Mkaguzi wa Vyakula na Dawa toka Mamlaka ya TFDA, John Mosha amesema watu wanaotumia dawa mbalimbali kuongeza na kupunguza ukubwa wa maumbile yao wako katika hatari ya kupata saratani ya ngozi kutokana na dawa wanazotumia kuaminika kuwa zina viambata vya sumu.
Baadhi ya dawa zilizopigwa marufuku ni pamoja na hip up cream, breast cream, lift up na fem tight.
Mosha amesema dawa hizo zina viambata sumu ambazo vinaingia kwenye ngozi na kusababisha saratani ya ngozi.
HABARI LEO
Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Nape Nnauye amesema Mwenyekiti wa CHADEMA,Freeman Mbowe anatakiwa ajiuzulu nafasi yake kutokana na hukumu aliyopewa na Mahakama ya Moshi juzi kumuaibisha.
Mbowe alikutwa ana hatia Mahakamani hapo kwa kesi ya kumpiga Msimamizi wa Uchaguzi mwaka 2010 ambapo Nape amesema Kiongozi huyo hana sifa ya kuwa kiongozi kwa kuwa hana kifua kigumu cha kuzuia hasira.
“Mtu mzima ukiwa umejifunga taulo na mtoto akaja kuichukua hutakiwi kumkimbiza mtoto, badala yake unachutama.. ukimbkimbiza na wewe utaonekana akili yako kama mtoto”—Nape Nnauye.
Nape amesema CHADEMA imejijenga kwa misingi ya ubabe na akawataka vijana vijana kuwa macho na kujihadhari.
MTANZANIA
Waziri Dk. Harrison Mwakyembe amekuwa kada wa 37 kuchukua fomu ya kugombea Urais CCM katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2015.
Dk. Mwakyembe amesononeshwa na mikakati miovu dhidi ya Lowassa wakati alipokuwa akijibu swali kama ana kinyongo na Lowassa.
“Naapa mbele ya MUNGU sina chuki na mtu yoyote kwa kuwa lile suala (RICHMOND) halikuwa langu bali lilikuwa la Bunge… Kumtaja MUNGU ni vibaya sana, nikisema uongo atanilaani”—Dk. Mwakyembe.
Waziri Mwakyembe amesema huwa anasononeshwa na baadhi ya watu wanaosambaza maneno kuwa bado ana chuki na Lowassa na alishtushwa kupigiwa simu kwamba anatumia mitandao ya kijamii kumchafua.
“Niliripoti Polisi na TCRA na nilipata Ushirikiano uliofanikisha baadhi ya wahusika kukamatwa.. kibaya zaidi mmoja ya waliokamatwa ni mpambe wa Wanaogombea Urais”—Dk. Mwakyembe.
MTANZANIA
Moses Mongo ambaye ni Mratibu wa Kanda ya Ziwa kutoka Taasisi ya Umoja wa Mataifa (UNA-TANZANIA) amesema wanafunzi wa Vyuo Vikuu wanaongoza kwa utoaji wa mimba kwa njia za kienyeji kwa kutumia mwarobaini na bluu ya kuweka kwenye nguo nyeupe.
Mongo alisema katika utafiti walioufanya mwaka 2014 katika Vyuo Vikuu vinne Kanda ya Ziwa wamebaini wanafunzi kutoa mimba kienyeji.
“Utafiti tuliofanya 2014 kwa kuzungumza na wanafunzi kila Chuo au Shule tumebaini wapo wanafunzi waliotoa mimba na wapo waliofariki kwa kutoa mimba lakini kwa kificho”—Moses Mongo.
Mongo alisema katika mazungumzo na wanafunzi hao walieleza kuwa suala la utoaji wa mimba ni la kawaida na matumizi ya kondomu huwa ni pale wanapoanza uhusiano kabla ya kuzoeana.
JAMBO LEO
Spika wa Bunge, Anne Makinda amewaagiza Mawaziri wote kuwepo Bungeni siku ya Jumatatu ili kujibu hoja za Mawaziri walizozitoa wakati wa kuchangia Bajeti.
Spika Makinda amewataka Wabunge wote nao kuwepo Bungeni ambapo vufngu vitapitishwa kwa utarafibu wa Wabunge kuitwa majina.
