WAKATI Kocha Mkuu wa Yanga akilia na kipa Deo Munishi ‘Dida’ akidai ameiponza Taifa Stars kukung’utwa mabao 3-0, Msaidizi wake na kocha wa zamani wa Stars, Boniface Mkwasa ametoa ya moyoni na kudai ni bora timu hiyo ifumuliwe yote kisha isukwe upya ili kuliepushia taifa aibu.
Makocha hao walitoa maoni yao kuhusu kipigo cha Stars ilichopewa juzi Jumapili usiku ugenini Misri katika pambano la mkondo wa kwanza la Kundi G la michuano ya kuwania Fainali za Afcon-2017.
Pluijm alisema kwa mtazamo wake, Dida ndiye aliyeiponza Stars kwa kufanya uzembe ambao uliigharimu timu kwa kutokuwa na mawasiliano mazuri na mabeki wake.
“Kiufundi, Dida aliwaangusha wenzake kwa uzembe aliofanya, kwa kweli inasikitisha kwa kilichotokea Misri,” alisema Pluijm.
Naye Mkwasa kwa upande wake alisema haoni sababu ya Stars kubeba gharama kubwa ya kambi yake huku ikiendelea kuwa na matokeo mabaya ambayo yanaweza hata kuwavunja nguvu wadhamini.
“Timu inapaswa kufanyiwa ukarabati wa hali ya juu ikiwezekana ivunjwe na kutengenezwa upya kabisa ili iweze kufanya vizuri kama wanataka kupata matokeo mazuri,” alisema
Mkwasa alisema Watanzania wameanza kuichoka timu yao na kuikatia tamaa kwa kuona kodi zao zinatumika visivyo katika kuihudumia.
“Stars imekuwa ikitumia gharama kubwa katika kambi kama hiyo iliyowekwa kwa wiki moja nje ya nchi kabla ya mechi na bado imefanya vibaya, hata kama ni kweli soka ni matokeo, lakini inabidi hili liangaliwe kwa mapana timu inatutia aibu sana,” alisema Mkwasa.
Kauli ya Mkwasa imekuwa saa chache baada ya Stars kuchezea kichapo cha mabao 3-0 mbele ya Misri katika pambano lao la kwanza la Kundi G kuwania kucheza fainali za Afcon za mwaka 2017