
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia
salamu za Rambirambi Waziri Mkuu Mheshimiwa Mizengo Peter Kayanza Pinda,
kufuatia kifo cha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma Mheshimiwa Celine Ompeshi Kombani.
“Pokea
rambirambi zangu za dhati, sote kwa pamoja tumepoteza mama mchapakazi,
hodari na aliyependa kushirikiana na wenzake katika kazi zake, hakika
tutamkumbuka siku zote” Rais Amesema.
Rais Pia
amemtumia salamu za pole mume wa marehemu Kombani, Bwana Swaleh Ahmad
Pongolani, watoto, ndugu na jamaa wa Mama Kombani.
“Nimepokea
taarifa za kifo cha mama Kombani kwa huzuni kubwa, najua machungu na
maumivu mliyonayo kwa kuondokewa na kiungo muhimu katika familia yenu,
poleni sana, mama ni nguzo ya familia, niko nanyi katika msiba huu mzito
kwenu” Rais ametuma salamu hizo kwa Mume wa Marehemu Celine, Bwana
Pongolani, watoto, wajukuu na ndugu wa Marehemu mama Kombani.
Rais
amesema pamoja na kwamba kifo hakiepukiki, bado ni kitu ambacho
kinashtua, kuhuzunisha na kuleta unyonge mkubwa kwa wafiwa katika jamii.
Marehemu
Kombani pia alikua ni mgombea ubunge wa jimbo la Ulanga Mashariki kwa
tiketi ya Chama Cha Mapinduzi, ambapo amekwisha kulitumikia jimbo hilo
kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita.
“Naungana
nanyi katika kipindi hiki kigumu kumuombea Mama Kombani ili mwenyezi
Mungu ampe mapumziko mema ya Milele” Rais amesema na kuwaombea wana
familia na ndugu wa Marehemu “Mwenyezi Mungu awatie nguvu, awape
uvumilivu na subira katika kipindi hiki”.
“Niko
nanyi katika kipindi hiki kigumu kwa hali na mali, nawaomba msijisikie
wapweke” Rais amesema na kuwatakia utulivu na amani katika kipindi hiki
cha msiba mkubwa kwa familia ya mama Kombani
Marehemu
Mama Kombani amefariki jana tarehe 24 Septemba, 2015 nchini India ambapo
alikua anapatiwa matibabu baada ya kugundulika kuwa na kansa.
Marehemu Kombani alizaliwa Juni 19, 1959 ameacha Mume, watoto watano na wajukuu wanne.
Mwili wa marehemu unatarajia kuwasili nchini kesho mchana na anatarajiwa kuzikwa Mkoani Morogoro katika shamba lake.
Mungu ailaze Roho ya Marehemu Celine Kombani mahali Pema Peponi, Amina.
Imetolewa na:
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais, Msaidizi,
Ikulu-DSM.
25 Septemba, 2015


0 comments:
Post a Comment