Wakati takribani makada 32 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wakiwa wameshatangaza nia na kuchukua fomu za kuwania kiti cha urais kwenye uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 25, wametangaza pia vipaumbele vya aina ya serikali watakayoiunda kama watapata fursa.
Wengi wameweka vipaumbele vyao ni elimu wakisema itakuwa bure kuanzia chekechea hadi kidato cha nne, wengine wamesema ajira kwanza, wengine wanazungumza kuendeleza mazuri ya serikali ya awamu ya nne inayomaliza muda wake ikiwamo kukamilisha mchakato wa Katiba inayopendekezwa huku wengine wakijinadi kwamba watakomesha ufisadi na rushwa.
Pamoja na kwamba ajenda zote ni nzuri, Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimezikosoa kikieleza kuwa kwa ujumla ahadi zinazotolewa leo na makada hao wa CCM zilikuwa kwenye Ilani ya uchaguzi ya Chadema mwaka 2010.
Salum Mwalimu ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), anasema ahadi za afya, maji, elimu, barabara, nishati na miundombinu ni miongoni mwa ahadi zilizotolewa na baadhi ya wagombea wanaotafuta urais lakini wameshindwa kuzitekeleza wakiwa kwenye nyadhifa walizonazo sasa.
Akiwa ziarani mkoani Iringa Mwalimu (pichani), kuhamasisha wananchi kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura, amekosoa ahadi zinazotolewa sasa.
Anasema watia nia hao wamekuwa wakipinga kwa makusudi mambo mengi ya msingi wakiwa ndani ya bunge na hata kuteteana wao wenyewe kwa wenyewe, lakini inashangaza sasa wameteka hoja zilizotolewa na Chadema miaka mitano iliyopita.
“Ukiangalia mwaka 2010, Dk. Wilbrod Slaa alisema Chadema kama kitapewa ridhaa na wananchi ya kuongoza nchi lazima wataweka elimu bure kwa Watanzania kuanzia awali hadi vyuo vikuu lakini leo hii hawa CCM wameichukua ile ajenda na kuifanya ya kwao lakini wa kipindi hicho cha miaka mitano wameshindwa kutoa elimu bure,” anasema.
Mwalimu anaongeza kuwa: “Tulifikiri baada ya sisi upinzani kutopewa ridhaa sasa wao wataweza kuongoza na kutatua kero zote pamoja na ahadi zote walizoziahidi wakati wanatia nia ya kuwania urais.”
Mwalimu anasema kuwa pamoja na kushindwa kutoa elimu hiyo bure kwa Watanzania walikuja na ajenda nyingine ambayo ilikuwa ya Chadema ambayo pia Dk. Slaa alisema Chadema ikiingia madarakani wangeanzisha mchakato wa katiba mpya ndani ya siku 100, hoja ambayo ilitekwa na CCM lakini ilishindwa kuitekeleza.
“Nayo CCM waliiba tukafiriki labda kwa kuwa wameichukua wataweza kuanzisha mchakato huo, Jaji Joseph Warioba akapita mikoani kwa ajili ya kuchukua maoni ya Watanzania kuhusu kupata katiba mpya lakini wao CCM wameipinga na kusema maoni yale sio ya wananchi, kwa hiyo mchakato umekwama,” anasema.
“Wamemdhihaki Jaji Warioba kwa kusema yale siyo maoni ya wananchi sasa hawa CCM wataweza kipi kama wameweza kupinga hata maoni hayo?” Anahoji.
“Ninachokisema ni kwamba hawa CCM wamekuwa wakipinga mambo mengi sana ya upinzani hasa ya maendeleo wakiwa mule bungeni wanateteana halafu wanakuja tena kuwadhihaki wananchi kuomba ridhaa ya kuongoza tena kwa kipindi cha miaka mitano mingine.” anasema.
Mwalimu anasema kuwa watia nia hao bado hawajakata tamaa na wanaendelea kuja na hoja zilezile ambazo walikuja nazo kipindi kilichopita na kusema kwamba watapambana na ufisadi, kuleta uchumi imara kwa Watanzania, kujenga miundombinu bora, huduma za maji, utawala bora, lakini hizi zote zilikuwapo wameshindwa kutekeleza sasa kipindi hiki wataweza kutekeleza kama siyo miujiza?” Anasema Mwalimu.
Anasema hata hoja ya ufisadi ni ajenda ya muda mrefu ya Chadema ambacho kiliwahi kuwataja hadharani majina ya mafisadi kwenye ‘list of shame.’
Mwalimu anasema kuwa kila kikao cha Bunge wanatenga bajeti kwa ajili ya kuwaletea maendeleo wananchi kwenye majimbo yao lakini fedha zile hazifiki zote na wanawalaghai wananchi kwamba CCM ndicho chama pekee ambacho kitawaondoa kwenye umasikini.
Anakumbusha kuwa hivi karibuni kumekuwapo na tuhuma za ulaji wa fedha nyingi kwenye kashfa ya wizi wa mabilioni ya Shilingi katika akaunti ya Escrow, fedha hizi zimeliwa na watu wachache wakiwamo wanachama wa CCM.
Anasema ndani ya CCM hakuna mtu msafi kwa madai kuwa wote wananuka rushwa hivyo hakuna atakayeweza kuunda serikali itakayokomesha rushwa na kuwaletea wananchi maendeleo.
“Ila Chadema tunaamini kwamba mwanzo wa kufa kwa CCM ni mwaka huu tupeni nchi tuwaekee mazingira safi ya kupata huduma nzuri kwa wananchi angalau na wao wawe wapinzani ili waweze kujifunza kwetu,” anasema Mwalimu.
Anasema saratani ya nchi hii ni ufisadi kwa sababu wananchi wameendelea kuwachagua makada wa CCM ambao wamekuwa wakiiba.
Akizungumza na wananchi wa Mufindi, anasema Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi ni ya pili Tanzania kwa mapato ikikusanya zaidi ya Sh. bilioni 14 lakini wananchi wa wilaya hiyo ni masikini kupindukia.
Anasema umasikini huo unasababishwa na wawakilishi wa wananchi katika Halmashauri hiyo kutokana na CCM hivyo wanajipangia wenyewe matumizi ya fedha bila kujali maslahi mapana ya wananchi.
“Nawapeni mfano angalieni halmashauri ambazo zipo chini ya Chadema halafu linganisheni na halmashauri ya wilaya ya Mufindi…Halmashauri ya manispaa ya Moshi inakusanya Sh. bilioni sita kuna huduma zote za kijamii na wanalipia huduma zote za ada watoto masikini lakini nawashangaa ninyi watu wa Mufindi mna kila rasilimali lakini mmeshindwa kuzitumia kwa sababu ya kuwapa CCM madaraka,” anasema.
Anawataka wananchi hao kuvunja ndoa na CCM na waichague Chadema ili waweze kuonja maendeleo kwa kunufaika na rasilimali walizonazo.
George Tarimo ni mwandishi wa gazeti la NIPASHE mkoani Iringa anapatikana kupitia simu namba 0759 678292/0719057666 au barua pepe georgetarimo5040759@gmail.com
CHANZO: NIPASHE