Kundi la muziki wa kizazi kipya
la Tip Top Connectons lenye maskani yake Manzese jijini Dar es Salaam,
leo limekabidhi vifaa vya michezo kwa timu shiriki za michuano ya
Magufuli Cup #Hapa Kazi Tu, mashindano yanayotarajiwa kuzinduliwa rasmi
Ijumaa (kesho) kwa mchezo kati ya Abajalo SC dhidi ya Zakhem SC kwenye
uwanja wa Mwl. Nyerere Makurumla.
Vifaa vilikabidhiwa kwa timu hizo
ni pamoja na jezi, mipira na vifaa vingine kwa ajili ya wachezaji na
waamuzi ambao watakuwa wanachezesha mashindano hayo.
Michuano hiyo ambayo
itashirikisha jumla ya timu nane itaanza kutimua vumbi rasmi kesho na
Mgombea Ubunge jimbo la Kinondoni kupitia tiketi ya Chama cha Mapinduzi
(CCM) Idd Azan anatarajiwa kufungua mashindano hayo.
Akikabidhi vifaa hivyo kwa timu
shiriki za mashindano hayo katibu wa mashindano wa Chama cha Mpira wa
Miguu mkoa wa Daes Salaam (DRFA) Daudi Kanuti amesema anatarajia kuona
mashindano hayo yakifanyika kwa amani na utulivu kama malengo
yalivyokusudiwa.
“Naamini timu zote zitacheza
mpira na tutapata bingwa wa mashindano haya kwa uwezo na si vinginevyo.
Kikubwa katika michuano hii ni kujenga ushirikiano na umoja miongoni mwa
vijana na kutunza amani hasa katika kipindi hiki tunapoelekea kwenye
uchaguzi mkuu”, amesema Kanuti.
Mashindano hayo yameandaliwa kwa
lengo la kuwakutanisha vijana ambao wanacheza soka hususan soka la
mchangani na kuwapa fursa ya kuonekana na kuonesha vipaji vyao pamoja na
mashabiki wa soka kushuhudia burudani na vipaji toka kwa wachezaji
mbalimbali lakini pia kulinda amani katika kipindi hiki kuelekea
uchaguzi mkuu.
Magufuli Cup ni michuano ambayo
itashirikisha timu nane toka vitongoji mbalimbali vya jiji la Dar es
Salaam. Timu hizo ni Abajalo SC, Tuamoyo, Goms United, Friends Rangers,
Zakhem SC, FC Kauzu, Burudani SC, pamoja na Faru Jeuri.
0 comments:
Post a Comment