Tangazo hilo limetolewa na Spika wakati kukiwa na hali ya utoro uliokithiri ndani ya Bunge hasa wakati wa kujadili Bajeti ya mwaka 2015/16.
Katika Mijadala hiyo Wabunge walionekana wachache huku Mawaziri nao wakiendelea na mbio za kusaka wadhamini Mikoani kwa ajili ya kupata ridhaa ya kupeperusha bendera ya CCM kwenye kugombea Urais.
JAMBO LEO
Mwanamke mmoja anayedaiwa kuwa Mtanzania amekamatwa na dawa za kulevya zenye uzito wa kilo 75 katika Uwanja wa Ndege India ambapo mwanamke huyo alikamatwa akiwa na hati ya kusafiria ya Tanzania.
Mwanamke huyo alikamatwa katika Uwanja huo ambapo aligundulika kubeba mzigo huo baada ya mbwa kunusa mizigo yake akiwa eneo la upekuzi.
Milind Lanjewar ambaye ni Ofisa wa Uwanja huo amesema hicho ni kiwango kikubwa zaidi cha dawa za kulevya kukamatwa katika kipindi cha hivi karibuni.
Lanjewar amesema mwanamke huyo alikuwa na mzigo wa unga ambao ni dawa za kulevya aina ya Methaqualone au Mandrax na Cocaine.
MWANANCHI
Harakati za makada wa CCM wanaowania urais kusaka wadhamini mkoani zinaendelea kukumbwa na vituko baada ya wanamgambo wa chama hicho, maarufu kama Green Guards, kumshushia kipigo Dk. Mussa Muzamill Kalokola aliyeingilia mkutano ulioandaliwa kwa ajili ya mgombea mwingine.
Huu ni mwendelezo wa matukio kadhaa ambayo yamekuwa yakitokea kwenye mchakato huo, ikiwemo ya wanachama kutaka kuchana fomu za mgombea baada ya kunyimwa ‘posho’ na kada mwingine kukosa wadhamini na kulazimika kuomba chakula cha mchana kutoka kwa mkuu wa Wilaya.
Dk Kalokola ambaye pia anadaiwa kushawishi wanachama wasimdhamini mgombea mwingine wa urais, Bernard Membe alidaiwa kuvamia mkutano ulioandaliwa kwa ajili yaEdward Lowassa na kutaka kulazimisha apewe kipaza sauti kwa ajili ya kuomba wanachama wamdhamini, kitu ambacho viongozi wa CCM wa wilaya hawakukubaliana nacho na alipoendelea kung’ang’ania ndipo Green Guards walipoamriwa wamuondoe eneo hilo.
Picha za video za tukio hilo ambazo zimesambazwa mitandaoni zinawaonyesha vijana hao wa Green Guards wakimsomba mzobemzobe mgombea huyo, kumuangusha kwa kumpiga ngwala na mkoba wake wenye stika ya fomu za mgombea Urais, ukionekana kuzagaa chini.
Alipoulizwa na Mwananchi kuhusu mkasa huo, Dk. Kalokola alikiri kupigwa katika tukio hilo lilitokea mchana Jumatano ya Juni 17, 2015 alipofika kwenye ofisi za CCM za Wilaya ya Tanga Mjini, siku ambayo mgombea huyo anadai alipangiwa na Katibu wa Wilaya.
Dk. Kalokola alisema baada ya kukabidhiwa fomu za kuomba kuteuliwa na CCM Julai 15 mwaka huu mkoni Dodoma, alikwenda mkoani Tanga ili kupata wadhamini.
MWANANCHI
Uwepo wa Machimbo mengi ya Wachimbaji wadogo wa dhahabu eneo la Bulyanhulu Shinyanga imedaiwa kuwa moja ya sababu ambayo iachangia watoto wengi kupata mimba za utotoni na wengine kukatisha masomo.
Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya ya Kahama, Zabron Donge amesema kutokana na hali hiyo Serikali imeweka mpango wa kushirikiana na wadau wengine ili kuhakikisha tatizo hilo linaisha na watoto wanamaliza Shule.
Mgodi wa Bulyanhulu nao umejipanga ili kutafuta suluhu ikiwemo kuwalipia ada wanafunzi wasio na uwezo.