https://play.google.com/store/apps/details?id=com.blog.ya.watanzania


.

.

.
  • Latest News

    .

    Upangaji matokeo unavyolitafuna soka la Tanzania

    iiii
    Na Mwandishi wetu
    Katika sehemu ya kwanza jana, tuliona jinsi utashi wa kuadhibu vikali tatizo la rushwa na upangaji wa matokeo kwenye mpira wa miguu nchini unavyokosekana kwa miaka mingi ndani ya Shirikisho la Soka (TFF) licha ya kuwapo kwa sheria madhubuti dhidi ya mchezo huo mchafu.
     
    Aidha, tuliona matamko makali ya Kamati ya Bunge inayohusika na michezo na serikali katika kutaka ukomeshaji wa rushwa kwenye soka la Tanzania kutoka kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, Said Mtanda na Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia.
     
    Endelea kusoma sehemu ya pili ya mfululizo wa habari hii.
     
    REFA JONESIA AKATAA HONGO MTIBWA
    Refa wa kati Jonesia Rukyaa (25), ni miongoni mwa waamuzi ambao walipata wakati mgumu msimu uliopita wa Ligi Kuu Tanzania Bara kutokana na kuombwa kuibeba timu ya Mtibwa Sugar.
     
    NIPASHE ilibaini kuwa mmoja wa watendaji wa Mtibwa Sugar FC (jina tunalihifadhi kwa sasa) alimpigia simu refa huyo anayeishi Kagera kwa nia ya kumpa hongo ili aibebe Mtibwa katika mechi yao ya mzunguko wa kwanza dhidi ya Ruvu Shoooting kwenye Uwanja wa Mabatini, Pwani Januari 25.
     
    Jonesia ambaye Desemba mwaka aliweka historia kwa kuwa mwamuzi wa kwanza wa kike kuchezesha mchezo wa watani Simba na Yanga, alikataa fungu kutoka kwa mtendaji huyo.
     
    Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa baada ya mechi kumalizika, alitumiwa ujumbe wa vitisho na mtendaji huyo kutokana na matokeo mabaya ambayo Mtibwa iliyapata. Kikosi cha ‘Wakatamiwa wa Manungu’ kililala 2-1 dhidi ya Ruvu Shooting siku hiyo.
     
    Mechi hiyo ilikuwa ya kwanza kwa Mtibwa Sugar kupata matokeo mabaya baada ya kucheza mechi tisa za Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita bila kupoteza hata moja. Waliuanza msimu kwa kushinda 2-0 dhidi ya Yanga, 3-1 dhidi ya Ndanda, 1-0 dhidi ya Mgambo, 0-0 dhidi ya Police Moro, wakailaza 2-0 Mbeya City kisha wakapata sare nne mfululizo za 1-1 dhidi ya Simba, Kagera, Stand United na JKT Ruvu.  
     
    “Naona umefanikisha ulichokuwa umekipanga. Sasa utanijua mimi ni nani. Nitakuonyesha… (akatukana matusi). Wewe ni mtu mdogo sana katika soka la Tanzania,” ilisomeka sehemu ya ujumbe uliotumwa na mtendaji huyo kwenye simu ya mkononi ya Jonesia.
     
    Akiwa Kagera mwishoni mwa wiki iliyopita, Jonesia ambaye mwaka huu aliweka rekodi nyingine ya kuwa mwamuzi wa kati wa kike mwenye beji ya Fifa aliye na umri mdogo zaidi kwenye orodha ya waamuzi wa kati wanaotoka Afrika, aliliambia gazeti hili kuwa kesi yake dhidi ya mtendaji huyo wa Mtibwa inashughulikiwa na TFF.
     
    “Kwa sasa suala hilo haliko mikononi mwangu. Viongozi wa TFF ndiyo wanalishughulikia. Baada ya kuwa ninapigiwa simu na kutumiwa ‘message’ (ujumbe) wa vitisho, niliwasiliana na viongozi wa Kamati ya Waamuzi ya TFF na kuwakabidhi kila kitu kuhusu suala hilo.
     
    “Baada ya kuwapa zile ‘message’ na namba za simu za huyo mtu, uongozi wa kamati uliniambia nikae kimya. Siwezi kuliongelea zaidi sual hilo kwa sababu tayari linafanyiwa uchunguzi na vyombo vya TFF kabla ya kukabidhiwa kwa vyombo vya dola,” alisema Jonesia.
     
    Alipoulizwa na NIPASHE kuhusu undani wa suala hilo, Mratibu wa Mtibwa Sugar, Jamal Bayser, alijibu kwa kifupi kwa kusema: “Sina taarifa hizo.”
     
    Gazeti hili pia lilizungumza na Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi ya TFF, Saloum Chama, ambaye alisema suala hilo litafikishwa kwenye vyombo vya dola mwezi huu.
     
