Na Baraka Mbolembole, Dar es Salaam
Asikudanganye mtu, hakuna timu iliyo tayari kumvumilia kocha asiye na matokeo mazuri. Muingereza Stewart Hall amerejea kwa mara ya tatu kama mwalimu mkuu wa Azam FC. Hall aliifundisha Azam kwa mara ya kwanza kuanzia Januari, 2011 mara baada ya kumalizika kwa michuano ya Mataifa ya Ukanda wa CECAFA Disemba, 2010. Hall alikuwa mkufunzi wa timu ya Taifa ya Zanzibar kabla ya kutua Azam FC.
Azam chini ya Muingereza huyo ikamaliza katika nafasi ya tatu nyuma ya Yanga na Simba kwa tofauti ya alama 6. Msimu wa 2011/12 Hall alikuwa karibu kuisaidia klabu hiyo kushinda ubingwa wa kwanza wa ligi kuu. Alishinda gemu mbili dhidi ya Yanga, moja dhidi ya Simba huku akitoa sare gemu moja. Licha ya kukusanya alama kumi kwa vigogo hao, Hall aliathirika na matokeo dhidi ya timu ndogo.
Alifukuzwa kazi mara baada ya Azam kufungwa katika mchezo wa fainali ya Kagame Cup dhidi ya Yanga, Julai, 2012 lakini aliweza kuisaidia timu hiyo kuingia ‘ Top two’ kwa kuwaangusha Yanga katika ligi kuu. Alifukuzwa kwa sababu zisizo za kimpira kwa kuwa tu alimpanga Ngassa licha ya ‘mmiliki wa timu’ kuagiza mchezaji huyo asipangwe katika mchezo wa fainali kwa kuwa alibusu nembo ya Yanga pia akivaa jezi ya klabu hiyo baada ya kufunga/kumalizika kwa gemu ya nusu fainali ya Kagame kati ya Azam FC na Vita Club.
Alijiunga na Sofa Paka ya Kenya na huko alikaa kwa miezi mitatu tu na kurejea Azam FC kuchukua nafasi ya mwalimu Mhindi, Boris Bunjak ambaye licha ya kupoteza gemu mbili tu katika mzunguko wa kwanza msimu wa 2012/13 mwalimu huyo aliondolewa kwa kilichoitwa ‘wachezaji kumuhitaji zaidi Hall’. Muingereza huyo aliisaidia Azam kufika hatua ya 16 bora ya michuano ya Shirikisho Afrika huku Azam ikimaliza tena katika nafasi ya pili katika ligi kuu safari hii wakiipiga kumbo Simba.
Miaka yote miwili ambayo Azam ilimaliza nafasi ya pili katika ligi kuu ilizidiwa pointi 6 na Simba msimu wa 2011/12 na Yanga msimu wa 2012/13 hivyo Hall aliweka mikakati kwa kushirikiana na timu nzima ya utawala na wachezaji kuwa wanapaswa kufikisha alama 59-61 ili washinde ubingwa kwa kuwa Yanga na Simba walichukua ubingwa wakiwa na alama zisizozidi 60.
Alianza msimu wa 2013/14 kwa sare mfufulizo na kufikia gemu ya Yanga mwezi Novemba tetesi za kufukuzwa kwake kazi zilipamba ‘moto’. Hall alitoa machozi mara baada ya kinda Joseph Kimwaga kuifungia timu yake goli la ushindi katika mchezo huo ambao ulimalizika kwa Yanga 2-3 Azam. Hall alikuwa amesalitiwa hata na baadhi ya wachezaji wake ambao walikuwa wakicheza chini ya kiwango kwa maelekezo ili afukuzwe kazi.
Aliachia kazi yake mara baada ya kumalizika kwa mkataba wake wa mwaka mmoja Disemba 2014 na nafasi yake ikachukuliwa a Mcameroon, Joseph omog ambaye aliisaidia timu hiyo kushinda ubingwa wa kwanza wa ligi kuu bara. Omog alifukuzwa kazi mapema mwaka huu baada ya Azam FC kuondolewa katika raundi ya awali ya klabu bingwa Afrika.
Hall tayari ameshinda ubingwa wa Kagame Cup, Julai mwaka huu amewasaini wakali wa Kimataifa kama Jean Mugiraneza, Allan Wanga, Ame Ally, Ramadhani Singano, huku akiwa na kina John Bocco, Didier Kavumbagu, Kipre Tchetche, Kipre Bolou, Paschal Wawa, Salum Abubakar, Himid Mao, Farid Musa, Mudathir Yahya, Kelvin Friday, Hamis Mcha, Shomari Kapombe, Mwadini Ally, Aishi Manula, Erasto Nyoni n.k Hall hatakuwa na sababu ya kuvumiliwa endapo timu itavurunda.
Ataanza na Tanzania Prisons timu ambayo haijapoteza mchezo wowote kati ya minne waliyocheza na Azam FC katika misimu miwili iliyopita. Watacheza mchezo wa pili wakiwa ugenini dhidi ya Stand United ya Shinyanga kisha wataifuata Mwadui FC kabla ya kurudi Dar es Salaam kuivaa Mbeya City. Hall atapita njia gani? Ni jambo la kusubiri na kuona.


0 comments:
Post a Comment