Mrajisi wa Baraza la Wauguzi na Wakunga Zanzibar Haji Haji Khamis akieleza mchakato wa kulisajili Baraza la Wauguzi na Wakunga katika uzinduzi rasmi uliofanyika Chuo cha Sayansi ya Afya Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Mwenyekiti wa Baraza la Wauguzi na Wakunga Zanzibar Bi. Amina Abdulkadir akitoa maelezo ya kazi za Baraza hilo katika sherehe za uzinduzi zilizofanyika Chuo cha Sayansi ya Afya Mbweni .
Waziri wa Afya wa Zanzibar Rashid Seif akizungumza na wajumbe wa Baraza la Wauguzi na Wakunga Zanzibar kabla ya kulizindua rasmi huko Mbweni, Chuo cha Sayansi ya Afya.
Baadhi ya washiriki wakimsikiliza mgeni rasmi katika uzinduzi wa Baraza la Wauguzi na Wakunga Zanzibar kwenye sherehe za uzinduzi wa Baraza hilo.Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar.
Picha ya pamoja ya mgeni rasmi Waziri wa Afya Rashid Seif na wajumbe wa Baraza la Wauguzi na Wakunga mara baada ya uzinduzi rasmi.
Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar.
Na Ramadhani Ali/Maelezo Zanzibar
Waziri wa Afya wa Zanzibar Rashid Seif ameliagiza Baraza la Wauguzi na Wakunga Zanzibar kusimamia kwa karibu watendaji wa kada hiyo ili waweze kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.
Akizungumza katika uzinduzi rasmi wa Baraza Wauguzi na Wakunga katika Chuo cha Sayanzi ya Afya Mbweni, Waziri Rashid Seif amesema wauguzi na wakunga ni walezi wanaoshughulikia matatizo ya watu hivyo wanatakiwa kutekeleza wajibu wao kwa uadilifu.
Amesema wananchi wanapofika Hospitali na vituo vya Afya wanategemea hifadhi na kinga ya wauguzi kabla ya kuonana na daktari na kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi ambayo yanahitaji kutafutiwa ufumbuzi na Baraza hilo.
Waziri wa Afya amelitaka Baraza kuwa karibu na kuwafuatilia wauguzi na wakunga kwenye vituo vyao vya kazi ili kuhakikisha kada hiyo inajengewa heshma yake inayostahiki.
Amesema kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa mama wajawazito wanapofika vituo vya afya kujifungua na baadhi yao hukataa kujifungua kwenye vituo hivyo kwa kuogopa kunyanyaswa na wakunga na wauguzi.
Amelishauri Baraza kufuatilia kwa karibu vyuo vinavyosomesha afya ya binaadamu na kuhakikisha vyuo hivyo vimesajiliwa rasmi na vinawataalamu wa fani hiyo na wanafunzi wanaojiunga wanazo sifa zinazotakiwa ili kutoa wauguzi wenye viwango vya taaluma hiyo.
Mwenyekiti wa Baraza la Wauguzi na Wakunga Zanzibar Bi. Amina Abdulkadir amemueleza Waziri wa Afya kwamba Baraza hilo litatekeleza wajibu wake wa kusimamia wafanyakazi wa kada hiyo na halitakuwa na muhali kwa mtu ama taasisi itakayokwenda kinyume na maagizo yake.
Amesema miongoni mwa kazi kubwa za Baraza la Wauguzi na Wakunga ni kulinda afya za raia, kuweka viwango katika maadili na utendaji wa wauguzi katika kutoa huduma bora na kuhakikisha wauguzi wote wana elimu inayoendana na teknolojia ya kisasa.
Amemuhakikishia Waziri kwamba Baraza litaanza kazi zake mara moja kwa kuwasajili wauguzi wote wenye sifa na wale ambao wataonekana wanadandia watakuwa hawana nafasi.
Baraza la Wauguzi na Wakunga limeundwa kwa sheria No.5 ya mwaka 2014 na ilipitishwa na Baraza la Wawakilishi tarehe 22 Oktoba na linawajumbe 13 kutoaka Taasisi za Serikali na Taasisi binafsi .