Tangu Chama cha Mapinduzi (CCM) kilipofungua milango kwa makada
wake wanaojiona wana sifa ya kuwania urais wakachukue fomu, wananchi
wameshuhudia msururu mrefu wa makada hao wakitangaza nia kwenye mikutano
ya hadhara na pili wakichukua fomu za udhamini.
Waliochukua fomu za udhamini hadi sasa wamefikia
38 na wanapita mikoani kutekeleza sharti la kudhaminiwa na wanachama 450
kutoka katika mikoa 15.
Upande mmoja ni jambo linalofurahisha kuona makada
hao wakitumia haki yao ya kikatiba na kidemokrasia kushiriki katika
mbio za kuwania urais. Pia kinadharia, ni jambo lenye afya kwamba kamati
za uteuzi zitapata wigo mpana wa kuwachuja hadi kumpata anayefaa, kwa
kuzingatia sifa zinazohitajika, kwa nafasi hiyo nyeti.
Upande wa pili, utitiri wa wagombea hao, ni
ushahidi kwamba chama hakina tena mfumo wa kuandaa viongozi wake ila
kinasubiri wazuke tu na kuifanyia sitihizai nafasi hiyo ya juu ya
uongozi nchini.
CCM inajua kuwa nafasi ya urais ni nyeti lakini
miongoni mwa waliotozwa Sh1 milioni na kupewa fomu ni wanaokosa sifa
kabisa kama kada ambaye elimu yake ni ya msingi tu wakati kiwango cha
elimu kinachohitajika ni shahada, na mwingine mwenye umri ulio chini ya
miaka 40 inayotakiwa kikatiba.
Hata kama, makada hao wanatimiza haki yao
kidemokrasia, CCM wanapokeaje fedha za fomu kutoka kwa makada ambao
kimsingi hawana sifa ya urais? Hapa CCM imejali zaidi fedha na siyo
demokrasia. Ikiwa katika jambo lililowazi kiasi hiki CCM imevurunda, si
itavurugwa na utitiri wa wagombea hao wakati wa kumpata kada anayefaa
kuwania urais?
Makada wengine waliopewa fomu ili waingie kwenye
mchujo ni naibu mawaziri na mawaziri katika Serikali ya Awamu ya Nne;
baadhi yao wameteuliwa hivi karibuni na hawajafanya kitu cha maana na
wengine wamekuwa mizigo. Mbali ya hao, wapo waliotajwa wazi katika
kashfa kubwa za ufisadi.
Hao wote wanapita mikoani kuomba udhamini
wakiikosoa Serikali ilivyoshindwa kupambana na rushwa na kukusanya kodi
na ilivyoshindwa kuboresha huduma za jamii kama elimu, afya na kuwapa
ajira vijana. Baadhi yao wanajipigia debe kuwa hakuna mwingine anayefaa
isipokuwa wao.
Vilevile, baadhi ya wagombea wanatumia wapambe
kuhonga wanachama ili wafurike kwa wingi kudanganya umma kuwa
wanadhaminiwa na wengi kwa madai wanapendwa; baadhi ya wagombea
wamefanyiwa fujo hadi mmoja kupigwa na vijana wa tawi la ulinzi la chama
hicho maarufu kama Green Guards.
Yanapofumbiwa macho, mambo haya ambayo
yanakidhalilisha peupe chama hicho kikongwe tena na makada wake, ni
ishara mbaya kuelekea kumpata mgombea atakayekuwa na uwezo wa
kuunganisha kambi zinazopingana ndani ya chama, kujitenga na matajiri na
kuongoza nchi kwa utulivu.
Tunapenda kuwakumbusha viongozi wa CCM kwamba
wakati Mwalimu Julius Nyerere anastaafu alisema; “Bila CCM imara nchi
itayumba.” Na kwa kuwasaidia wakati wa uteuzi wa mgombea urais mwaka
1995 alipendekeza wote waliotajwa katika vyombo vya habari kuwa
wanahusika na kashfa za kisiasa au za rushwa waondolewe ili wabaki walio
safi tu, na pia mgombea wa CCM asiwe mwenye kukumbatia matajiri.
Leo ni tofauti, tunachokiona ndani ya CCM kinatia
shaka kwani licha ya utitiri huo mrefu wa wagombea urais tunadhani chama
hicho kilipaswa kujua sifa za awali za wagombea wake kabla ya kuchukua
fedha.
Mathalani jambo la umri na elimu ni sifa ambazo zipo wazi, je kulikuwa na sababu gani ya kuchukua fedha kutoka kwa wagombea ambao tayari wanaonekana kukosa hata sifa za msingi kabisa
Credit: Mwananchi
Mathalani jambo la umri na elimu ni sifa ambazo zipo wazi, je kulikuwa na sababu gani ya kuchukua fedha kutoka kwa wagombea ambao tayari wanaonekana kukosa hata sifa za msingi kabisa
Credit: Mwananchi