RAIS
Mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa( katikati) akiwa ameongozana
na Waziri wa Kazi na Ajira, Bi. Gaudensia Kabaka (wa kwanza kulia), Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Dk. Ramadhan Dau, Meneja
Miradi wa Shirika hilo Muhandisi John Msemo (watatu kushoto)
alipotembelea mradi wa ujenzi wa Daraja la Kigamboni kwa mualiko maalum
kutoka NSSF mwishoni mwa wiki. Wengine ni maafisa wa serikali na NSSF.
RAIS
Mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa( katikati) akipokea maelezo
kuhusu mradi wa ujenzi wa Daraja la Kigamboni kutoka kwa Meneja Miradi
wa shirika hilo Muhandisi John Msemo (kulia kwake) alipotembelea ujenzi
huo kwa mualiko maalum kutoka NSSF.
Muonekano wa Daraja kwa sasa.
RAIS
Mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa (katikati) akiwa kwenye picha
ya pamoja na Waziri wa Kazi na Ajira, Bi. Gaudensia Kabaka (wan ne
kulia) pamoja viongozi na maofisa wa Shirika la NSSF wakiongozwa na Mkurugenzi
Mkuu wa Shirika la hilo, Dk. Ramadhan Dau (kulia kwake) alipotembelea
moja ya miradi ya nyumba za makazi zinazojengwa na shirika hilo eneo la
kigamboni.
Na Mwandishi wetu
Dar es Salaam, 11th, Oct, 2015: RAIS Mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa amempongeza rais anayemaliza muda wake Jakaya Kikwete pamoja na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF)kwa kusimamia utekelezaji wa ujenzi wa daraja la Kigamboni linalotarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu.
Mradi
wa daraja hilo lenye urefu wa mita 680, unaogharimiwa kwa pamoja kati
ya mfuko wa NSSF na serikali kwa gharama ya Dola za Kimarekani Milioni
143.5 (Sh. Bilioni 248), ulipangwa kumalizika ndani ya miezi 36
tangu kuzinduliwa kwake mwezi Septemba mwaka 2012.
Akizungumza
mara baada ya kupokea taarifa ya kina kuhusiana na mradi huo jana
jijini Dar es salaam alipotembelea daraja hilo kwa mwaliko maalum kutoka
NSSF, Mh. Mkapa alisema uamuzi wa kutekeleza mradi huo ni wa kijasiri
kwa kuwa unahusisha kiasi kikubwa cha rasilimali fedha na muda.
“Pia
kitendo cha Rais Kikwete kutoogopa kutumia nguvu za nje ya serikali
yake ili kufikia malengo ya kimaendeleo ndio chachu ya mafanikio kama
haya…ningependa sana kuona daraja hili likizinduliwa na Rais Kikwete
mwenyewe,’’ alisema Mh. Mkapa.
Awali
akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Meneja Miradi wa NSSF
Muhandisi. John Msemo alisema kwa sasa ujenzi wa daraja hilo umekamilika
kwa asilimia 94 huku akibainisha kuwa zimebaki mita 25 ili kuunganisha
kabisa daraja hilo.
“Awali
mradi ulipangwa ukamilike Januari mwaka huu lakini kutokana na
changamoto zilizojitokeza, ujenzi utakamilika mwishoni mwa mwaka huu na
daraja litaanza kutumika mapema mwezi wa kwanza hapo mwakani,’’ alisema.
Kwa
mujibu wa Muhandisi Msemo, wakati wa kusimika nguzo zinazoshikilia
daraja hilo, ilibainika kuwa umbali wa mita 56 kutoka sakafu ya bahari
kulikuwa na uwazi ambao ungeathiri daraja hilo.
“Wataalamu
ilibidi kusimama kwa muda kwa ajili ya kuziba uwazi huo, hivyo
imesababisha kalenda ya mradi kubadilika ili tuweze kufanya kazi yenye
ubora,” alisema huku akizitaja changamoto nyingine kuwa ni pamoja na
kesi za fidia kwa wakazi waliokuwa wanaishi eneo la mradi, majaribio ya
migomo ya wafanyakazi pamoja na malighafi za ujenzi kupatikana mbali na
eneo la ujenzi.
Hata
hivyo alisema kukamilika kwa mradi huo kutazaa changamoto kadhaa ambazo
zinatakiwa kufanyiwa kazi na serikali mapema zikiwemo suala la
msongamano wa magari kwenye makutano ya barabara za Kilwa
–Mandela, Nyerere-Mandela, Veta Chang’ombe-Kawawa pamoja na uduni wa
barabara unganishi zikiwemo zile za Vijibweni-Mji Mwema pamoja na
Gerezani- Ohio.
“Lakini
pia faida kubwa zaidi ambayo kama taifa tumeipata kwenye mradi huu ni
pamoja na suala la uzoefu wa kusimamia na kuendesha miradi ya namna hii
ambapo wataalamu wetu wengi wa ndani wameelimika kiasi cha kutosha
kuweza kusimamia miradi ya namna hii…Kifupi kama taifa tunao wataalamu
wa kusimamia ujenzi wa daraja la Dar es Salaam –Zanzibar muda ukifika,’’
alibainisha.
Kwa
upande wake Waziri wa Kazi na Ajira, Bi. Gaudensia Kabaka alitoa wito
kwa wahandisi wa mradi huo kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi huo
huku pia wakiangalia namna itakayomuwezesha Rais Jakaya Kikwete kufanya
uzinduzi wa daraja hilo (Soft Opening) kabla hajamaliza muda wake.
Kwa
upande wake pia, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa NSSF, Dk. Ramadhan Dau
mbali na kumshukuru Mh Mkapa kwa kuasisi Mradi huo mwaka 2002alisema
daraja hilo likikamilika litaweza kuinua uchumi wa eneo la Kigamboni na
kuwa sehemu nzuri ya uwekezaji, hivyo aliwataka wananchi kulitumia
kikamilifu kwa ajili ya maendeleo yao.
Mbali na
daraja hilo Mh Mkapa pia alipata wasaa wa kutembelea miradi mingine
inayotekelezwa na mfuko huo ikiwemo ile ya ujenzi wa nyumba za makazi
eneo la Kijichi na ule wa ‘Dege Eco village’ yote ikiwa eneo la
Kigamboni.
0 comments:
Post a Comment