https://play.google.com/store/apps/details?id=com.blog.ya.watanzania


.

.

.
  • Latest News

    .

    WASOMI, WANANCHI WAMSHUKIA KINANA


    Dar es Salaam. Kauli ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kuwa wabunge wa chama hicho wanaunga mkono kila hoja inayowasilishwa na Serikali bila kutathmini matokeo yake, imekosolewa na wasomi na wananchi waliosema amechelewa, huku wabunge wake wakikiri udhaifu.

    Kinana, ambaye tangu ateuliwe kushika nafasi hiyo amekuwa akikosoa utendaji wa mawaziri na maofisa wengine wa Serikali, juzi alipokuwa akihitimisha ziara zake mjini Mwanza, alikosoa hata mfumo wa CCM wa kumfanya Waziri Mkuu kuwa kiongozi wa wabunge.

    Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili wachambuzi hao walisema kuwa kauli hiyo imechelewa kwa kuwa hakuna dalili za chama hicho kubadilika kutokana na mifumo, utamaduni na utawala waliopitia viongozi wengi wa CCM.

    Profesa Mpangala: CCM iondolewe

    Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Rucu), alisema CCM inatakiwa ifanye vitu viwili ili kuwe na mabadiliko anayoyataka Kinana.

    “Cha kwanza itoke madarakani ili ikajipange upya, na cha pili kama itabaki madarakani ihakikishe inamchagua kiongozi shupavu asiyeyumbishwa na mifumo iliyopo ya chama,” alisema Profesa Mpangala.

    Alisema viongozi wa sasa wa CCM wamekuwa wakituhumiwa kwa rushwa, ufisadi tofauti na siku za nyuma alizosema hata kama rushwa ilikuwapo ilikuwa kwa kiwango kidogo.

    “Chama kimebadilika sana, kimekuwa na viongozi wabinafsi, wanaotaka maendeleo yao binafsi badala ya wananchi waliowachagua,” alisema.

    “Kauli ya Kinana inaonyesha wazi anataka mabadiliko na ni wazi kuwa chama hicho kinahitaji mabadiliko ambayo hayawezi kufikiwa bila kufuata hizo njia mbili. Watoke ili watambue walikuwa wanakosea wapi kwa kujifunza kwa wenzao watakaoshika dola au kwa dola nyingine, au wabaki kwa kumuweka kiongozi shupavu asiyeyumba.

    “Ninachokiona na kukisema wazi ni kwamba Kinana hawezi kukibadilisha chama kwa hatua kilichofikia... rushwa, ufisadi, umimi vimekuwa ndiyo dira. Viongozi wamepoteza mwelekeo, wamejisahau, wanahitaji muda wa kurekebisha walipokosea.”

    Mbunda: Wabunge CCM si makini

    Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Richard Mbunda aliungana na Kinana kukubaliana kuwa wabunge wa CCM si makini na ndio maana wanapitisha sheria ambazo ni kandamizi kwa wananchi.
    Alisema Serikali haiwajibiki badala yake inafanya maamuzi ya kubebana hata pale ambapo mambo yapo wazi na yanahitaji uwajibikaji ili wahusika wajifunze.

    “Ukitaka kuona kuna jambo halipo sawa ni pale ambapo vyama vya upinzani vinapiga kelele, chama tawala kinapiga kelele, kama hizo za Kinana. Walioshindwa kujituma sidhani kama wapo tayari kuelekezwa hasa kwa kipindi ambacho wapo mawindoni kusaka ushindi,” alisema Mbunda.

    “Kuzungumza ni suala moja na utekelezaji ni suala jingine, hususan mzungumzaji anapokuwa mmoja,” alisema. “Maoni yangu ni kusikia kwa ufasaha na ukamilifu nini kitafanyika ili kutoka huko kunakoitwa kupotoka na kuwatwisha wananchi mzigo kutokana na maamuzi ya wabunge wa chama tawala, ”alisema Mbunda.

    Dk Aneth Komba: Serikali siyo sikivu

    Mkuu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Dar es Salaam (Duce), Dk Aneth Komba alisema ipo wazi kuwa Serikali siyo sikivu na kwamba wabunge wamekuwa wakiambiwa kero mbalimbali lakini hakuna kinachofanyika.

    Alisema kuna vitu akiviona, kuvisoma na kuvisikia huwa anashangaa kama maeneo hayo yana wabunge kutoka chama tawala.

    Alisema kuna shule ambazo wanafunzi wanachangia darasa na ubao, huku kukiwa na mbunge anayehudhuria kila kikao cha bunge, lakini hatambui majukumu yake na kuacha mambo kama yalivyo.

