Mchezaji na nahodha wa timu ya
Mbeya City Juma Nyoso ameendelea kufanya vitendo ambavyo si vya
kiungwana na vinavyohitaji kupingwa kwa nguvu zote kwenye soka si la
Tanzania pekee bali duniani kote ambako mchezo huu unachezwa.
Nyoso amemfanyia kitendo cha
udhalilishaji mchezaji na nahodha wa Azam FC John Bocco ‘Adebayo’ wakati
wa mchezo wa timu ya Azam FC dhidi ya Mbeya City uliochezwa kwenye
uwanja wa Azam Complex, Chamazi ambapo Azam FC waliiibuka na ushindi wa
goli 2-1.
Kitendo kilichofanywa na Juma
Nyoso ni cha kulaaniwa na kupigwa vita kwasababu kinaharibu maana halisi
ya mchezo wa soka ambao ni wa kistaarabu unaochezwa na waungwana
wapenda amani lakini kwa beki huyu wa Mbeya City haiko hivyo.
Msimu uliopita Nyoso alimfanyia
kitendo kama alichokifanya leo kwa John Bocco aliyekuwa mshambuliaji wa
Simba kwa wakati huo Elius Maguri ambaye kwa sasa anakipiga Stand United
ya Shinyanga. Mazingira ya matukio hayo mawili yanafanana kwa asilimia
nyingi.
Beki huyo wa zamani wa Simba SC
alifanya tukio hilo wakati mpira ukiwa umesimama kama ilivyokuwa kwa
Maguri msimu uliopita. Tukio la kumdhalilisha Maguri lilipelekea Nyoso
afungiwe kucheza mechi nane za ligi kuu Tanzania bara.
Nyoso akifanya tukio la udhalilishaji dhidi ya Elius Maguri msimu uliopita wakati Maguri akicheza kwenye klabu ya Simba SC
Nyoso aliomba radhi kwa kamati ya maadili ya TFF na kwa Maguri pia lakini aliahidi kuorudi kitendo kama hicho kwa siku zijazo.
Lakini ukiwa ni msimu mmoja tu
umepita tangu Nyoso apewe adhabu kwa kosa la kumdhalilisha Maguri, leo
amerudia kosa lilelile kwa mazingira yaleyale akiwa amevaa kitambaa cha
unahodha wa timu ileile.
Hapa napata mashaka na tabia za
Nyoso na kujiuliza maswali mengi kichwani moja ya maswali hayo ni kama
Juma Nyoso yuko timamu kichwani au la! Nadhani pia anahisi ufahari au
ushujaa kufanya vitendo visivyokubalika kwenye soka.
Napata mashaka pia na malezi
pamoja na mazingira aliyolelewa Nyoso kutokana na vitendo vyake ambavyo
naweza nikaviita ni vya ajabu. Haiwezekani mchezaji yuleyule akafanya
vitu vilevile ndani ya muda mfupi huku akiwa ametoka kwenye adhabu ya
kosa kama hilo ndani ya miezi michache iliyopita.
Si dhani kama mtu huyu anastahili
hata kuvaa kitambaa cha unahodha wa timu kwasababu nahodha ni kiongozi
wa wachezaji ndani na nje ya uwanja. Sijui anawaonesha wachezaji wa
Mbeya City na watanzania kuwa yeye ni kiongozi wa aina gani.
Awali alifungiwa mechi nane na
kusababisha kuyumba kwa timu yake kwasababu inamtegemea kwa kiasi
kikubwa uwanjani. Timu hii ndiyo inatoa mshahara kumlipa mchezaji huyu
ambaye kukosekana kwake uwanjani kwasababu za kijinga kunapelekea timu
kufanya vibaya.
Nyoso ni mchezaji mwenye mzoefu
na amecheza timu kubwa pamoja na timu ya taifa, amecheza mechi nyingi za
kimataifa na anajua maana ya kuwa mzoefu kwenye timu. Hatukutegemea
vitendo kama hivi vifanywe na mtu kama yeye tena mara mbili kwa watu
tofauti.
Ili kulinda nidhamu ya soka na
wachezaji, TFF inabidi ichukue hatua kali na za haraka kwa Nyoso
kwasababu si kitendo cha kwanza kufanywa kwa mchezaji huyo. Safari hii
adhabu iwe kali zaidi ili kuzuia tambia chafu kama hizi zinazolishusha
soka letu ambalo watu wanapambana kusogea mbele lakini wengine
wanatuvuta nyuma.
Nampongeza Rais wa TFF Bw. Jamal
Malinzi kwa kuwa mtu wa mwanzo kabisa kulikemea jambo hili kupitia
account yake ya twitter mara baada ya kuona kitendo kilichofanywa na
Nyoso na kuahidi kuchukua hatua kali kwa mhusika wa tukio hilo.


0 comments:
Post a Comment