    “Ni kweli tulipokea malalamiko ya refa Jonesia kutumiwa ujumbe wa vitisho. Suala hilo tunalifanyia kazi. Mimi nitakuwa Dar es Salaam Juni 18 mwaka huu, tunakuja huko kuchunguza vielelezo vya huyo mtu anayehusika na shtuma hizo,” alisema Chama na kueleza zaidi: 
     
    “Hili linahusisha vyombo vya usalama maana linahitaji kuingia mitandaoni kupekua taarifa za mtu. Ukilifanya bila kuvihusisha vyombo vya usalama, wanaweza kukushtaki na ukapata matatizo ambayo ni makubwa.”
     
    MAREFA WAISHUSHA DARAJA RUVU SHOOTING
    Katika hatua nyingine, Chama aliweka wazi kuwa marefa wawili waliosimamia mechi ya mwisho ya Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Stand United na Ruvu Shooting mjini Shinyanga Mei 9 mwaka huu wamefungiwa miezi 12 kutokana na kuchezesha kwa kuwabeba wenyeji.
     
    “Waamuzi wanatudhalilisha. Ukiangalia mechi ya Stand na Ruvu Shooting, haina utata kwamba marefa waliingia na matokeo yao. Kibaya zaidi wameiadhibu ile timu (Ruvu Shooting) mpaka kuishusha daraja. Baada ya kubaini hilo, tuliwafungia miezi 12 marefa wawili walioichezesha. Tulimfungia refa wa kati Amon Paul wa Mara na ‘Line One’ (Refa Msaidizi Namba moja), Martin Mwalyage wa Tabora,” alisema Chama na kueleza zaidi:
     
    “Tatizo la rushwa kwa marefa ni kubwa sana nchini ndiyo maana tumepanga kukabiliana nalo. Kwanza tumepanga kupunguza idadi ya marefa, tuwe na marefa wachache ambao tutawalipa vizuri. Tumepanga kuwalipa laki tano (Sh. 500,000 ambayo itakuwa mara mbili ya ilivyokuwa msimu uliopita) kwa kila mechi. 
     
    “Pia tumeandaa kanuni kali kuanzia msimu ujao. Mwamuzi anapewa rushwa, anavuruga mchezo, unaleta athari kubwa kama hiyo ya kuishusha timu daraja, halafu unamfungia mwaka mmoja. Huoni kwamba ni adhabu ndogo sana? Tumeliona hilo na kuamua tuwe tunawafuta jumla kwa kuwafungia maisha. Akichezesha ovyo, atafungiwa maisha, aende akalime nyanya au kufuga nguruwe.”
     
    MABADILIKO YA RATIBA
    Wadau wa soka waliozungumza na gazeti hili, walidai TFF imekuwa ikipanga matokeo kwa namna fulani kwa kuzibeba baadhi timu kutokana na kuzipangia ratiba nzuri ya mechi za ugenini mzunguko wa pili ambao umekuwa ukionekana mgumu kwa timu shiriki ikilinganishwa na ushindani unaokuwapo mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
     
    Katibu mkuu wa zamani wa Yanga, Abdul Sauko, alidai kuwa shirikisho hilo ndilo limekuwa likiharibu soka la Tanzania kwa kufanya mabadiliko ya mara kwa mara ya ratiba ya hiyo.
     
    Akitolea mfano msimu wa 2014/15, Sauko alidai ratiba ya mechi ya mzunguko wa pili kati ya Azam FC na Yanga ilibadilishwa kwa lengo la kuibeba Azam kuipiku Simba kumaliza nafasi ya pili katika msimamo wa ligi.
     
    “TFF ndiyo wameishusha Police Moro FC. Timu hii ilipaswa kucheza dhidi ya Yanga ambayo ilikuwa tayari imeshamalizana na Azam FC, lakini mechi ikapanguliwa ili kuwarahisishia kazi Azam wakutane na Yanga ambayo ilikuwa imeshacheza dhidi ya Police Moro na kutwaa ubingwa. Tunalipeleka wapi soka la Tanzania?” Alihoji Sauko.
     
    Kwa mujibu wa ratiba ya ligi hiyo msimu wa 2014/15, mechi ya Azam FC dhidi ya Yanga ilipaswa kuchezwa Aprili 4, lakini ikapigwa kalenda na TFF hadi Mei 5 huku Police Moro FC waliokuwa wacheze dhidi ya Yanga Mei 2 wakilazimika kuikabili timu hiyo Aprili 27.
     
    Baada ya Yanga kushinda 4-1 katika mechi hiyo na kutwaa taji la 25 la Tanzania Bara, timu hiyo ya Jangwani ilipoteza mechi zote mbili za mwisho wa msimu huo zilizofuata dhidi ya Azam (2-1) na Ndanda FC (1-0). Ushindi dhidi ya Yanga ndiyo uliiwezesha Azam kumaliza nafasi ya pili katika msimamo wa ligi na kufuta ndoto za Simba kushiriki michuano ya Afrika mwakani.
     
