Na Baraka Mbolembole
Mfungaji bora wa ligi kuu ya
Uganda, Hamis Kiiza amejitofautisha msimu katika ufungaji. Akiwa na
klabu yake mpya, Simba SC, Mganda huyo tayari amefunga magoli matano
kati ya sita ya timu yake katika michezo mitatu ya ligi kuu Tanzania
bara msimu huu.
MAGOLI MA3 YA KICHWA
Kiiza, 25 aliisaidia Simba
kushinda kwa mara ya kwanza ndani ya miaka mitatu katika uwanja wa
Mkwakwani, Tanga. Alikuwa mchezaji wa kwanza wa Simba kufunga katika
michezo 7 ambayo Simba ilizikabili Coastal Union, JKT Mgambo na African
Sport katika nyakati tofauti ndani ya miezi 36. Alifunga dakika ya 67′
akiunganisha kwa kichwa krosi ya mshambuliaji mwenzake, Musa Hassan
Mgosi wakati Simba iliposhinda 1-0 dhidi ya African Sports, Septemba 12.
PASI YA IBRAHIM AJIB
Wakati Simba ikiongoza 1-0 na
mechi ikiwa 50/50, kocha wa Simba, Muingereza, Dylan Kerr alimuinua
Kiiza katika benchi kuchukua nafasi ya kiungo-mshambulizi, Mwinyi
Kazimoto, Mganda huyo hakuchua dakika nyingi sana kufunga na kuifanya
timu yake kuwa mbele kwa magoli 2-0 dhidi ya JKT Mgambo, Septemba 16
katika uwanja huohuo wa Mkwakwani, Tanga na kuisaidia timu yake kushinda
mechi ya pili mfululizo. Goli hili alifunga dakika ya 73′ kwa mguu wa
kushoto akimalizia pasi ya mshambulizi mwenzake kijana Ibrahim Ajib.
DAKIKA YA 30′, 46′, 9O’, ‘ HAT-TRICK’ YA KWANZA SIMBA, ‘ HAT-TRICK’ YA KWANZA VPL
Simba iliwapumzisha kabisa
wachezaji wake, nahodha, Mgosi na mlinzi wa kati, Mganda, Juuko Murishid
katika mchezo wao wa tatu dhidi ya Kagera Sugar jana Jumapili, mlinzi
wa kulia, Hassan Kessy na kiungo-mshambulizi, Kazimoto walianzia katika
benchi lakini bado ushindi wa asilimia 100 uliendelezwa na Kiiza ambaye
alifunga magoli matatu kwa mpigo ‘hat-trick’ kwa mara ya kwanza akiwa
mchezaji wa Simba msimu huu.
Mabao hayo matatu kwa mpigo ni
‘majibu mengine mabaya’ upande wa mahasimu wao Yanga SC ambao walimtema
takribani miezi 18 iliyopita ili tu asajiliwe mshambulizi ‘aliyechemsha’
Mbrazili, Geilson Santos ‘Jaja’. Alifunga kwa kichwa dakika ya 30′
akimalizia krosi ya mlinzi wa kushoto, Mohamed Hussein, akafunga tena
kwa kichwa dakika ya 46′ akiunganisha krosi-pasi ya kiungo, Awadh Juma.
Magoli yote hayo mawili alifunga
akiwa ‘huru’ bila uwepo wa walinzi wa Kagera Sugar. Goli lake la tatu
alifunga dakika ya 90′ kwa mguu wa kulia akimalizia pasi ya kiungo,
Kazimoto. Nani anafuata baada ya mshambulizi huyo kufunga ‘hat-trick’
yake ya kwanza katika ligi kuu bara?. Hakuwahi kufanya hivyo akiwa
Yanga.
0 comments:
Post a Comment