Kocha wa Manchester United mholanzi Loius Van Gaal amesema kuwa pamoja na kufungwa katika mechi dhidi ya Swansea, magoli 2-1 haileti tija ya yeye kupaniki na kusajili wachezaji katika siku hizi mbili za mwisho za usajili.
Akiongea mara baada ya mchezo huo wa Swansea, Van Gaal amesema siku zote ni lazima upime ubora wa mchezaji unaemtaka kwa kipindi cha mwezi mmoja ama zaidi, na kwamba usajili wa kupaniki hauna tija wala msaada kwa timu na mwisho ni hasara.
Katika mchezo huo, Van Gaal anasema kila mtu aliona namna United walivyokua wakimiliki mpira, lakini akasisitiza kosa lao kubwa ni kutotumia nafasi kufunga magoli na kuzuia wasifungwe.
Javier Hernandez ‘Chicharito’ na golikipa David De Gea walikaa nje na kuhusu hilo Van Gaal akakataa kuzungumza chochote kwa madai kuwa hawezi kujibu maswali ya aina moja kila wakati.
Mashabiki na wadau wa soka mbalimbali wamekua wakizungumzia suala la Manchester United kusajili mshambuliaji mpya kikosini kutokana na kutoridhishwa na uwezo wa nahodha wao Wayne Rooney aliyepewa mikoba ya kucheza kama mshambuliaji msimu huu.
Hata hivyo mara kadhaa Van Gaal amekua akisisitiza kuwa hawana shida ya kutafuta mshambuliaji mpya na kwamba mambo yatakaa sawa muda ukifika.
Suala la golikipa David de Gea, bado hakijafahamika mustakabali wake kuhusu kuhamia Real Madrid na kwamba inasubiriwa kuona nini kitatokea katika siku mbili hizi za mwisho za usajili wa dirisha la usajili barani ulaya.
0 comments:
Post a Comment