    RATIBA MECHI ZA UGENINI
    Sauko pia alidai kuwa ubingwa wa Azam FC katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2013/14 ulitokana na TFF kuipangia ratiba nzuri timu hiyo ya Wanalambalamba katika mechi za ugenini.
     
    “TFF wanaiogopa Azam FC, wanashindwa kuiambia ukweli. Msimu huu (2014/15) Azam ilitolewa mapema raundi ya kwanza ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika, lakini ndiyo timu iliyokuwa na mechi nyingi za viporo katika Ligi Kuu Tanzania kuliko Yanga ambayo ilifika hadi hatua ya 16 bora ya michuano ya Kombe la Shirikisho.
     
    “Angalia namna ilivyokuwa msimu uliopita (2013/14), Azam ilikuwa na mechi chache za nje ya Dar es Salaam mzunguko wa pili,” alisema.
     
    Madai ya Sauko yaliungwa mkono na Kocha Mkuu wa Mbeya City FC, Juma Mwambusi, ambaye aliishauri TFF kutorudia utaratibu wa kupangua ratiba za ligi misimu ijayo.
     
    “Kama kuna mashindano ya Afrika yanayosababisha ligi isimame, basi isimame kwa timu zote. Kwa kweli mabadiliko ya mara kwa mara ya ratiba msimu uliopita sikupendezwa nayo,” alisema Mwambusi.
     
    Kuhusu ratiba ya mechi za ugenini, Mwambusi alisema: “Unapocheza mechi nyingi mfululizo kwenye uwanja wa nyumbani, inaweza kukusaidia ukawa na nguvu nyingi ukapata pointi nyingi kuliko unapokuwa ugenini.”
     
    Mwambusi alisema kuna haja TFF kutoa mapema ratiba ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao ili ijadiliwe na wadau na kufanyiwa marekebisho mapema kabla ya kuanza kwa msimu ikiwa itakuwa na upungufu.
     
    Kwa mujibu wa ratiba ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2013/14, Azam FC ilicheza mechi tatu nje ya Dar es Salaam mzunguko wa pili. Mechi hizo zilikuwa dhidi ya Mgambo Shooting (Tanga), Ruvu Shooting (Mlandizi, Pwani) na Mbeya City FC (Mbeya).
     
    Mzunguko wa kwanza Azam FC ilicheza mechi sita nje ya jiji hilo zikiwamo tatu za mwanzoni mwa msimu ilizocheza ugenini mfululizo dhidi ya Mtibwa Sugar mkoani Morogoro Agosti 24, 2013, Rhino Rangers FC mjini Tabora Agosti 28, 2013 na Kagera Sugar FC mjini Bukoba Septemba 14, 2013.
     
    Yanga ambao ni mabingwa wa msimu uliopita, nao walipangiwa ratiba nzuri na TFF kwa mechi za ugenini. Timu hiyo ya Jangwani ilicheza mechi sita nje ya Dar es Salaam mzunguko wa kwanza dhidi ya Mtibwa Sugar (Morogoro), Stand United (Shinyanga), Kagera Sugar (Bukoba, Kagera), Police Moro (Morogoro), Coastal Union (Tanga) na Mbeya City (Mbeya).
     
    Ikiwa ni mbinu zilizile zilizodaiwa na Sauko kuibeba Azam FC msimu wa 2013/14, Yanga inayonolewa na Mdachi Hans van der Pluijm, ilipangiwa ratiba yenye mechi tatu za nje ya jiji hilo mzunguko wa pili msimu uliopita dhidi ya Prisons, Mgambo Shooting (Tanga) na Ndanda FC (Mtwara).
     
    KAULI YA YANGA, AZAM
    Kocha msaidizi wa Yanga, Boniface Mkwasa, alisema kinachoibeba timu yake kucheza mechi nyingi Dar es Salaam ni kitendo cha baadhi ya timu kutokuwa na viwanja vikubwa.
     
    “Yanga inakuwa na mechi nyingi Dar es Salaam kwa sababu hata inapocheza za ugenini dhidi ya JKT Ruvu na Ruvu Shooting, inakuwa kwenye Uwanja wa Taifa kwa sababu wapinzani wetu hao hawana uwanja mkubwa kwa ajili ya mechi zetu ambazo zinakuwa na mashabiki wengi,” alisema Mkwasa.
     
    Alidai kuwa Yanga imefanya vizuri msimu uliopita si kwa sababu ya upendeleo wa marefa na ratiba ya mechi za ugenini, bali kuwa na kikosi kizuri kilichoshinda mechi nyingi nyumbani na ugenini.
     
