https://play.google.com/store/apps/details?id=com.blog.ya.watanzania


.

.

.
  • Latest News

    .

    MWAKYEMBE AKANA KUTUMIA RICHMOND KUMCHAFUA LOWASSA...... UMOJA WA ULAYA NAO WAKANA KUHUSIKA KUMCHAFUA..


    WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Harrison Mwakyembe, ameibuka na kusema hajawahi kumshambulia kwenye mitandao Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuhusu sakata la Richmond.
    Kauli hiyo ya Dk. Mwakyembe imekuja siku chache baada ya kusambazwa kwa waraka unaodaiwa kuandikwa naye, ukimuhusisha na tuhuma za kumshambulia Lowassa, jambo ambalo amelifananisha kuwa ni sawa na siasa za kitoto.Akizungumza jana katika kipindi cha Power Breakfast kinachorushwa na kituo cha redio Clouds FM, alisema kutokana na kusambazwa kwa waraka ambao umeandikwa nyadhifa zake za ubunge na uwaziri, hivi sasa ameshaanza kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watu waliokuwa wakiusambaza.Waziri Mwakyembe ambaye kitaaluma ni mwanasheria na mwanahabari, alisema anapata shaka hata na baadhi ya vyombo vya habari pamoja na mitandao hiyo na kudai kuwa anamshambulia Lowassa.

    “Ninashangazwa sana na hii mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari (magazeti), vimekuwa vikiandika vitu vibaya ikiwa ni pamoja na kumshambulia Lowassa wakati hata siku moja sijazungumza nao.
    “Kitendo cha baadhi ya watu wa aina hii kuwaandika vibaya wanasiasa katika mitandao ya kijamii kwa kutumia majina ya watu wengine ni ishara ya woga wa kisiasa na kushindwa kujiamini katika misimamo yao.
    “…Kinachonikera kupindukia ni kuwa taarifa hizo sijawai kuziandika ila kuna mtu ama kundi maalumu la watu limeziandika na kuweka jina langu na nafasi zangu za uongozi kama mbunge na waziri, huu si uungwana na wala si siasa kwa kuchezea majina ya watu. Kama siasa zimefika huku basi ni za hatari,” alisema.
    Dk. Mwakyembe ambaye pia ni Mbunge wa Kyela mkoani Mbeya, alisema katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu, watu wanapaswa kuacha woga na kutojiamini.

    “Kitendo cha kutumia majina ya watu na kuelezea hisia zao ni kukosa ujasiri na hata yanayosambazwa kwenye mitandao hayaendani na hadhi yangu kiongozi, sina tabia ya woga na uongo,” alisema.

    Alisema baada ya kupata taarifa zilizopo mitandaoni alilazimika kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi Kitengo cha Makosa ya Mtandaoni pamoja na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ili kulalalimikia mchezo huo mchafu.

    Dk. Mwakyembe alisema vyombo hivyo vimeshaanza uchunguzi mkali ili kuwabaini watu walioandika na kutuma taarifa hizo.
    “Hizo porojo zilianza tu polepole, zilienda mitandao ya kijamii na magazeti kuwa nimesema Lowassa hana sifa ya kuwa rais, wengine walisema niliwaambia nitapambana kufa na kupona Lowassa asiingie Ikulu wakati sijaongea nao na sijawahi kusema, huu ni mchezo wa kitoto uliopitiliza, lakini una madhara makubwa,” alisema Dk. Mwakyembe.
    Alisema kutokana na hali hiyo, amedhamiria na kuhakikisha kesi ya kwanza ya matumizi mabaya ya mitandao inaanzia kwake kwa kuwa hana utamaduni wa woga, na watu wanapaswa kuwa wazi endapo wanakuwa na vitu na si kutumia majina ya watu.

    Dk. Mwakyembe alisema anashangazwa na watu kutumia jina lake kumchafua kwa kuwa hana tatizo na mtu yeyote na kama chanzo ni suala la Richmond, ilikuwa ni kazi aliyopewa na Bunge.

    Alisisitiza kuwa alifanya kazi hiyo vizuri kwa kumuweka Mungu mbele, lakini si kuongea uongo jambo ambalo si utamaduni wake.
    “Wananchi wanapaswa kutambua kuwa nchi inaendeshwa kisheria na ninaamini wahusika wote waliofanya tukio hilo watachukuliwa hatua za kisheria,” alisema.
    Umoja wa Ulaya Nao Wakanusha;
    Jana Umoja wa Ulaya (EU) ulikanusha vikali kwamba balozi wake nchini alifanya mkutano na waandishi wa habari na kumtahadharisha Rais Jakaya Kikwete kwamba nchi yake inaweza kuingia matatani na EU kama Lowassa atateuliwa kuwa mgombea urais kupitia CCM.

    Ofisa Habari wa EU, Susanne Mbise jana alikanusha taarifa izo na kusema kuwa hata wao wamesikia taarifa hizo, lakini ukweli wa jambo hilo upo kwenye taarifa waliyoweka kwenye mtandao wa Face Book ya Umoja huo.

    Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyosainiwa na Ofisa anayeshughulikia Siasa na Habari, Luana Reale wa kitengo cha habari, Balozi huyo hajafanya mkutano wowote na mwandishi yeyote na kwa maana hiyo hajatoa taarifa yoyote kwa vyombo vya habari.

    Reale alisema kuwa tangu Juni mosi mwaka huu Balozi huyo hayuko nchini kwani alisafiri kwenda makao makuu ya Umoja huo na hajarejea nchini.

    Alisema kuwa EU ina uhusiano mzuri wa muda mrefu na Tanzania ambao umejengwa juu ya misingi ya kuheshimiana na kuaminiana.

    EU inatoa taarifa hizo baada ya watu wasiojulikana kusambaza taarifa za uzushi na uongo kwenye mitando ya kijamii wakidai kuwa Rais Kikwete ameonywa kwamba Lowassa akipitishwa kuwania urais uhusiano wa Tanzania na EU utaingia shakani na kwamba hawataisaidia katika miradi ya maendeleo.

    Wazushi hao walidai kuwa Lowassa ni mtuhumiwa namba moja wa rushwa nchini na kutaja kuwa anahusika katika kadhia ya Richmond na NIC.
    https://play.google.com/store/apps/details?id=com.blog.ya.watanzania

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: MWAKYEMBE AKANA KUTUMIA RICHMOND KUMCHAFUA LOWASSA...... UMOJA WA ULAYA NAO WAKANA KUHUSIKA KUMCHAFUA.. Rating: 5 Reviewed By: Unknown
    Scroll to Top