Geita. Kazi ya uandikishaji wapigakura imezidi kukumbwa na matatizo baada ya wananchi kuwafgungia waandikishaji ndani ya kituo kutokana na kupata taarifa kuwa muda uliopangwa kwa ajili ya mitaa ya Buhalahala, Kisesa na Moringe umekwisha, huku wakiwa hawajapata nafasi ya kusajiliwa.
Wakati vurugu hizo zikitokea, wananchi wa kata nne za wilayani Bukombe wanahofia kukosa nafasi ya kuandikishwa kutokana na maeneo yao kutoingizwa kwenye mfumo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), huku watu watatu, wakiwamo watoto wawili wilayani Hanang wakikamatwa kutokana na kujiandikisha mara mbili huku wakiwa hawajafikia umri unaotakiwa.
Tukio la Geita limetokea siku chache baada ya mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kuwataka wananchi mkoani Kilimanjaro kutoruhusu mashine zinazotumika kuandikishia wapigakura kwa njia ya kielektroniki (BVR) kuondolewa vituoni endapo kuna watu ambao hawajaandikishwa.
Uandikishaji mkoani Geita ulianza Juni 17, mwaka huu kwa kata tatu za Buhalahala, Mwatulole na Kalangalala na muda uliopangwa kumalizika ni juzi. Hali ilikuwa mbaya kwenye kata hizo baada ya wananchi kukaa vituoni hadi usiku wakisubiri kuandikishwa, na walipopata taarifa kuwa kazi hiyo haitaendelea kwa kuwa siku zilizopangwa zimemalizika, walichukua uamuzi huo wa kuzuia waandikishaji hadi watakapoandikisha wote waliokuwa wamesalia.
“Nimekuja hapa nina siku ya tano leo (juzi). Kila nikija sipati nafasi ya kuandikishwa wengine wanakesha vituoni siku ya tano, lakini hawajaandikishwa na leo ndiyo mwisho,” alilalamika mkazi wa Mwatulole, Marwa Ernest.
Mkazi mwingine, Neema Charles alisema:“Mwandikishaji anatuambia macho hayaoni, kwa hiyo sisi tufanyeje, tunataka kitambulisho kwani ndiyo cha msingi mwaka huu.”
Wananchi hao ambao walionekana kuwa na jazba, huku wakitishia kuchoma mashine kama wasingeandikishwa, walidai kuwa shughuli hiyo imetawaliwa na rushwa.
Hali hiyo ilikikumba kituo cha Shule ya Sekondari ya Kalangalala, ambako hadi saa 1:30 usiku mwandishi alishuhudia zaidi ya wananchi 200 wakiwa kituoni wengine wakipigana na kusukumana kila mmoja akitaka kuandikishwa.
“Hapa muda unaisha na leo (juzi) ndiyo mwisho, hatujui hatima yetu, wananchi wengi hatujaandikishwa, tumeshaomba tuongezewe mashine lakini hatusikilizwi zaidi tunashuhudia wenye fedha ndiyo wanaandikishwa,” alisema mkazi wa Kisesa, Mariana Peter.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Hellen Kahindi alikiri kuwapo kwa vurugu hizo na kwamba walikosea kuweka vituo pembezoni mwa mji, jambo lililosababisha wananchi wa mjini kukimbilia maeneo hayo wakihofia kutoandikishwa.
Alisema vurugu hizo zilisababisha magari mawili ya Serikali kuvunjwa vioo, huku waandikishaji wakiponea chupuchupu kutokana na kuwapo na vurugu kubwa eneo la kutokea hadi polisi walipoingilia kati.
“Tunashukuru hakuna madhara makubwa yaliyotokea kwa waandikishaji na vifaa, lakini tumejipanga kwa zoezi hili jipya ili matatizo hayo yasijitokeze kwani tumeongeza wino na kwenye mashine,” alisema Kahindi.
Wakati huohuo; wananchi wa Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, huenda wakashindwa kuandikishwa kutokana na kata zao nne kutowekwa kwenye mfumo wa utawala na hivyo kutotambulika na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Wakizungumza kwa nyakati tofauti juzi, maofisa wa kata hizo mpya za Katente, Katome, Bulangwa na Bulenga walisema maeneo yao hayamo kwenye mfumo wa NEC.
Ofisa mtendaji Kata ya Katome, Lukuba Shitwala alisema kutokana na kata yake kutokuwa kwenye mfumo huo, huenda zaidi ya wananchi 9,000 wakakosa kuandikishwa.
Hata hivyo, mkurungenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, James Ihunyo alisema tayari kata hizo zimeingizwa NEC, licha ya awali kutokuwamo, hivyo akawaomba watendaji kuhamasisha wananchi kujitokeza vituoni.
Watoto wajiandikisha Hanang’
Watoto wawili wenye umri wa miaka 15 wa Kijiji cha Nangwa, wilayani Hanang’ na mtu mwingine mmoja wilayani Babati mkoani Manyara wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kujiandikisha zaidi ya mara tatu huku wakiwa hawajafikia umri wa 18 unaotakiwa.
Mkuu wa mkoa wa Manyara, Joel Bendera alisema atahakikisha wote wanafikishwa mahakamani ili wachukuliwe hatua kali za kisheria kwa kuwa alishapiga marufuku watu kujiandikisha zaidi ya mara moja.
Mbali na watoto hao, mtu mwingine alijiandikisha mara tatu ni mkazi wa Boay wilayani Babati aliyetumia majina tofauti, akiitwa Petro Hhari kwenye kituo cha Shule ya Msingi ya Ditsoma A, Peter Tluway katika kituo cha zahanati na Peter Hary katika kituo cha ofisi ya kijiji hicho.
Mratibu wa BVR mkoani Manyara, Mwajabu Nyamkomola alithibitisha kupata taarifa za matukio hayo.
Mkuu wa wilaya ya Simanjiro, Mahamud Kambola alisema uandikishwaji unaendelea vizuri na wananchi wajitokeze.
Imeandikwa na Joseph Lyimo, Jackline Masinde na Ernest Magashi