    “Sijui hayo mengine, lakini hili la Serikali kutokuwa sikivu lipo wazi. Malalamiko yanatolewa kila kona, siyo kwenye elimu, afya, usafiri tu, bali kila nyanja ina malalamiko. Kama ingekuwa inasikia, bila shaka yangekuwa yamekwisha au kupungua,” alisema Dk Komba.

    Mgaya: Hakuna utekelezaji

    Katibu Mkuu wa Tucta, Nicolas Mgaya, alirejea katiba na ilani ya CCM na ilani ambazo alisema zimeweka wazi mambo ambayo chama kinatakiwa kuwafanyia wananchi, lakini akaongeza kuwa kwa bahati mbaya waliopewa majukumu, hawatekelezi.

    Alisema imefikia hatua watu wanaichukia Serikali kutokana na matendo ya viongozi waliopo madarakani kuwa si mazuri.

    “Serikali imeonekana dhaifu, inatekeleza dhuluma kwa wananchi. Ni kitu cha kawaida mwananchi kunyang’anywa ardhi, akapewa mwenye fedha hata kama katoka nje kwa sababu tu anazo. Hiyo inaonyesha ni kwa kiasi gani ilani ya CCM na katiba vimewekwa kapuni na viongozi na kila mtu anafanya analolitaka kwa maslahi yake,” alisema Mgaya.
    “Kiongozi mmoja akiingia anaongozwa na washauri, inategemea atapata ushauri wa aina gani na hao watakaompa watakuwa wamemlenga nani. Bila shaka alichokiona na kukisema Kinana itakuwa kwa manufaa yao, hivyo tunarudi kule kule. Hakuna usikivu wala kupinga, mzigo unakuwa wa mwananchi wa kawaida,” alisema Mgaya.

    Bashiru Ally: Hakuna vitendo

    Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bashiru Ally alisema uhusiano kati ya dhamira na vitendo ni tofauti hivyo Kinana anaweza kuwa na dhamira nzuri, lakini akashindwa kujitosheleza katika vitendo.

    Alisema kuwa dhamira ya kutaka kuirudisha CCM mikononi mwa wananchi inahitaji mapambano ya kweli kutoka kwa waliomo ndani ya chama.

    Alifafanua kuwa CCM ni taasisi ina watu wenye nguvu, wasomi, wenye maslahi yao ambao kwa hali yoyote lazima washirikishwe katika mapambano hayo, hivyo kazi ni ngumu kuipinga nguvu hiyo.

    “Sidhani kama Kinana anaweza kupambana na nguvu hiyo. Watu wapo kwenye chama kwa ajili ya maslahi yao na wanaweza kufanya lolote kuyalinda,” alisema Ally.

    Wabunge CCM wazungumza

    Mjini Dodoma, wabunge waliohojiwa na Mwananchi walikiri udhaifu huo wa kupitisha hoja za Serikali bila ya kutathmini athari zake, lakini wakasema hiyo inatokana na mfumo wa CCM.

    Mbunge wa viti maalumu, Diana Chilolo alisema kauli ya Kinana ni ya kweli, lakini akasema haitendi haki kwa wabunge ambao wamekuwa wakiwajibika ipasavyo.

    “Mfano mzuri hata mimi, jamani gazeti lenu ndilo ambalo limekuwa likieleza ukweli kuhusu niliyofanya kwa muda wote. Natengeneza taarifa zangu na kuibana serikali naibana kiukweli, hata sasa nimeshatuma taarifa yangu kwa katibu kuonyesha namna ambavyo nafanya kazi,” alisema Chilolo.

    Mbunge wa Mbongwe, Agustino Masele alikiri kuwapo na baadhi ya wabunge wasowajibika, lakini akajitetea kuwa hilo linatokana na mfumo mbovu uliopo CCM.

    “Tunaendesha Bunge kwa mazoea sana. Sasa mwenyekiti wa wabunge ni Waziri Mkuu na katibu wake ni (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu -Sera na Uratibu wa Bunge, Jenister) Mhagama. Ni kama bunge linaendeshwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, unafanyaje katika hilo,” alisema Masele.
    CHANZO: MWANANCHI
    https://play.google.com/store/apps/details?id=com.blog.ya.watanzania

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Post a Comment

    Item Reviewed: WASOMI, WANANCHI WAMSHUKIA KINANA Rating: 5 Reviewed By: Unknown
    Scroll to Top