    Hata hivyo, kati ya mechi tano ambazo Yanga ilipoteza msimu uliopita, tatu zilikuwa za nje ya Dar es Salaam dhidi ya Mtibwa, Kagera Sugar na Ndanda.
     
    “Kitu ambacho mimi ninaona kuna upendeleo, ni baadhi ya timu kucheza mechi nyingi nyumbani mwishoni mwa msimu. Ushauri wangu kwa TFF ni kwamba mechi za mwisho zichezwe katika viwanja ‘neutral’ (timu zote zinazochuana zinakuwa mgeni kwenye uwanja husika). Mfano mechi ya mwisho wa msimu ya Ndanda dhidi ya Yanga ichezwe Mbeya badala ya Mtwara ili kuepusha majanga kama yaliyotokea Shinyanga,” alisema.
     
    Katika mechi ya mwisho ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita kati ya Stand United na Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga Mei 9, wenyeji Stand ambao walishinda 1-0, walidaiwa kuwahujumu wapinzani wao kwa kupuliza sumu katika vyumba vya kubadilishia nguo.
     
    Kwa mujibu wa Makamu wa Rais wa TFF, Wallace Karia, suala hilo linachunguzwa na vyombo vya dola na litatolewa ufafanuzi zaidi baada ya uchunguzi kukamilika.
     
    Baada ya kutafutwa na gazeti hili jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita, Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Azam FC, Saad Kawemba, alisema timu yao imekuwa inacheza mechi nyingi ndani ya jiji hilo kutokana na timu nyingi kutokuwa na viwanja.
     
    “Wizara ya Michezo ilipaswa kutoa ushahidi kwa kuzitaja timu zinazoshiriki katika kupanga matokeo. Waziri anapotoa kauli kama hiyo, tena kwenye chombo kikubwa kama Bunge, alitakiwa ahojiwe na kutoa ushahidi,” alisema Kawemba na kueleza zaidi:
     
    “Ikumbukwe kuwa Dar es Salaam na Pwani wana nusu ya Ligi Kuu Tanzania Bara. Yanga au Azam zinapocheza mechi ya ugenini dhidi ya JKT Ruvu zinakuwa Dar es Salaam kwa sababu JKT Ruvu haina uwanja, inatumia uwanja wa Azam. Inapocheza mechi ya nyumbani dhidi ya Azam inakuwa Azam Complex, maana yake Azam FC apata ‘advantage’ (faida) ya kuwa nyumbani wakati JKT ni mwenyeji.”
     
    Kuhusu mechi yao dhidi ya Yanga kusogezwa mbele, Kawemba alisema: “Azam hatuna mpango huo wa kupanga matokeo. Sisi ni ‘professional club’ (klabu yenye weledi) inayoendeshwa kwa misingi ya ‘professionalism’ (kiweledi).”
     
    “Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Simba (Geofrey Nyange ‘Kaburu’) ndiye Makamu wa Rais wa Simba na ndiye aliyepanga ratiba hiyo. Azam tulilalamika mno kuhusu ratiba ya mzunguko wa pili, lakini hatukusikilizwa. Tumecheza mechi nyingi ndani ya muda mfupi,” alisema zaidi Kawemba.
     
    KATIBU MKUU TFF
    Katika mahojiano na NIPASHE jijini Dar es Salam Ijumaa ya wiki iliyopita, Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa, aliiambia NIPASHE kuwa mabadiliko ya mara kwa mara ya ratiba ya Ligi Kuu Tanzania Bara hayakulenga kuzibeba baadhi ya timu, bali kupisha shughuli nyingine za kisoka za shirikisho hilo.
     
    “TFF haikuwa na lengo la kuzibeba Azam na Yanga. Mabadiliko ya ratiba yalitokana na kutofanyika kwa michuano ya Kombe la Chalenji na baadaye baadhi ya timu zikatakiwa kwenda Zanzibar kushiriki mashindano Kombe la Mapinduzi ambayo hatukuwa na uhakika wa kufanyika mwaka huu.
     
    “Mbaya zaidi, baada ya Kombe la Mapinduzi, kukawa na mechi za viporo za Azam na Yanga ambazo zilikuwa zinashiriki michuano ya kimataifa. Tunajipanga kuhakikisha Kamati ya Mashindano na Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) wanatoa ratiba ya msimu ujao ambayo haitaingiliana na ratiba za michuano mingine ikiwamo ya kimataifa ya CAF na Fifa,” alisema.
    CHANZO: MTANDAO WA IPP MEDIA
    https://play.google.com/store/apps/details?id=com.blog.ya.watanzania

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: Upangaji matokeo unavyolitafuna soka la Tanzania Rating: 5 Reviewed By: Unknown
    Scroll to Top