na hekima na busara unapotaka kugombea
nafasi ya ngazi ya juu ikiwamo urais, huwezi kwenda kuchukua fomu
wakati hata hujawahi kushika wadhifa wowote ndani ya chama. Unataka
kwenda kujifunza ukiwa madarakani? Watu kama hao kuweni nao makini,”
alisema Membe.
Alisema mtu anayetaka kugombea urais anapaswa
kuzingatia vigezo 13 vilivyowekwa na chama, lakini kuna watu wameshindwa
kujipima kabla ya kuchukua fomu.
“Walitakiwa kujitathmini wenyewe kwani hata haya
makofi mnayonipigia mimi na hao wengine mnawapigia nawaomba mchuje na
kuwa makini,” alisema Membe.
Katika hatua nyingine, Membe alisema hakuna chama
tawala chochote duniani kitakachoangushwa na wapinzani, bali chama
chenyewe kinajimaliza na wanachama wake kutokana na kuwa na mamluki
ndani yake.
Lowassa atikisa Mbeya
Wakati huohuo, Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa
amesema akichaguliwa kuwa rais mbali na kuendesha nchi kwa mchakamchaka,
atahakikisha anawatetea wafanyabiashara ndogondogo ‘Machinga’ ili
wafanye biashara zao bila kuhangaika na kufukuzwa barabarani.
Alisema ataimarisha biashara za mipakani kwa
kuhakikisha wananchi wanawezeshwa kiuchumi ili kuona kila mmoja anakuwa
na uchumi ulioimarika kwa kupewa mikopo ya kutosha kwa ajili ya
kuendesha biashara zao.
“Ikizingatiwa Mkoa wa Mbeya umepakana na nchi za
Zambia na Malawi, lakini wananchi hamnufaiki chochote na mipaka hiyo.
Nikiingia madakarani nitahakikisha naweka mipango ya kuwawezesha
kiuchumi ili kuinua vipato vyenu kupitia biashara za mipakani,” alisema
Lowassa.
Awali, Katibu wa CCM Mkoa wa Mbeya, Adam Kundya
alisema viongozi wengi huingia na kutoka miyoyoni mwa watu
wanaowaongoza, lakini kiongozi wa kweli huacha nyayo zake kwenye mioyo
ya wananchi.
Kabla ya Lowassa kutua katika viwanja hivyo, ilitangulia
helikopta iliyokuwa imembeba Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM wa Wilaya
ya Busega Mkoa wa Simiyu, Dk Raphael Chegeni ambayo alizunguka hewani
kwa takribani dakika saba akiwa usawa wa Ofisi za CCM kabla ya kutua nje
ya ofisi hizo.
Makamba adai kujenga viwanda Tabora
Kwa upande mwingine, Naibu Waziri wa Mawasiliano,
Sayansi na Teknolojia, January Makamba amesema pamoja na Mkoa wa Tabora
kuchangia pato kubwa la Taifa hasa kupitia zao la tumbaku, haufaidiki na
uchumi.
Akizungumza na wanachama waliomdhamini mjini
Tabora alisema wananchi wanatumia nguvu kubwa kuzalisha, huku kipato
chao kikiwa hakilingani na jasho wanalolitoa.
Alisema mkoa huo hauna viwanda kabisa licha ya kulima mazao ya tumbaku na pamba.
“Hapa mnalima pamba na tumbaku, lakini hakuna
viwanda vya mazao hayo na hivyo ajira kuzipeleka nje ya mkoa na kuwaacha
vijana wenu hawana ajira,” alisema.
Makamba alisema kukijengwa viwanda vya mazao ya
tumbaku na pamba, vijana watakuwa wamepata ajira ambayo sasa hawana
kutokana na viwanda kujengwa nje ya mkoa.
Stella Ibengwe na Suzy Butondo, (Shinyanga), Godfrey Kahango, Justa Musa na Brandy Nelson (Mbeya) na Robert Kakwesi (Tabora).
credit mwananchi
credit mwananchi